loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mshtakiwa ana haki kumkataa jaji au hakimu kabla ya hukumu

Majaji hao ni Engera Kileo na Nathalia Kimaro ambao walikuwa katika jopo la majaji watano wa kesi hiyo. Majaji hao walijitoa baada ya warufani wote watatu wakiongozwa na Jeetu Patel kuwasilisha barua ya kutokuwa na imani nao kwa sababu ni wa kabila moja na mrufaniwa, Bw. Mengi, wakati warufani wote ni watanzania wenye asili ya kiasia (wahindi).

Warufani walibainisha katika barua yao kwamba mmoja wa majaji hao wawili waliojitoa katika jopo hilo amekuwa hawatendei haki washtakiwa watanzania wenye asili ya kiasia katika kesi alizowahi kusikiliza.

Walisema wanaamini hata Mengi naye hangekubali kusikilizwa na majaji wenye asili ya kiasia katika kesi hiyo.

Hata kama sababu walizotoa warufani hazikuwa na nguvu sana, lakini zikionesha woga na wasi wasi wa kutotendewa haki, majaji hao waliamua kujitoa na kumwachia Jaji Mkuu kupanga majaji wengine waungane na watatu waliobaki ambao ni waheshimiwa William Mandia, Kipenka Musa na Batuel Mmilla.

Mtazamo wa jumla wa kisheria ni kwamba mshtakiwa au mdaiwa au mfungua mashtaka au mdai mahakamani hawezi kuamua ni Jaji au Hakimu gani asikilize kesi yake. Mahakama ndiyo inayompanga Jaji au Hakimu wa kesi yoyote, iwe ya jinai au ya madai.

Hata hivyo, iwapo kumejitokeza haja ya mshtakiwa au mdaiwa au mdai kutaka abadilishiwe Jaji au Hakimu kwa vile hana imani naye au hapendi tu, anapaswa kuwa na sababu za kuridhisha ambazo atazisikiliza yule yule jaji au hakimu anayemkataa.

Naye Jaji au Hakimu anayekataliwa anaweza kukubali kujiondoa au akakataa kama kuna sababu za msingi au hakuna sababu za msingi.

Ila mara nyingi Jaji au Hakimu akikataliwa iwe kwa sababu nzito au sababu zisizo nzito au pengine wasi wasi tu wa anayetoa ombi hilo kama tulivyoona katika kesi ya Mafisadi Papa, Jaji au Hakimu ataamua kujitoa ili haki iweze kutendeka kwa kesi kusikilizwa na Jaji au Hakimu mwingine.

Ni vizuri majaji au mahakimu wakajisikia kuaminiwa na pande zote husika za kesi ili haki sio tu itendeke bali ionekane imetendeka. Vigezo muhimu na rahisi ambavyo mtu aweza kutumia kumkataa jaji au hakimu ni kuangalia kama misingi ya haki za asili inazingatiwa katika usikilizaji wa kesi.

Haki hizo hueleza kwa mfano jaji au hakimu asiyefanya upendeleo katika mwenendo mzima wa usikilizaji shauri kama vile kuupatia upande mmoja fursa ya kutoa ushahidi na kuunyima upande mwingine kufanya hivyo.

Msingi mingine inahusu jaji au hakimu kutokuwa na uhusiano wa karibu na upande mmoja wa kesi kama vile urafiki, undugu wa damu, ushiriki wa masuala fulani na kadhalika.

Au kuwa ni mlalamikaji kupitia watu wengine. Mfano kama kesi ikihusu wizi ambao jaji au hakimu naye aliibiwa. Kwa kifupi kigezo kikubwa ni kile cha kuwepo uwezekano mkubwa wa upendeleo katika shauri ambapo uamuzi wa jaji au hakimu waweza kutiliwa shaka.

Aidha, ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 kwamba mshtakiwa au mdai mahakamani anapaswa kusikilizwa kikamilifu na pia kupewa haki ya kukata rufaa na nafuu nyingine kisheria.

Katika kesi ya ZABANI PANGA MALEZA vs JOACKIM KIWARAKA, Maombi ya Madai Namba 33 ya Mwaka 1987 mdai alisema: “Sina imani na hakimu huyu. Naomba kesi yangu isikilizwe na hakimu mwingine.”

Lakini hakimu huyo alikataa na akang’ang’ania kuendelea kusikiliza shauri hilo. Hakimu huyo alikataa kujitoa akidai kwamba wadaiwa wa pande zote mbili hafahamiani nao na kwamba mdai hakutoa sababu za msingi za kwa nini anamkataa hakimu huyo. Kesi iliendelea kwa rufaa hadi Mahakama Kuu ambayo ilikubaliana na hakimu.

Mdai alikata tena rufaa katika Mahakama ya Rufaa mbele ya Jaji Lameck Mfalila. Mheshimiwa Jaji Mfalila pamoja na mambo mengine alisema:

“Sio lazima mdai atoe sababu za msingi kwa nini anamkataa hakimu. Suala la msingi ni kufikiria kama huyo mshtakiwa au mdai ambaye ni mtu wa kawaida, ni kweli anaamini na ana wasi wasi kuwa hawezi kupata haki mbele ya hakimu huyo (anayemkataa)”.

Kwa hiyo suala la kumkataa hakimu ni zaidi ya sababu zinazoweza kutolewa ikiwemo zile za kukiuka misingi ya haki za asili tulizozijadili awali. Kwa mujibu wa Mheshimiwa Jaji Mfalila, ambaye uamuzi wake ndio msimamo wa kisheria hivi sasa kwa vile ni uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, kumkataa hakimu kuendane na imani ya kweli ya yule anayemkataa kwamba hatatendewa haki na hakimu huyo.

0715/0754 362 544 au baruapepe; alloycekomba@gmail.com

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Alloyce Komba

1 Comments

  • avatar
    Kingazi shemzituh
    02/01/2021

    SoMo ni zuri na limeeleweka vema, naomba kujua utaratibu wa kufuata pindi mm ni mlalamikaji na Sina Imani na hakimu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi