loader
Dstv Habarileo  Mobile
Namna Mwanza ‘walivyofyeka’ maambukizi ya Ukimwi

Namna Mwanza ‘walivyofyeka’ maambukizi ya Ukimwi

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Francis Mkanbenga wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, zilizofanyika Mkuyuni jijini Mwanza. Mkanbenga anasema kuwa kupungua kwa maambukizi hayo, kumetokana na watu kuitikia mwitikio wa huduma mbambali za kiafya zinazotolewa na watumishi wa afya, zikiwemo za kujitokeza kwa hiari kwenda kupima afya zao.

Anasema hali hiyo ilisababisha idadi ya watu wanaotumia huduma za ushauri nasaha na upimaji wa hiari kuongezeka kwa asilimia 21.3 ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo wateja 68, 972 ( wanawake wakiwa 29,896 na wanaume 39,076) waliojitokeza kupima afya zao, wateja 5,509 , wanaume wakiwa 2,153 na wanawake 3,356 walikutwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Hii ni dalili njema kuwa watu wanaelewa umuhimu wa kuchunguza afya zao hii ni jitihada zinazofanywa na wadau na serikali kuhamasisha jamii kujitokeza kupima afya zao”, anasema na kuongeza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kwa Ukimwi, waathirika wa Ukimwi ili waweze kupaza sauti zao kwa kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na maambukizi mapya.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi kwa mwaka huu ni “Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi inawezekana”, ambapo katika kutekeleza kauli hiyo, Mkanbenga anasema moja ya mipango iliyowekwa na halmashauri katika kuitekeleza kauli mbiu hiyo ni pamoja na kujenga uwezo wa vikundi vya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili viondokane na utegemezi wa kiuchumi na kuwasaidia watoto wanaoishi na katika mazingira magumu.

“Tutajenga uwezo wa wadau mbalimbali kwa kuwapatia fedha ili kuimarisha shughuli za Ukimwi katika jiji letu, ambapo kiwango cha fedha hicho kimeongezeka kutoka Sh milioni 9 kwa mwaka 2005/06 hadi Sh milioni 78.5 kwa mwaka 2012/13”, anasema. Anasema kati ya vikundi 14 vya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi jijini Mwanza, vikundi 12 vimefadhiliwa kiasi cha Sh milioni 14 kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.

Anasema katika kupambana na Ukimwi, Jiji limejipanga kupunguza maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi kwa makundi maalum yaliyo katika hatari ya kuambukiza au kuambukizwa Ukimwi. Anayataja makundi hayo kuwa ni pamoja na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaouza miili yao, watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na madereva wa pikipiki (bodaboda) na baiskeli.

Aidha Jiji limedhamiria pia kupunguza unyanyapaa hadi kufikia sifuri na kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi.

“Ili kutimiza azma hii, Jiji litaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wadau wafanye kazi zao vizuri kwa ushirikiano ili kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi”, anasema.

Kwa upande wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi, kupitia risala yao iliyoandaliwa na Kamati Tendaji iliyosomwa na Suzana Daudi, waliwashukuru viongozi wa madhehebu ya dini, kitaifa, mkoa, wilaya , kata hadi mtaa , Azaki na wananchi kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye maadhimisho hayo ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Suzana anasema kuwa siku hiyo inawakumbusha wadau na wananchi kwa ujumla kupanga mikakati endelevu ya kuzuia maambukizi mapya, kuzuia unyanyapaa na kukabiliana na vifo vitokanavyo na Ukimwi.

“Tunazishukuru asasi zisizo za kiserikali na taasisi mbalimbali zilizo na dawati la Ukimwi sehemu zao za kazi, Kamati za Ukimwi ngazi mbalimbali kwa jitihada zao za kuhamasisha wafanyakazi na jamii kushiriki kikamilifu kwenye harakati dhidi ya VVU/ UKIMWI na athari zake”, anafafanua na kuzitaja baadhi ya asasi hizo kuuwa ni Baylor –Bugando, The Desk and Chair Foundation, Bilal Muslim Tanzania, Africa Probiotic Yoghurt Network (APYN), Peace and Development for Muslims (PDM), Shirika la kutetea haki za wanawake la Kivulini na dawati la jinsia la OCD Wilaya ya Nyamagana.

Anatoa shukrani za pekee kwa Jiji la Mwanza kwa kuunganisha watu wenye virusi vya Ukimwi na wadau wengine na kuwafanya wamoja kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kutekeleza mipango ya Ukimwi na maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani ambayo huadhimishwa Desemba 1 kila mwaka, kiasi cha Sh 47.6 kimetumiwa na wadau mbalimbali kwa maadhimisho ya Wiki ya Ukimwi jijini Mwanza.

Suzana anasema vimekuwepo vikwazo vinavyokwamisha shughuli za kudhibiti Ukimwi jijini Mwanza, ambavyo vimekuwa vikiwakwamisha wadau na waathirika wa Ukimwi. Anavitaja vikwazo hivyo kuwa ni upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuimarisha mapambano ya VVU na UKIMWI kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na wadau.

“Vikwazo vingine ni jamii kutowajibika ipasavyo katika kuwasaidia watoto yatima, wajane, wagane na wagonjwa wa Ukimwi kutokana na ubaguzi na unyanyapaa ambao bado uko miongoni mwa wakazi wa jiji la Mwanza kutokana na utegemezi uliojengeka kwa jamii”, anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, anautaka uongozi wa Jiji la Mwanza kuweka mipango shirikishi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na wilaya dhidi ya mapambano ya Ukimwi. Anasema hali hiyo itapunguza maambukizi mapya ya Ukimwi kuanzia ngazi ya familia, kaya, ukoo, mtaa, kijiji, kata hadi taifa.

“Shirikisheni wananchi kuanzia ngazi ya mtaa, mkifanya hivyo unyanyapaa na vita dhidi ya Ukimwi na Tanzania bila ya Ukimwi inawezekana”, anasema na kulishukuru Jiji la Mwanza na wadau walio katika mapambano ya Ukimwi kwa kuleta mabadiliko chanya katika mahusiano ya kujaamiana kwa kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi kwa asilimia 7.8.

Konisaga anasema kuwa tathmini mbalimbali bado zinaonesha kuwa bado kuna mianya ya mtu kuambukiza VVU katika jamii kupitia ngono zembe kutoka kwa mtu aliyeambukizwa VVU.

Anasema sababu inayochangia kuwepo kwa hali hiyo ni pamoja na mila na desturi za kurithi wajane, wasichana kufanyiwa ukeketaji, mwanamke kuoa mke mwenzake huku akihudumiwa na mume mwingine kwa tendo la ndoa (nyumba ntobu), utakasaji wa wajane, ulevi na umasikini unaoambatana na tamaa.

Anaziomba asasi za kiraia, kamati za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi zote, viongozi wa madhehebu ya dini na wa kisiasa na wadau mbalimbali waendelee kuhamasisha jamii dhidi ya maambukizi mapya. Anaitaka jamii kuwajali na kuwathamini watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kutetea haki zao, kama za binadamu wengine, kuondoa sheria za kibaguzi kwa mtu aliye na VVU na kuhimiza usawa wa kijinsia.

“Tunahimizwa kuimarisha huduma za nyumbani , ufuasi wa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV’s) kwa wanaozitumia, lishe bora kwa Waviu, kubuni miradi ya kujiongezea kipato kwa waviu, kuimarisha upendo kwa waathirika na afua za Ukimwi mahala pa kazi”, anahitimisha Konisaga.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi