loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwalimu alivyolivalia njuga suala la ngoma

Mwalimu alivyolivalia njuga suala la ngoma

Miaka ya nyuma ngoma za asili zilikuwa zikipewa sana kipaumbele kuanzia shule za msingi hadi Sekondari ambapo inapofika Ijumaa katika shule nyingi nyakati za mchana huwa kipindi cha michezo kinaanza na ngoma za asili huwa hazikosekani.

Kwa miaka ya hivi karibuni shule nyingi mijini na vijijini hazitilii tena maanani uwepo au umuhimu wa ngoma hizo licha kuwa baadhi ya shule chache zimekuwa zikitumia ngoma hizo wakati wa matukio mbalimbali shuleni kama mahafali au kuna wageni maalum ndipo vikundi huandaliwa na kufanya mazoezi kwa ajili ya kutumbuiza.

Utandawazi unatajwa kuwa ni sababu inayopelekea kusahaulika kwa utamaduni huo kwa watoto wa shule sasa muda mwingi unatumika kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana mtu anayecheza ngoma za asili kuwa ni mshamba asiye na thamani yoyote. Hata hivyo kuna baadhi ya shule mkoani Dodoma ambazo zimeamua kurudisha ngoma za asili mashuleni kwa lengo la kudumisha utamaduni wa Mtanzania.

Shule ya Sekondari ya DCT Mvumi iliyopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ni miongoni mwa shule ambayo imeamua kuunda kikundi cha ngoma za asili. Mwalimu wa kikundi hicho, Emmanuel Chidong’oi anasema kikundi hicho kilianza Septemba mwaka 2013 ambapo lengo lilikuwa ni kutoa burudani na pia kuwafundisha wanafunzi utamaduni na jinsi ya kuimba na kucheza nyimbo za asili kwa ajili ya faida yao ni vizazi vya baadaye.

Anabainisha kwamba mara ya kwanza kundi hilo kutumbuiza ilikuwa ni kwenye mahafali ya mwaka huu ya wanafunzi wa kidato cha nne ambapo ngoma zilizotumbuiza ni za kabila la Kigogo zinazoitwa Muheme. Baada ya kumaliza kutumbuiza wadau mbalimbali pamoja na viongozi wa shule wakapenda burudani ile na kuahidi kusaidia kikundi hicho ili kiweze kupata vifaa ikiwemo ngoma na sare.

Pia Mratibu wa Mfuko wa shule hiyo Nedkemp ambaye ni raia wa Uingereza aliahidi atasaidia ngoma na sare. Tayari mfadhili huyo ametoa fedha kwa ajili ya kununua ngoma nne za kikundi hicho.

“Baada ya kupiga ngoma peke yake wakati kikundi kinaimba sasa tunataka tuongeze marimba, maze kwa vile shule imekubali kuundwa kwa kikundi hiki Mkuu wa shule amekubali kugharamia vifaa hivyo ambavyo vitapatikana baada ya shule kufunguliwa,” anasema. Aidha madhumuni makubwa ni kuwakumbusha vijana wa sasa kwamba wadumishe tamaduni za asili na zile kisasa.

Pamoja na hayo mwanzoni wakati wanaanzisha kikundi hamasa haikua kubwa sana lakini baada ya kuanza kutumbuiza hamasa imekuwa kubwa. Dhamira yake ni kufanya kikundi hicho kuwa kikubwa na kitakachokwenda mahali popote kitakapohitajika kwa ajili ya kutoa burudani.

Anaona kwamba kikundi hicho ni chachu kubwa ya wanafunzi kwani kitakuwa ni sehemu ya mazoezi ya kuwafanya vijana wasipotoke na kujiingiza kwenye makundi mbalimbali yasiyofaa. “Pia dhumuni lingine ni kukumbusha wazazi wapi wametoka na wanatakiwa kurithisha asili hiyo kwa watoto wao ili isipotee,” anasema. Chidong’oi anasema kikundi hicho kinaundwa na watu 10 ambao ni wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu.

Akielezea changamoto anasema, amekuwa akibezwa na walimu wenzake kwani wanamuona kama anapoteza muda kwa vitu ambavyo havina maana na walimu wengine wanadiriki kuwaambia wanafunzi wasifike kwenye mazoezi.

“Hilo linadhihirisha kwamba watu hawauthamini utamaduni wanaona kama kitu kisicho na maana lakini kumbe kuna ujumbe na mafundisho mengi kwenye nyimbo za utamaduni vitu ambavyo haviwezi kuachwa vipotee,” anasema.

Pia wamekuwa wakikodisha vifaa wakati wa kutumbukiza hali ambayo hufanya kuingia gharama. “Hatuna sare kwa ajili ya wanafunzi kuchezea ngoma na wanafunzi wamekuwa wakivaa sare za shule wakati wa maonesho hali haioneshi huo ni utamaduni halisi wa Mtanzania,” anasema.

Aidha suala la muda wa mazoezi nalo ni tatizo kwani mara nyingi muda uliopo shuleni ni kwa ajili ya wanafunzi kujisomea na wakati mwingine wanatakiwa kufanya mazoezi. Pamoja na changamoto hizo anaamini siku moja kikundi hicho kitafikia ndoto zake kwa kuwa kikundi bora cha ngoma za asili ambacho kitautangaza vyema Mkoa wa Dodoma.

Mwalimu huyo anasema aliamua kuanzisha kikundi hicho kwani anapenda utamaduni kutoka moyoni mwake kwani tangu akiwa shule ya msingi alikuwa akiimba na kucheza ngoma za Kigogo kama Nindo, Msunyunho, Malimba, Kyamba na ngoma za Muheme. Akielezea historia yake anasema alizaliwa mwanzoni mwa mwaka 1970 katika Kijiji cha Mgunga Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Anatoka familia ya wafugaji wa ng’ombe na kwenda kwake shule ilikuwa ni vigumu sana kwa sababu ya mifugo iliyokuwepo nyumbani kwao hasa kwa babu yake lakini hata hivyo baba yake alifanya jitihada za kumpeleka shule.

Mwalimu huyo anasema alisoma shule ya msingi Mgunga na kumaliza shule ya Msingi Gulwe iliyopo Wilaya ya Mpwapwa mwaka 1993 ambapo alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Pugu iliyopo Jijini Dar es Salaam hadi alipohitimu mwaka 1997 na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Tosamaganga mwaka 1998 ambapo alihitimu kidato cha sita mwaka 2000.

“Hadi kufikia hapa ni vikwazo vingi nimepitia, kwanza nilichelewa kuanza shule ya msingi na hata sekondari nimesoma kwa shida kubwa licha ya mzazi wangu kuwa na uwezo wa kunihudumia,” anasema.

Alipomaliza kidato cha sita alianza kufundisha kwa kujitolea na hatimaye akaenda kuchuku mafunzo ya ualimu wa leseni mwaka 2004 na mwaka 2006 akaanza masomo ya stashahada ya ualimu, chuo cha ualimu Morogoro akahitimu mwaka 2008. Pia aliendelea na shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha St. John ambapo alihitimu mwaka 2011.

“Utamaduni naupenda tangu moyoni hivyo huwa nasikia amani sana nikisikia au kuona ngoma hizo zikichezwa au kuimbwa,” anasema.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi