loader
Picha

Mwongozo mpya udahili kidato 5 uzingatiwe

Kwa mujibu wa taarifa katika vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, kutokana na mwongozo huo, sasa wanafunzi wenye umri wa zaidi ya miaka 25 hawaruhusiwi kudahiliwa kuingia kidato cha tano.

Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Ave-Maria Semakafu katika taarifa hiyo, alivitaja vigezo vingine vya udahili huo kuwa ni pamoja na mhitimu wa kidato cha nne kuwa na ufaulu wa masomo yasiyopungua matatu.

Ufaulu katika masomo hayo unapaswa kuwa katika kiwango cha A, B au C katika masomo yasiyokuwa ya dini katika mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari ya kidato cha nne. Kigezo kingine kwa mujibu wa wizara, taarifa hiyo ilisema ni mhitimu wa sekondari kupata alama (pointi) za ufaulu katika masomo saba zisizozidi 25.

Wizara kupitia kwa Dk Semakafu ilisema kabla ya mwanafunzi kudahiliwa, lazima jumla ya alama zake za ufaulu katika masomo ya tahasusi ziwe kati ya tatu hadi 10, na kusiwepo na alama ya ‘F’ katika somo lolote kati ya masomo hayo ya tahasusi.

Taarifa ilibainisha kuwa, kipo kigezo kingine ambacho kinaelezea kuwa, wanafunzi pia watadahiliwa kiushindani kulingana na vigezo vitakavyowekwa na shule husika ambayo mwanafunzi ameomba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi wenye sifa linganishi ambao matokeo yao ya mitihani siyo yale ya kutokea Baraza la Mitihani la Taifa, waombaji wa udahili watatakiwa kutumia matokeo yaliyofanyiwa ulinganifu na Baraza la Mitihani la Taifa.

Sisi tunasema, tunaipongeza serikali kwa kubuni na kuweka vigezo vya udahili vitakavyowachochea wanafunzi wa shule za sekondari, kusoma kwa umakini na kuelewa ipasavyo ili wapate sifa za udahili, tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo wengine waliweza kusoma kwa mtindo wa ‘bora liende’, na bado wakadahiliwa kuingia kidato cha tano.

Matokeo ya hali hiyo, wengine walikuwa mzigo kwa walimu hata kwa masomo ya tahasusi jambo ambalo, halioneshi nuru ya kielimu kwa siku za usoni.

Tunasema, hii itawafanya wanafunzi hao kuepuka kusoma kwa upendeleo na ubaguzi wa masomo hali imechangia wanafunzi wengine kupata ugumu wanapokutana na masomo waliyopuuza katika siku za usoni hususan wanapolazimika kutumia elimu waliyoipata.

Kwa msingi huo, tunawasihi wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wenyewe hususani ambao watoto wao ama wanafunzi wenyewe wako kidato cha nne na cha tatu, kuanza upya na kuweka mkazo wa pekee kuuelewa na kuuzingatia mwongozo huu ili zamu yao ikifika, wasione cha ajabu.

Wakati tukiwatakia mema katika masomo na mitihani yote ijayo, tunapenda kuwasisitiza wadau wote wakiwamo hasa wanafunzi wa sekondari tukisema: “Sekondari zingatieni mwongozo mpya udahili kidato cha tano.”

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi