loader
Dstv Habarileo  Mobile
‘Mume wangu ni zawadi kutoka kwa Mungu’

‘Mume wangu ni zawadi kutoka kwa Mungu’

Daktari huyo na familia yake walikwenda Vatican usiku kwa kutumia ndege ya Serikali ya Italia. Mipango ya kuiondoa familia hiyo Sudan ilifanywa kwa usiri mkubwa, na imefahamika kwamba, hadi anaondoka nchini humo, Meriam hakufahamu anapelekwa wapi. Mwanamke huyo ni mke wa raia wa Marekani, Daniel Wani (27), wana watoto wawili, Martin na Maya.

Kwa mujibu wa Wakili wa Meriam, Elshareef Ali Mohammed, mwanamke huyo alielezwa usiku kuwa anaondoka Sudan lakini hakuambiwa anapelekwa wapi. “Hakuna mtu kutoka serikali aliyefahamu hadi ndege ilipopaa isipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, na ninadhani alimweleza Rais,” anasema Wakili huyo.

“Wiki iliyopita kuna kundi lilitishia kushambulia ubalozi wa Marekani walipokuwa wanaishi, kwa hiyo tusingeweza kuendelea kusubiri,” anasema. “Alikuwa na muda mfupi sana…alitaka kuwaeleza watu kwamba anaondoka lakini hakukuwa na muda, hakujua hata anakokwenda,” anasema Wakili huyo. “Sikuamini” Meriam anamweleza Mkuu wa Waitalia waliopo Darfur, Antonella Napoli.

“Nikaibaini ndoto yangu kubwa zaidi kwenye maisha yangu, kukutana na Papa,” anasema Meriam. Baada ya Meriam kuachiwa kutoka gereza alipokuwa anasubiri viboko na kunyongwa, na akakamatwa tena, Sudan Kusini ilijitolea kusimamia mazungumzo kati ya watetezi wa Meriam na Serikali ya Sudan, lakini jambo hilo halikufanikiwa. Mume wa Meriam, Daniel Wani (27) ni mzaliwa wa Sudan Kusini.

Kwa kuwa Italia ndiyo Rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya (EU) na kwa kuzingatia pia nafasi ya Papa kiimani, nchi hiyo ikaingilia kati ili kumuokoa Meriam. “Lilikuwa ni suala la kisiasa tuliloanza kulijadili muda mrefu uliopita…Serikali ya Sudan ilifikiri wana uhusiano mzuri na Italia kwa hiyo wangemuachia (Meriam) aondoke,” anasema Mr Elshareef.

Kwa mujibu wa Wakili huyo, ndege iliyomuondoa Meriam na familia yake Sudan, ilitoka Rome ikiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Lapo Pistelli. Pistelli anasema, hadi Meriam anaondoka Sudan hakuelezwa chochote, ikiwa ni pamoja na kutoambia kuwa anakwenda wapi kwa sababu waliogopa kumvunja moyo kama mpango huo usingefanikiwa.

Anasema, mara kwa mara, kupitia kwa Balozi wa Italia aliye Khartoum, Armando Barucco, nchini hiyo ilikuwa inawasiliana na Sudan kuhusu kesi ya Meriam. Inadaiwa kuwa, kupitia mawasiliano hayo, Sudan iliieleza Italia kuwa kulikuwa na fursa ya kidiplomasia kuhusu jambo hilo na kwamba, ilikuwa tayari kumrudishia Meriam hati yake ya kusafiria ambayo ingemwezesha kuondoka.

“Nilimjulisha Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na iliamriwa kwamba, twende Khartoum haraka,” anasema Pistelli. “Hatukuwalipa chochote na wala hatuwaahidi chochote, tunajua namna ya kufanya siasa bila kufungua waleti” anasema. “Walifurahi sana (familia ya Wani) walipofahamu hatimaye wangeondoka Sudan, kilikuwa kipindi kigumu sana kwao wote. Hatukuthubutu kuamini ingetokea hadi ndege ilipopaa, tutawa tunasherehekea,” anasema Elshareef.

Meriam anasema “Kila mara nilikuwa na imani yangu na upendo wangu kwa mume wangu, zawadi kutoka kwa Mungu…nilipotakiwa kuikana imani yangu ya Kikristu nilijua nilikuwa nahatarisha maisha yangu kwa kukataa lakini sikutaka kuukana ukristu.” “Nitaanza maisha mapya na familia yangu, tutaenda New Hampshire anapoishi shemeji yangu, Gabriel, atatusaidia, wote tutakuwa pamoja, kama familia, asante Italia, asante Mungu, wote tupo salama,” anasema Meriam.

Meriam na familia yake wameondoka Rome nchini Italia, Julai 31 mwaka huu kwenda Marekani wakiwa na fikra za kuanza maisha mapya ambayo kwa kiasi kikubwa yatahitaji msaada ili kujikimu kwa kuwa kuna taarifa zinazodai kuwa, Wani amefukuzwa kazi nchini Marekani kwa kuwa alikaa muda mrefu Sudan katika harakati za kuokoa maisha ya mkewe.

“Kiasi fulani nina hofu kuondoka Rome, tumekuwa na furaha sana hapa, tumejisikia kama familia halisi,” anasema Meriam na kubainisha kwamba, wakati wanasubiri kukamilishwa kwa taratibu kwa ajili ya kuondoka huko kwenda Marekani, walitembelea sehemu mbalimbali za jiji hilo.

Kwa mujibu wa Meriam, miongoni maeneo waliyotembelea ni safari iliyokuwa na hisia kwenye ukumbi wa kumbukumbu ambako maelfu ya wakristu waliuawa kwa sababu walikuwa na msimamo kuhusu imani yao. Familia ya Wani pia imepata fursa ya kusali katika kanisa maarufu zaidi jijini Rome la Mtakatifu Paul.

“Tuliona jiji lote, tulienda Colosseum, Jumapili tulienda kwenye misa, na tulienda kununua vitu, tulirudi kwenye maisha, na sasa sijui nitarajie nini lakini kwa kiasi fulani wote tutakuwa pamoja,” anasema mwanamke huyo anayejitambulisha kuwa ni daktari wa hospitali, alihitimu katika Chuo Kikuu cha Khartoum nchini Sudan.

Mume wa Meriam anasema “Kaka yangu atatusaidia, na nina uhakika jumuiya ya Kikristu New Hampshire itakuwa nasi. Mara nyingi mambo ya baadaye huwa hayajulikani lakini nina uhakika,” mwanaharakati, Antonella Napoli anasema, ziara ya familia hiyo Colosseum imeigusa familia hiyo jasiri, na kwamba, iliguswa mno kwa namna walivyopokewa jijini Rome.

Wakati wakiwa Rome kwa wiki moja, Wani, Meriam na watoto wao walipewa nyumba ya kuishi na ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kuishi pamoja kama familia tangu azaliwe mtoto wa pili kwa wanandoa hao, Maya. Wani na familia yake wakati wapo Italia walipewa nguo mpya na wakatembezwa sehemu mbalimbali wakiwa na ulinzi wa polisi.

Martin anakaribia kutimiza umri wa miaka miwili, aliishi jela na mama yake kwa miezi kadhaa wakati mwanamke huyo anasubiri kuchapwa viboko 100 na kunyongwa, Maya amezaliwa gerezani Mei 27 mwaka huu.

Ilidaiwa kwamba, ndani ya wiki mbili kuanzia siku alipojifungua (Mei 27, 2014), kama Mahakama ya Rufaa isingetoa uamuzi wa rufaa kubatilisha hukumu ya viboko na kunyongwa, mama huyo angechapwa viboko 100, na kisha angenyongwa baada ya kumuachisha Maya.

Meriam na Martin walianza kukaa jela Septemba mwaka jana, Mei 15 mwaka huu akatiwa hatiani na kuhukumiwa. Meriam aliieleza Mahakama Kuu ya Sudan kuwa, ‘Sijawahi kuwa Muislamu, tangu mwanzo nililelewa kikristu’. Siku chache kabla ya kujifungua, mwanamke huyo alimwambia mumewe kuwa ni bora afe kuliko kuiasi imani yake.

“Kama wanataka kuniua waendelee tu, waniue kwa sababu sitabadili imani yangu,” alisema Meriam wakati anazungumza na mumewe alipokwenda kumtembelea jela. Meriam alisema kuwa, yeye ni Mkristu na hawezi kujifanya Muislamu ili asiuawe. “Nilikataa kubadili, siuachi ukristu ili tu niendelee kuishi… nafahamu ningeweza kuishi kwa kuwa Muislamu na ningeweza kuilea familia yetu lakini nahitaji kuwa mkweli kwangu,” anasema Meriam akiwa jela.

Wakati wa kesi iliyomkabili ya kuuacha uislamu na kuwa Mkristu, Meriam huyo aliwasilisha mahakamani cheti cha ndoa kuthibitisha kuwa yeye ni Mkristu. Pamoja na ushahidi huo, Jaji anasema, kwa kuwa baba wa mwanamke huyo alikuwa Muislamu, ingawa aliitelekeza familia wakati wanaishi kwenye kambi ya wakimbizi kusini mashariki ya Sudan wakati Meriam akiwa na umri wa miaka sita, yeye (Meriam) pia ni Muislamu hivyo amevunja sheria kwa kuiacha dini hiyo.

Mama mzazi wa Meriam alizaliwa Ethiopia, wazazi wake ni Wakristu. Wakati Meriam anahukumiwa Jaji Abbas al Khalifa alimuuliza kama angerudi kwenye Uislamu, akajibu ‘Mimi ni Mkristu’, na ndipo akahukumiwa kifo kwa kunyongwa. Baada ya shinikizo kubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani, Meriam aliachiwa Juni 26, siku iliyofuata akakamatwa katika uwanja wa ndege jijini Khartoum wakati yeye na familia wanajiandaa kuondoka Sudan.

Ingawa Martin amebatizwa hivyo ni mkristu, sheria za Sudan zinamtambua kuwa ni Muislamu kwa kuwa hazimtambui Meriam kuwa ni Mkristu, hivyo hakuruhusiwa kukaa na baba yake kwa sababu mwanamume huyo ni Mkristu. Baba mzazi wa Meriam alikuwa Muislamu, mama wa mwanamke huyo ni Mkristu wa dhehebu la Orthodox.

Kwa mujibu wa Wani, idara ya Serikali ya Sudan ilimtaka awasilishe ushahidi wa kipimo cha vinasaba (DNA) kuthibitisha kwamba Martin ni mwanawe, aliwasilisha lakini wahusika hawakuviamini. Kwa muda mrefu wakati Meriam na Martin wapo jela, Wani hakuruhusiwa kuwatembelea, lakini baada ya kuzaliwa Maya, mwanaume huyo alishinikiza aruhusiwe kwenda kuwasalimu.

Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya Sudan, sheria za nchi hiyo zinamtambua Martin kuwa ni Muislam, na pia ndoa ya Meriam na Wani ni batili. “Walitaka kunizuia lakini nilitaka kwenda kumsalimia (mkewe). Siku alipozaliwa (Maya), hawakuturuhusu kumuona (Meriam) kwa sababu alikuwa amefungwa minyororo miguuni,” anasema Wani.

“Waliogopa kwamba, kama ningeingia ndani na kumuona anajifungua akiwa kafungwa minyororo ningesema hilo jambo,” anasema Wani. “Tulipokwenda pale asubuhi walisema kuna agizo na huwezi kumuona, baada ya hapo tulikwenda kwenye uongozi wa juu wa gereza kupata ruhusa” anasema Wani.

“Walijaribu kusema ilikuwa ni amri kutoka juu na nikauliza nani? Una maana Waziri wa Mambo ya Ndani? Niliweza kuingia ndani kwa sababu ya kujifungua (Meriam), baada ya hapo waliniruhusu niingie kumsalimia mara mbili kwa wiki. Wakati anajifungua alikuwa amefungwa minyororo,” anasema.

“Nilikuwa nikirudia kuwaeleza kwamba nilitaka kukitoa kichanga gerezani, ningeweza kumpeleka (Meriam) kwenye hospitali alipojifungulia Martin, kwanza walisema sawa, baadaye walikataa,” anasema siku chache baada ya kufika Marekani. Wani anasema, kwa takribani mwaka, familia yake imekuwa ‘jehanamu’.

Kwa kuwa Meriam ameolewa na Mkristu, Mahakama alisema amevunja sheria hivyo lazima auawe. Wani anasema, anahitaji muda ili arudi kwenye hali ya kawaida, na kwamba, mkewe anahitaji muda mrefu zaidi, lakini anafurahi kwa kuwa wamerudi nyumbani. Ingawa familia ya Wani ipo Marekani lakini hadi sasa Meriam bado ana mashaka kuhusu usalama wao, na kila anapomuona mtu asiyemfahamu anaogopa.

Ingawa wapo nyumbani lolote linaweza kutokea hasa kwa kuzingatia ahadi ya mwanaume aliyejitambulisha kuwa ni kaka wa mwanamke huyo, Al Samani Al Hadi, ambaye alisema, endapo Meriam angeachiwa, yeye atamuua. “Jina lake si Mariam, jina lake ni Abrar al- Hadi, mimi ni al- Samani al-Hadi Mohamed Abdullah, kaka yake mkubwa…lile jina lilitushtua, hivi ndivyo sheria inavyosema, na kamwe hatuwezi kupotosha hilo.

Akifa tutakuwa tumetekeleza neno la Mungu. Ufumbuzi ni kwamba, anyongwe, kama tulivyoamriwa na Mtume wetu, amani iwe juu yake…anayeiasi dini yake lazima umuue,” anasema. Wakili wa Meriam, Elnour, amekaririwa akisema “Kuna Waislamu wengi wamechukizwa na hili, na wanasema kwamba, kama Mahakama haimuui Meriam wao watafanya hivyo akiachiwa”.

Kwa kuzingatia hayo, ingawa Meriam na familia yake wapo nyumbani Marekani, hawapo salama, mamlaka zinazohusika ziwalinde. Makala haya yataendelea wiki ijayo kwa kueleza walichokisema Meriam na mumewe baada ya kufika Marekani. Yameandikwa kwa msaada wa mtandao.

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi