loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Muundo wa Bunge, uraia pacha vyatawala Bunge la Katiba

Kutokana na kamati zote kupingana na muundo wa serikali tatu na kutaka serikali mbili, zimekubaliana au kukaribiana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo wa bunge ambapo nyingi ya kamati hizo zimetaka kuwepo bunge moja au mabunge mawili yenye chemba au sehemu tatu.

Rasimu ya Warioba imependekeza kuwepo Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bunge la Tanganyika na la Zanzibar. Wajumbe wa Bunge Maalumu ambao wanaanza mjadala mpana kwa pamoja leo wanapendekeza sehemu au chemba moja ijadili masuala ya Zanzibar, sehemu ya pili ijadili masuala ya Tanzania bara na ya mwisho ijadili masuala ya Muungano.

Miongoni mwa kamati ambazo jambo hilo limejitokeza ni Kamati namba moja inayoongozwa na Mwenyekiti Ummy Mwalimu na Kamati namba 11 ambapo Makamu Mwenyekiti wake, Hamad Masauni Yusuf anasema jambo hilo wajumbe wake wengi wamelitaka.

Masauni anasema kwenye kamati yake, wajumbe wengi wanataka kuwe na sehemu mbili za bunge ambazo ni Bunge la Muungano na la Tanzania Bara na wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar wasiruhusiwe kujadili mambo ya bara ila washiriki ya Muungano pekee.

“Hata hivyo, tumeona ina changamoto kwani kuna mambo tumeona si ya muungano, lakini yapo chini ya mamlaka ya muungano mfano Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) si la muungano lakini linasimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo lipo kwenye muungano,” anasema.

Anasema katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inapendekeza wabunge wawe 70 lakini kamati hiyo imeona isiweke idadi na badala yake idadi hiyo itegemee idadi ya majimbo na sheria zitakavyokuwa. Kwa upande wa Mwenyekiti Mwalimu, anasema suala la muundo wa Bunge limeleta mjadala mzito na kumekuwa na pande mbili; moja inataka bunge liwe na sehemu mbili na mwingine uendelee muundo wa sasa wa Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi.

Katika kulielezea hilo anampa nafasi mjumbe Ali Kessy Mohamed ambaye ni Mbunge wa Nkasi, aliye kwenye upande wa kutaka sehemu mbili za bunge anayeelezea kuwa wengi wanataka kuwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano litakalowakilisha upande wa Tanzania Bara na wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

“Tunataka wawakilishi wa Zanzibar wakija bara wajadili mambo ya muungano tu na inapofika mambo yetu ya bara waondoke. Haiwezekani wao 50 tu lakini mtu ayajue mambo ya kwangu Nkasi (Rukwa), mimi mwenyewe siyajui. Ila kwenye mshahara na posho malipo yawe sawa,” anafafanua Kessy.

Kamati namba tatu inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Michael Francis inataka muundo wa Bunge uwe wa bunge moja na kuwe na sehemu tatu kwa wabunge kutoka Zanzibar wajadili masuala yao, Tanzania bara nao wajadili yao na wakutane kwa pamoja kujadili masuala la Muungano tofauti na ilivyo sasa ambapo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanajadili masuala ya Zanzibar na wanakutana na wabunge wa Tanzania bara kujadili masuala ya bara na muungano kwa pamoja.

Dk Francis anasema wabunge hao watapatikana wawili kwa kila jimbo kwa kuzingatia jinsi, yaani atasimama mwanamke na mwanaume. Kwa upande wa Kamati namba 10, Mwenyekiti wake Anna Abdallah anasema wamekubaliana serikali mbili kama ilivyo sasa lakini nafasi ya viti maalumu ifutwe na kila jimbo kuwe na wagombea wawili, mwanamke na mwanaume ili kufikia uwiano wa asilimia 50 kwa wanawake na wanaume.

Pamoja na muundo wa Bunge ambao wabunge wengine kama Said Amor Arfi anaeleza ni kuonesha kwamba wanatambua muundo wa serikali tatu, wajumbe pia wamejadili na wengi kukubali uraia pacha lakini wote wameungana kwenye kutaka kuwekwe mipaka. Mwenyekiti wa kamati namba Tano, Hamad Rashid Mohamed, anasema uraia pacha umeleta mjadala mkali.

Anasema pamoja na kupata elimu kutoka kwa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na Idara ya Uhamiaji wameamua suala hilo waliache na kupigiwa kura ndani ya Bunge kwani waliangalia kiuchumi kama utasaidia uwekezaji nchini na watakaopewa uraia huo wana utaalamu wa teknolojia kwa faida ya nchi.

“Tuliangalia pia kwa sehemu zenye wakimbizi kutoka Rwanda na Burundi wao wanataka uraia kwa faida gani? Lakini tukaona tofauti na mazingira ya wanaotokea India na China wenye pesa zao wanaleta kuwekeza. Pia tumeangalia kiuchumi mtanzania aliyeukana utanzania kwenda nje anataka kurudi nyumbani ana fedha kiasi gani za kutaka kuja kuwekeza nchini au wana teknolojia au utaalamu gani,” anasema.

Masauni akizungumzia jinsi kamati yake ilivyolijadili suala hilo la uraia pacha anasema wamekubaliana kwa kupiga kura na kulipitisha lakini wanataka kuwe na mipaka. Anasema wajumbe wa kamati yake wanataka, kwa mfano, mwenye uraia pacha asigombee urais wala nafasi yoyote ya uongozi kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu.

“Kwa kifupi wajumbe wanataka mwenye uraia pacha asichague wala kuchaguliwa,” anasema. Kwa upande wa kamati anayoongoza Mwalimu, katika kipengele cha uraia pacha wamekubaliana kwamba aliye na uraia wa aina hiyo asipewe uongozi kwenye vyombo vya dola kama Mkuu wa Polisi au Jeshi la Wananchi.

Mbali na muundo wa serikali na uraia pacha, kamati hizo zimekubaliana bila kuhitilafiana juu ya Rais wa Zanzibar kuwa makamu wa Rais. Hata hivyo, zimetofautiana kidogo kwa wengine kutaka awe makamu wa kwanza wa rais na wengine wakitaka awe makamu wa pili wa rais. Pia wanataka kuundwe Tume kisheria itakayoshughulikia kero za Muungano na mwenyekiti wake awe Makamu wa Rais.

Mbali na hayo, wajumbe hao pia wameboresha vipengele kadhaa kwenye rasimu hiyo ikiwemo wananchi kupewa uwezo kisheria kuwaondoa wabunge wao madarakani wasioweza kutatua kero za wapigakura wao. Mwenyekiti wa Kamati namba Tano, Hamad Rashid Mohamed, anabainisha hayo ikiwa ni sehemu ya mabadiliko yaliyopendekezwa na wajumbe wengi wa kamati yake wakati wakijadili Sura ya Tisa ya Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.

Katika sura hiyo ya Tisa, rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba inazungumzia juu ya Kuundwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano na madaraka yake na katika sehemu ya pili ya sura hiyo inaelezea juu ya uchaguzi wa wabunge na ndani yake wapigakura wamepewa haki ya kumwajibisha mbunge iwapo ataunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au ya taifa.

Pia rasimu inasema mbunge anaweza kuwajibishwa kwa kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapigakura wake, kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi.

Akielezea hoja zilizotolewa na wabunge wa kamati yake katika kubadilisha sehemu hiyo ya rasimu Mwenyekiti huyo anasema “hii ikiachwa italeta vurugu katika nchi kwa sababu hakuna kigezo cha kumpima mbunge. Hili ni so complicated (jambo linalochanganya) na utekelezaji wake ni mgumu na hii itakuwa chanzo cha vurugu katika katiba na kwenye katiba haitakiwi kuwe na ugumu wa jambo, sasa tumeona tukiondoe.”

Wiki hii wabunge wanajadili maoni ya kamati hizo ndani ya bunge na hapo ndipo kutajulikana kipi cha kufuatwa kama kuwe na uraia pacha au la na pia muundo wa bunge utapitishwa na wabunge wote wa bunge hilo Maalumu la Katiba.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi