loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Msajili wa vyama aanza kuisuka Arusha mpya yenye amani

Mkoa huu tangu umalizike uchaguzi, haujatulia vyema kisiasa, kiuchumi na kiutalii kutokana na kukumbana na matukio kadha ya mauaji yaliyotokana na milipuko ya mabomu katika mkutano wa Chadema na risasi za moto, wakati Polisi wakijaribu kuzuia chama hicho kisifanye maandamano.

Pia bomu lingine lilirushwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti, ambapo watu watatu walifariki dunia na kufanya jumla ya watu waliofariki katika matukio yote kuwa zaidi ya kumi. Hali hii imelifanya Jiji hili kupunguza sifa yake kubwa ya kuwa kitovu cha utalii, kutokana na matukio haya kutisha baadhi ya watalii na kukataa kurudi nchini kutembelea kwa kuhofia maisha yao.

Licha ya mambo hayo kutokea , Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi, anasema Mkoa huo hauwezi kubaki katika hali hiyo, bali unahitajika kurudisha hali yake ya zamani kuwa sehemu ya kimbilio la mataifa mbalimbali.

Mutungi anaanza harakati zake za kutaka mkoa huu uwe tulivu na amani kwa kukutanisha viongozi wa vyama vya siasa, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na viongozi wa dini mbalimbali mkoani na kuona umuhimu wa kufanya mkutano wa pamoja utakaojumuisha vyama vyote vya siasa mkoani hapa.

Anasema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya mpira maarufu kwa jina la Shehe Amri Abeid, huku wafuasi wa vyama vyote wakiwa kwenye mavazi ya kawaida yasiyoonesha alama yoyote ya vyama vyao na viongozi wote wa vyama watakuwa katika sare za vyama vyao na watakaa jukwaani, huku bendera za vyama vyao zikipepea jukwaani.

Jaji Mutungi anasema katika mkutano huo salamu kubwa itakuwa Arusha Oye, au Tanzania ikiwa ishara ya kutanguliza Tanzania kwanza na vyama baadaye.

“Lakini maana yake nini hasa ya salamu hizi badala ya salamu za vyama ni kutaka watu wote wa vyama waone kama wanahitajika katika suala la kulinda amani na kutanguliza utaifa kwanza, lakini tunawakumbusha kuwa siasa sio uadui, bali utofauti wa sera na mawazo, kulingana na kila mtu na chama chake,” anasema Jaji Mutungi.

Anasema lengo lake kubwa anatarajia baada ya mkutano huo Mkoa wa Arusha uwe na amani, ili uweze kusonga mbele katika nyanja ya uchumi unatokana na utalii. Jaji Mutungi anasema kunapokuwa na mapambano baina ya vyama vya siasa na polisi kwa kuzuia maandamano yanayofanyika, hapo ndipo kila upande unapotakiwa kutumia busara na kulitanguliza taifa kwanza ili kuleta na kulinda amani.

Aidha anasema katika vurugu hizi watu wengi wanapata sababu za kujipenyeza na kuanza kuleta hila kuwa ni vurugu zitokanazo na watu wa Moshi kwa madai kuwa wafanyabiashara wa Arusha wakikosa amani wao watapata soko, jambo ambalo siyo kweli.

Katika kuzunguka na kulisikia suala hili nimekataa kabisa sababu wamiliki wa maduka yaliopo Arusha asilimia zaidi ya 70 ni Wachaga na hata hoteli za kitalii ni za Wachaga, hivyo kusema Wachaga wanakuja kuleta vurugu Arusha ili wao wanufaike siyo kweli bali watu wanatafuta sababu.

Anasema ni vema pande zote kuanzia dola, vyama vya siasa vikatafakari na kuanza ukurasa mpya, sababu vurugu hizo hazinufaishi taifa wala mtu yeyote, bali faida kwa nchi jirani ambao hupata manufaa kwa kupata wageni wengi wa utalii. Anasisitiza amani ni tunda la haki, hivyo ni vema hata Jeshi la Polisi likatumia busara katika kutekeleza majukumu yake ya kazi na siyo kutekeleza kila amri au maelekezo anayopewa na wanasiasa.

“Nasema hivi katika utekelezaji wa majukumu ya kiuchumi, siasa zisichukue mkondo, bali uchumi uchukue mkondo wake na sio kutekwa na siasa,” anasema Jaji Mtungi Pia anasema hata viongozi wa dini ni vema wakaepuka siasa wanapokuwa katika madhabahu, kwani nchi wataipeleka pabaya na inatupasa kumkataa shetani kwa nguvu zote kama vile Wakristo wanapobatizwa na kuulizwa kama unamkataa shetani na kuitikia twamkataa.

“Arusha tumkatae shetani na mambo yake yote, katika hili tuwe kama Wakristo tunapobatizwa tunaulizwa unamkataa shetani na mambo yake yote unasema ndio na Arusha tuseme hapa tumkatae shetani wa kuvuruga mji,” anasema Jaji Mutungi.

Anasema athari za kukosekana amani Arusha ni kubwa, kwa sababu amepita kufanya uchunguzi kwa baadhi ya hoteli za Mkoa wa Arusha, kuona jinsi walivyoathirika na vurugu zilizotokea, wengi wamemweleza wameathirika kwa kupunguza upokeaji wa idadi ya watalii.

“Katika hoteli nyingi nilizopita hapa Arusha kuchunguza suala hili la vurugu limesababishaje sekta ya utalii kukosa mapato, nimejibiwa wameathirika, kwani wageni waliokuwepo wakati mabomu yakipigwa waliapa kutorudi tena Tanzania kwa kuhofia maisha yao, sasa hapa hasara kwa taifa na hata mtu mmoja mmoja,” anasema Jaji Mutungi.

Anawataka watu w ote wanaoishia mkoani humo kuwa wa kwanza kuhubiri amani na siyo chuki, ili kuzaliwe Arusha waliyokuwa nayo miaka kumi nyuma. Naye Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa Mulongo anasema katika kuhakikisha Mkoa huo unakuwa na amani, wameanza kwa kupatana wao viongozi kama yeye na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema na sasa wapo kitu kimoja.

“Hamjajua tu sisi ni wamoja, waliopandikiza mgogoro kwetu sisi tumevuka huko siku nyingi na nawaomba waandishi wa habari nyie ni wadau muhimu katika kulinda amani lindeni amani hii na kuunga mkono safari mpya tunayoanza,” alisema Mulongo. Mulongo akirudia mara kwa mara kuvisihi vyombo vya habari kutoongeza chumvi katika habari zao, anasema kunapokuwa na amani kila mmoja anaweza kufanya shughuli zake za uzalishaji mali bila wasiwasi.

“Lakini amani ikitoweka kwanza ni gharama kuirudisha na pia kila mtu anapata hasara kwa kukosa muda wa kuzalisha mali na hivyo ni vema kila mmoja awe mstari wa mbele kulinda amani hii,” anasema Mulongo.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, anaanza kuzungumza katika mkutano huo kuwa, anashangaa wanahabari kutaka kuvunja miguu kumpiga picha akiwa na Mulongo wameketi pamoja na kuzungumza kama marafiki.

“Sisi hatuna mgogoro jamani umeisha siku nyingi na tumekula hata chakula mara nyingi, kwani nimegundua huwezi kufanya kazi zako kama kiongozi bila kushirikiana na viongozi wenzako kama Mkuu wa Mkoa na yeye hawezi fanya majukumu yake bila kuwa pamoja na mimi au wananchi,” anasema Lema.

Lema anasema vitu vyote hivyo vinategemeana na utawala unategemea watu katika kutekeleza majukumu yake, hivyo ni vema pande zote zikaheshimiana ili kulinda amani. “Lakini hapa nasisitiza ili amani iwepo mahali popote ni lazima kuwe na tunda la haki, hili ni msingi mkubwa wa amani, pale tunda la haki linapokosekana ndipo amani inapotoweka,” anasema Lema.

Anasema Arusha kwa sasa ni mahali salama kabisa kufanya kila shughuli, hivyo kama wadau wa vyama vya siasa walikosa kwa kusababisha kukosekana kwa amani, wanaomba kusamehewa na wale wote waliowakwaza.

Aidha anamsihi Msajili kutekeleza majukumu yake bila ubaguzi kama alivyoanza, kwani vyama vya siasa vya upinzani wanaiangalia kwa jicho tofauti ofisi hiyo na kumpima, hivyo kama lengo la kuleta amani nayeanapaswa kuvibeba vyama vyote vya siasa kama watoto wake wa ubavu mmoja.

Lema anavigeukia vyombo vya habari naye kwa kuviomba kutokuza habari kwenye jambo dogo, ili kulinda amani inayopaswa kulindwa na kila mmoja.

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi ...

foto
Mwandishi: Veronica Mheta

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi