loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwanamichezo kuwa bonge nyanya ni hatari

Mwanamichezo kuwa bonge nyanya ni hatari

Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia wanamichezo hususan wale wa mchezo wa mpira wa miguu wanaocheza soka la kulipwa, pindi wanapozihama timu zao za awali na kuelekea kwenye timu mpya zilizowasajili wakipimwa afya zao.

Hali kadhalika tumeshuhudia kabla ya mapambano ya ngumi kufanyika, mabondia husika wakipimwa uzito wa miili yao ikiwa ni kigezo kimojawapo cha pambano la ngumi kuweza kufanyika, hii yote ni kutokana na umuhimu wa kupima afya kuwa mkubwa sana hasa kwa wanamichezo kutokana na historia kuonesha namna wanamichezo wanavyopoteza maisha wakiwa ulingoni na viwanjani, huku awali wakionekana kuwa na afya njema.

Kwenye pambano la ngumi uzito wa bondia ndio kigezo kikubwa ambacho kinaamua ubingwa anaoshikilia bondia husika na si vinginevyo. Kutokana na sheria na taratibu za mchezo huo mabondia hawana budi kupimwa uzito kabla ya pambano lao la ngumi kufanyika na iwapo pambano litaahirishwa kwa zaidi ya saa 48 kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika basi mabondia watatakiwa wapime upya uzito kabla ya pambano.

Kuna makundi tofauti ya uzito yaliyopo kwenye ngumi kuanzia uzito mwepesi hadi uzito wa juu. Ni makosa kwa bondia mwenye uzito uliopo kwenye kundi lingine kupambana na bondia ambaye uzito wao haufanani, hii inaweza kusababisha madhara kiafya hasa pale mabondia wanapotofautiana sana uzito, ingawa mapromota wenye tamaa ya kujikusanyia mapato pasipo kujali kitakachompata bondia huwa wanalazimisha pambano lifanyike wakati mabondia wanatofautiana uzito.

Kuna tabia pia ya kutaka kupunguza uzito kwa kasi ya ajabu kwa mabondia ili aweze kushiriki pambano, hii ki afya sio nzuri kwani uzito wa mtu anayekusudia kupunguza uzito wake basi zoezi hili lifanyike taratibu ikibidi kupungua uzito kwa paundi tatu mpaka tano kwa wiki moja sio mbaya.

Vitu ambavyo mara nyingi husababisha wanamichezo au hata watu wa kawaida kuwa na uzito mkubwa ni pamoja na ulaji wa vyakula visivyo na uwiano mzuri wa virutubisho ambapo kwa kawaida, binadamu anapaswa kula mlo kamili, wenye kiwango stahiki cha virutubisho kulingana na mahitaji ya mwili.

Inapotokea mtu akawa anakula kula hovyo vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta kwa wingi au virutubisho vingi kuliko vinavyohitajika na mwili, uzito wa mwili huongezeka na kusababisha tatizo hili. Halikadhalika kutofanya mazoezi ya mwili angalau mara tatu kwa wiki kwa muda usiopungua nusu saa husaidia sana kuchoma mafuta na nishati iliyozidi mwilini.

Inapotokea mtu akawa anakula lakini hafanyi mazoezi, matokeo yake huwa ni kuongezeka kwa uzito wa mwili. Mitindo ya maisha inayosababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa kwenye nchi zilizoendelea, yamesababisha kuongezeka kwa tatizo la watu kuwa na uzito mkubwa wa mwili.

Badala ya mtu kutembea kwa miguu ili kupunguza mafuta yasiyohitajika, utakuta muda mwingi anatumia gari, badala ya kupanda ngazi anatumia lifti, ofisini badala ya kusimama au kutembea, anatumia viti vya kuzunguka vyenye magurudumu. Matokeo yake, chakula unachokula kinakosa kazi na matokeo mafuta yanaanza kurundikana mwilini.

Vinasaba (genes) kwa baadhi ya watu hurithi vinasaba vya unene kutoka kwa wazazi wao na kujikuta wakinenepeana hata kama wanaishi maisha ya dhiki, na pia kuna sababu za kitabibu ambapo baadhi ya dawa wanazopewa wagonjwa kutibu maradhi mbalimbali, husababisha mgonjwa kunenepeana na kuongezeka uzito kwa kiasi kikubwa.

Pia kuna baadhi ya mgonjwa ambayo huambatana na ongezeko la uzito wa mwili. Body Mass Index (BMI) ni kipimo cha unene wa mwili kwa kuangalia urefu wa mtu na uwiano wake wa uzito hasa kwa watu wenye umri wa miaka 18 hadi 65. Kipimo hiki kilianzishwa na mtakwimu wa Kibelgiji Adolphe Quetelet (1796 - 1874).

Kipimo hiki kinakusaidia kujua kama wewe una uzito mkubwa zaidi au la. Ingawa kipimo hicho hakioneshi kiwango cha mafuta mwilini moja kwa moja lakini kinaonesha kiwango cha unene ambao hukadiria hatari ya kupatwa magonjwa mbalimbali. Kipimo cha BMI kinatumika kwa wanawake na wanaume walio na umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Namna ya kujua BMI yako, inatakiwa uchukue uzito ukiwa katika kipimo cha kilogramu, gawanya kwa urefu ukiwa katika mita za mraba. Kiwango cha BMI sawa au chini ya 18.5 kinaonesha kuwa uzito wa mtu ni mdogo chini ya kiwango kinachotakiwa kiafya. Ki- wango cha BMI kikiwa sawa na 18.5 hadi 24.9 kinaonesha kwamba uzito wa mwili ni wa kawaida na unaotakiwa.

Kiwango cha BMI kinapokuwa kati ya 25.0 na 29.9 kinaonesha kuwa mtu ana uzito mkubwa. Lakini kiwango cha BMI kinapokuwa 30 na kuendelea inaonesha kuwa uzito wa mtu ni mkubwa mno. Mbali na BMI vilevile mzunguko wa kiuno au (waist size) unaozidi inchi 40 kwa wanaume na wanawake inchi 35, unaonesha kuwa mtu yuko katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya kama vile kisukari, shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya moyo.

Kuna madhara ya kuwa na uzito mkubwa wa mwili kwani yameenda mbali zaidi na yanagusa mwili, akili na jamii kwa jumla. Madhara ya kiafya yanajumuisha magonjwa ya moyo, kurundikana kwa mafuta ndani ya mwili hususan ndani ya mishipa inayopitisha damu, husababisha kupungua kwa ujazo wa mishipa hiyo hivyo kuzuia damu kuzunguka mwilini kwa urahisi.

Hii husababisha msukumo wa damu kubadilikabadilika, jambo ambalo husababisha shinikizo la damu (blood pressure) na shambulio la moyo. Maumivu ya mgongo, kiuno na viungo kwani mwili unapoongezeka uzito kuliko uwezo wake, husababisha maumivu ya viungo mbalimbali ambavyo huelemewa na uzito wa mwili.

Watu wenye uzito mkubwa husumbuliwa na maumivu ya mgongo, kiuno na viungo vya miguu hususan magoti na vifundo (ankles). Kisukari ambapo mtu anayekula bila mpangilio, bila shaka atakuwa na tabia ya kupenda vitu vyenye sukari kwa wingi, mafuta na kemikali nyingine ambazo huwa na madhara kwa mwili.

Si hivyo tu, mtu mwenye uzito mkubwa, mwili wake hushindwa kuzalisha kichocheo cha insulin ambacho hurekebisha kiwango cha sukari mwilini na kujikuta akiishia kupata ugonjwa wa kisukari. Kiharusi (Stroke) ambapo watu wenye uzito mkubwa wapo kwenye hatari kubwa ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.

Magonjwa mengine wanayoweza kuyapata watu wenye uzito mkubwa ni saratani, angina (kifua kubana), matatizo katika mmeng’enyo wa chakula na Osteoarthritis.

Madhara ya kiakili, ambapo mtu mwenye uzito mkubwa, huwa katika hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa kama kupoteza kumbukumbu, kusumbuliwa na msongo wa mawazo mara kwa mara, kushindwa kujiamini na kushindwa kudhibiti hasira au mshtuko na kujikuta wakizimia au kupoteza fahamu wanaposhtuliwa au kupokea taarifa mbaya kama misiba, ajali na kadhalika.

Madhara ya kijamii ambapo watu wenye uzito mkubwa wa miili, wanaelezwa kuwa wavivu katika masuala ya uzalishaji kutokana na kuelemewa na uzito wa miili yao. Wataalam wamebaini kuwa watu wenye uzito mkubwa wa miili, huchoka haraka hata wakifanya kazi ndogo na hivyo kupunguza kasi ya shughuli za uzalishaji.

Pia watu wenye uzito mkubwa wa miili hukumbwa na unyanyapaa kutoka wa jamii. Wengi huzomewa wanapotembea mitaani, kuchekwa au kushangawa sana, jambo ambalo huwaumiza na kuwafanya wajione kama jamii haiwakubali na sasa wanasema vijana wa mjini kitambi noma.

Hivyo kwa wanamichezo na hata watu wa kawaida suala la kupima uzito lina umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku, kwani kuongezeka au kupungua kwa uzito kuna maana yake. Upungufu wa uzito unaweza kuwa kiashiria au hatua ya mwanzo ya upungufu wa lishe bora anayotakiwa kuipata mhusika.

Suala la kupima uzito linaanzia kwa mama mjamzito na hata baada ya kujifungua mtoto naye anakwenda kliniki kupima uzito. Kwa wale waliobahatika kuzichunguza kadi za kliniki ni dhahiri kuwa watakuwa wameona kielelezo kinachoonesha ukuaji wa mtoto kwa kutumia kupima uzito aliokuwa nao.

Kadi hizi kutokana na vidokezo vya hatari vilivyoainishwa ambapo pia kuna hatua za kuchukuliwa kwa mfano kwenye rangi nyekundu kukiwa na nukta ya uzito kwenye eneo hilo basi mtoto hana budi apelekwe kwa daktari hospitalini ili kuweza kutatua tatizo alilokuwa nalo.

Ndio kusema wanamichezo inabidi wazingatie suala la kupima afya ikiwa ni pamoja na uzito wa miili yao kwa faida yao binafsi kwani, watu wenye uzito mkubwa uliopitiliza kiwango hawana tofauti na bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote kwa maradhi. Mwandishi ni mtaalamu wa sayansi za afya na mazingira kutoka Chuo cha Afya Mpwapwa.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Osmund Mbangati

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi