loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mradi wa kumaliza vifo kwa wanawake, watoto waimarika

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee anasema Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo wa Mkakati wa Kitaifa wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya akinamama wajawazito, vichanga wanaozaliwa na watoto (One Plan, 2008).

“Mradi huu ulilenga kuhudumia wanawake elfu 70 lakini mpaka tunapozungumza ndugu mwandishi wa habari mradi huu umewafikia zaidi ya wanawake 74,099,” anasema Mdee katika mazungumzo kwa njia ya simu.

Naibu Mkurugenzi huyo wa NHIF, ambayo ndiyo inashirikiana na benki hiyo ya Ujerumani katika kufanikisha mradi huo anasema kupitia mradi huo kiasi cha Shilingi milioni 644 kimelipwa kwa vituo vya matibabu vya mikoa ya Mbeya na Tanga vilivyotoa huduma kwa akinamama wajawazito.

“Tulipanga katika mradi zaidi ya bilioni 6 kulipwa, tumelipa kiasi hicho kidogo sana,” alisema Mdee na kuongeza kwamba halmashauri nyingi zimeonekana kutofuatilia fedha hizo na hivyo kukwamisha malengo ya mradi wenyewe. Aidha anasema Sh 400,443,000 zimetumika kulipia familia za wanawake wajawazito ili kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo kuwezesha Halmashauri 17 za mikoa ya Mbeya na Tanga kuomba fedha za Tele kwa Tele kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Chanzo cha mradi Chanzo cha mradi huu ni ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Ujerumani, ushirikiano ambao katika miaka ya 2006/07 ulizaa ushirikiano kati ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani.

Awali Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za Kijerumani likiwemo Shirika la GiZ ambalo wamekuwa na msaada mkubwa katika maendeleo ya mradi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Kaimu Mkurugenzi wa CHF, Rehani Athumani anasema kwamba kuanzishwa kwa programu hiyo kumelenga pia kuangalia namna ya kuwawezesha akinamama wajawazito wasio na uwezo kupata huduma bora za matibabu wakati wa ujauzito katika kipindi chote cha miezi 9 cha ujauzito.

“Huduma hizi ni zilezile wanazopata wanachama wote wa NHIF. Tunaamini kwamba kwa kuhakikisha kuwa huduma hizi wanazipata wanawake wajawazito na watoto tutakuwa tunatengeneza taifa ambalo lina afya na lipo tayari kwa uzalishaji wa uchumi kutokana na kuwepo kwa afya bora,” anasema Athumani.

Aidha anasema kuwa lengo jingine la mradi huo ni kumuwezesha mama mjamzito na kichanga kilichozaliwa kupata huduma za matibabu za NHIF hata baada ya mtoto huyo kuzaliwa, hivyo huduma za NHIF ni kwa mwaka mzima wa kwanza. Pia madhumuni mengine katika mradi huo ni kuziwezesha familia za akinamama wajawazito kupata huduma za CHF katika mwaka wa pili baada ya kuwa mama na mtoto wamepata huduma hizo katika mwaka wa kwanza.

Katika mwaka wa pili, kaya nzima inapata huduma za matibabu CHF. Ukubwa wa mradi Katika hotuba yake wakati anakabidhi vifaa tiba vya mradi huo mjini Mbeya, Dk Rashid alisema kwamba mradi huo ulianza katika mikoa ya Tanga na Mbeya na baada ya kuonesha mafanikio makubwa sasa umeongezwa mikoa miwili ya Lindi na Mtwara.

Kuongezwa kwa mikoa hiyo, bila kumung’unya maneno unaona kuwa ni jitihada za kutumia vyema fedha za mradi zipatazo Shilingi bilioni 6 ambazo mikoa ya Tanga na Mbeya katika kipindi cha miaka miwili ya mradi zimeshindwa kutumika.

Naibu Waziri aligusia kwa namna ya diplomasia kuhusu suala la halmashauri nyingi kutofuata utaratibu wa kuomba fedha. Alisema kwamba kitendo cha Halmashauri za wilaya kutowasilisha madai yao ili walipwe na NHIF kinakwamisha nia njema ya mradi. Ukiangalia utendaji uliojitokeza kwenye halmashauri ni wazi kuna aina ya uzembe unaosababisha kutoomba fedha hizo.

Kiundani zaidi kisa cha fedha hizi kutoombewa kunafanya maboresho yaliyokusudiwa kuwa ya juujuu zaidi kwani nia ilikuwa kuboresha huduma katika maeneo hasa kwa kutengeneza uwezo wa kununua dawa za ziada ambazo ni kilio kikubwa.

“Mradi huu ni fursa ya kuboresha huduma hasa ya dawa. Utashangaa huduma imeshatolewa kwa akinamama wajawazito lakini fedha haziombwi,” alisema Naibu Waziri.

Katika kuimarisha huduma hizi ni dhahiri kasoro zilizojionesha kwa mikoa ya Mbeya na Tanga hazifai kurudiwa kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara iliyoongezwa katika mradi.

Changamoto Wakati kuna ukweli usiopingika kwamba elimu zaidi inahitajika kuwahamasisha akinamama wajawazito na familia zao wajiunge na kunufaika na mradi huu kwani una manufaa makubwa katika maisha yao ya kila siku, halmashauri zinatakiwa kuanza kufikiria mradi huu kuwa endelevu hasa kutokana na kuonekana kuwasaidia sana wanawake wajawazito na wagonjwa wengine.

Hii inatokana na ukweli kuwa kasi ndogo ya uandikishaji wa akinamama wajawazito inatokana na mradi kutopata mwamko mkubwa katika siku za mwanzo.

Pamoja na changamoto ya elimu ili kuvukwa kwa lengo kuwe na maana zaidi, changamoto ya halmashauri kutoomba fedha ni mbaya zaidi kwa kuwa zinatengeneza pengo ambalo halistahili kuwepo kutokana na kuwapo kwa fursa ya fedha za kununulia dawa na vifaa tiba.

Ni vyema wakuu wa mikoa husika wakalipatia ufumbuzi suala hili ikiwemo wakuu hao kusimamia watendaji ili wawajibike katika kutoa taarifa za mara kwa mara za utekelezaji wa mradi huo, hususan suala la madai yao kwa NHIF.

Kaimu Mkurugenzi wa CHF, Rehani pia kwa upande wake anasema katika mahojiano kwamba kasi ya uandikishaji familia za akinamama wajawazito katika Mfuko wa CHF bado ni ndogo ukilinganisha na idadi ya akinamama walioandikishwa kwenye mradi.

“Kuna wanawake wengi mtaani kwangu mimi naona bado idadi haijawiana. Kwa kuwa mradi unapomsajili mjamzito familia yake pia inaandikishwa kwenye CHF ili inufaike katika mwaka unaofuata, bado kuna idadi ya akinamama waliomaliza mwaka wa kwanza wa huduma zao katika NHIF lakini wanapoingia mwaka wa pili ambapo huduma zao zinakuwa chini ya CHF, wanakuwa bado hawajapewa kadi zao na familia zao,” anasema Rehani.

Je, kuna la kujifunza? Ukiangalia mwenendo wa mradi huu inaonesha kwamba kuna uwezekano wa kuueneza nchi nzima na hasa kwa kuzingatia kwamba sasa unaingia mikoa ya Lindi na Mtwara. Hata hivyo, mfumo unatakiwa kuangaliwa kwa makini na kufanyiwa kazi pale unapolegalega hususan mwamko wa baadhi ya halmashauri. Huu ni mradi unaoweza kuokoa mamia ya wanawake wasiokuwa na uwezo ambao wanahitaji huduma ya uzazi na ulezi salama.

Kama watendaji wakiangalia uzoefu wa utekelezaji wa mpango huo kama ilivyojionesha katika mikoa ya Tanga na Mbeya ambapo Mfuko wa NHIF umepata uzoefu wa kutosha, miradi ya aina hii haitakutana na changamoto kubwa mbele ya safari.

Lakini hilo linawezekana kwa kuanza kujenga uwezo wa ndani ili mradi huu utakapofikia ukomo uweze kuwa endelevu. Kwa upande mwingine, watu wenye uwezo wa kufikiria watakubaliana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kwamba ipo haja kwa NHIF na mikoa husika kuanza kuliangalia suala la uendelevu wa mradi huu.

Kwani masuala kama vituo vya huduma kutowasilisha madai yao kwa huduma walizotoa kwa akinamama wajawazito pamoja na kuwa wamekuwa wakilipiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni kukazia maagizo ya ufuatiliaji, hali ambayo itasaidia kuondoa tatizo la dawa kwa kuwa vituo vitakuwa na fedha za kutosha zinazotokana na utoaji wa huduma za tiba.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: beda msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi