loader
Dstv Habarileo  Mobile
Namna Foundation for Civil Society ilivyoinua wananchi

Namna Foundation for Civil Society ilivyoinua wananchi

Hivi karibuni shirika hili lilikutanisha wadau wake ambao ni Asasi za Kiraia (AZAKi) kusherehekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Katika mkutano huo mbali na kusherehekea miaka hiyo mambo mbalimbali yalijadiliwa kwa lengo la kujenga taasisi na kumkomboa Mtanzania.

Shirika hilo limejikita katika kuwawezesha wananchi kuwa na msukumo imara wa kuleta mabadiliko katika kuboresha utawala wa kidemokrasia nchini kupitia mafunzo mbalimbali na pia miradi. Hata hivyo katika mkutano huo wa siku tatu uliohitimishwa na hafla ya kusherehekea miaka kumi toka kuanzishwa kwake, Rais wa shirika hilo, Stigmata Tenga, alizikumbusha asasi kubuni njia mbalimbali zitakazoweza kuziingizia asasi hizi kipato.

Tenga alisema, ni wakati sasa Asasi zinatakiwa kusimama imara kuepuka fedha zinazotoka kwa wafadhili kwa kubuni miradi ili kujiletea maendeleo wao wenyewe.

“Ni wakati sasa wa kusimama na kuangalia namna ya kutafuta vyanzo mbalimbali vya kujiingizia fedha kwasababu fedha za wahisani zinashuka kila kukicha na kwa mwaka huu imeshuka zaidi, hii ni hatari kama hatutakua na njia za kujisaidia,” anasema Tenga. Anasema shirika linajivunia matunda ya msaada kwa AZAKi kwa kuhamashisha wananchi katika maendeleo yao wenyewe.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, John Ulanga, anasema mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania uliliongezea shughuli za kufanya shirika hilo. Akifafanua anasema, kwa mwaka huu kulikuwa na maombi mengi sana ya Katiba pamoja na kwamba fedha zilizokuwepo ni kidogo lakini shirika lilijipangia kutoa kipaumbele kwa Katiba na kusimamisha miradi mingine.

“Msifikiri kwamba tulikuwa tukipuuza maombi yenu, hapana hali haikuwa hivyo, maombi tulikuwa tukipokea mengi ya miradi lakini fedha haikuwa ya kutosha,” alisema Ulanga. Anasema bajeti kwa mwaka ilikuwa ni dola milioni 15 lakini fedha ambazo wamezipokea mpaka sasa ni Sh bilioni 12 hivyo kuna nakisi kubwa.

“Wafadhili hivi sasa nao wako kwenye mkutano kuona kama watatupatia fedha zilizobaki, tusipozipata itabidi tuangalie tutakapopunguza matumizi, mkiona hampati majibu ya maombi yenu sio kwamba tunafanya uzembe,” alisema Ulanga. Alisema hata hivyo mwaka huu asasi hizo zilivunja rekodi ya maombi ya fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya kwa sababu ilipewa kipaumbele.

Ulanga anasema mafanikio yaliyopatikana katika jamii katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Foundation for Civil Society kuwa ni kubwa na hivyo kutoa mchango mkubwa kwa Serikali. Anasema zaidi ya Watanzania milioni nane wamefikiwa kwa namna moja au nyingine na wanaruzuku wanaowezeshwa na shirika hilo katika eneo la sera, utawala bora na uwajibikaji.

Anasema asasi kuendesha kampeni na kuwafikia watu wengi katika wilaya mbalimbali na kuwaelimisha kuhusu haki za wazee na kuwaelimisha watu kuhusu umiliki wa ardhi. Ulanga anasema mwaka jana ufadhili wa shirika hilo kwa AZAKi uliwezesha zaidi ya watu 320,000 kushiriki kwenye midahalo ya kujadili masuala muhimu yaliyoingizwa kwenye rasimu ya Katiba mpya.

Anasema kati ya wananchi waliotoa maoni yao kwenye Katiba mpya kupitia asasi hizo, watu 48,579 wenye ulemavu walishiriki na asilimia 70 ya maoni yao yaliingizwa kwenye rasimu ya Katiba mpya. Kwa mujibu wa Ulanga, shirika hilo limewezesha kuruka hewani katika vyombo vya habari midahalo ya Katiba ili kuhakikisha watu wanaoishi vijijini wanafikiwa.

Aidha kwa mwaka jana Ulanga anasema shuguli zilizotekelezwa ziliwekwa katika msisitizo wa kuyafikia maeneo makuu ya matokeo ya Mpango Mkakati wa mwaka 2009 hadi 2013, ambayo ni ushiriki katika sera, utawala bora na uwajibikaji na kuimarisha uwezo wa AZAKi.

Asasi zilizolenga kushughulikia masuala ya sera zilijikita kwenye mahitaji muhimu kwa makundi yanayoishi katika mazingira hatarishi, afya, maji, mazingira, ardhi, tija katika kilimo, elimu na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

“Masuala ya sera yaliwalenga zaidi wazee, watu wenye ulemavu, watoto, vijana na watu wanaoishi na VVU kwa kuhakikisha wanashiriki kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya nchi,” anasema Ulanga. Aidha katika watu 3,740,511 walifikiwa wanawake walikuwa 139,913.

“Eneo hili kuu la matokeo lilitumia Sh bilioni 6.1 ya fedha iliyotolewa mwaka 2012, matokeo yalikuwa mazuri, kwani asilimia 80 ya walengwa walisema wameshawishi angalau sera moja na asilimia 60 walisema wameleta mabadiliko kwa kutamka hadharani maoni yao kuhusu masuala ya jamii yanayowahusu,” “Kupitia ufadhili wetu wa midahalo ya Katiba, maendeleo yalionekana kwa jinsi wananchi wanavyojihusisha kwenye masuala ya sera kwa kuweka masilahi ya taifa kwanza,” anasema Ulanga.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Regina Kumba

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi