loader
Dstv Habarileo  Mobile
Nani Mtani Jembe: Simba, Yanga ni patashika

Nani Mtani Jembe: Simba, Yanga ni patashika

Mechi hiyo maalumu imeandaliwa na wadhamini wa timu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambapo mbali na zawadi ya Sh milioni 100, kingine ni kuongeza hamasa iliyopo kwa timu hizo ambazo zinaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi kuliko timu nyingine hapa nchini.

Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kuona kama mechi hiyo itakuwa ya kawaida kutokana na baadhi ya watu kuchukulia kama mchezo wa kirafiki, na timu hizo kuweka upinzani wao pembeni . Nikuhakikishie hilo halitokuwepo kwenye mchezo huo, kwanza kwa mujibu wa waandaaji, mshindi lazima apatikane na siku zote Simba na Yanga haziwezi kucheza mechi ya kirafiki kutokana na uhasama uliopo baina ya timu hizo.

Unapozungumzia ushindani wa Simba na Yanga ni sawa na kuzungumzia na El Clasico ya Hispania ambayo inazihusisha FC Barcelona na Real Madrid au Liverpool na Manchester United za Uingereza na kwa Italia kwenye Seria A unaweza kuzitaja AC Milan na Inter Milan lakini tofauti ya upinzani kati ya timu hizo za wenzetu na hizi za kwetu ni kiwango cha soka.

Ushindani wa timu hizi mbili unaonesha ile timu dhaifu ndiyo inayopata ushindi bila kujali uimara wa upande wa pili, lakini ni mara chache sana mwamuzi anaye pangwa kuchezesha mechi yao kukosa lawama kutokana na kila upande kuamini mwamuzi anaibeba timu pinzani.

Ni vigumu kutabiri timu gani kati ya hizo mbili itaibuka na ushindi japokuwa Yanga ina nafasi kubwa ya kuondoka na Sh milioni 100 kutokana na uimara wa kikosi ilichonacho. Kwa sasa Simba kwa asilimia kubwa inaundwa na wachezaji chipukizi ambao hawana uzoefu wa mechi zenye ushindani kama hiyo ya leo.

Waswahili husema soka linadunda na Yanga ikiwa na kikosi chake kilichokamilika inaweza kupoteza mchezo wa leo, lakini ukweli ni kwamba Simba bado ina mapungufu mengi ukianzia kwenye benchi la ufundi, kocha Zdrovko Logarusic bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inakuwa sawa na kufanya vizuri kwenye mechi hiyo pamoja na zile za ligi kuu.

Zoezi ambalo nahisi litakuwa gumu kwa Logarusic kuwepo kwa idadi kubwa ya wachezaji wageni kwenye kikosi chake ambao kwa mwonekano wa haraka lazima watatakiwa kuingizwa ndani ya timu haraka kulingana na mapungufu yaliyopo kwa sasa.

Kingine ni mgogoro uliopo ndani ya klabu hiyo ambao unatokana na uongozi wa juu, Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji kutokuwa na maelewano mazuri na kuwepo na malumbano kila kukicha na kuiweka timu hiyo katika wakati mgumu zaidi akiwepo na kocha Logarusic.

Kutokana na hilo, Logarusic katika mechi ya leo atakuwa akifanya kazi mbili kwa wakati mmoja kwanza kuipanga timu hiyo icheze kwa kuelewana lakini ya pili ni kutaka ushindi, kitu ambacho siyo rahisi unapocheza na timu yenye wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu na wenye uzoefu kama wa Yanga japo akishinda atastahili pongezi.

Tofauti ya Logarusic na Ernie Brandts wa Yanga ni uzoefu wa kuijua vizuri Ligi ya Tanzania bara na kuifahamu timu unayokwenda kupambana nayo hiyo ndiyo faida aliyokuwa nayo Brandts katika mchezo wa leo ambaye naye ilimkuta wakati anakabidhiwa timu mwanzoni wa ligi ya msimu uliopita mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Simba japo aliweza kuambulia sare ya bao 1-1 na mechi ya pili alishinda mabao 2-0 lakini alikuwa tayari ameizoea timu pamoja na ligi yenyewe.

Mara ya mwisho, Simba na Yanga kukutana ilikuwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Oktoba 20 mwaka huu ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3, Yanga ikitangulia kufunga mabao yote kipindi cha kwanza na Simba ikasawazisha kipindi cha pili.

Takwimu za kupata matokeo mazuri kwenye mechi za Simba na Yanga zinambeba Brandts kwani tangu alipoanza kuinoa timu hiyo Septemba mwaka jana, amekutana na Simba mara tatu ameshinda mechi moja na kutoka sare mbili.

Lakini mbali na hilo rekodi nyingine zinazo husisha mechi za Simba na Yanga katika kipindi cha miaka saba iliyopita, inaonesha Yanga imeshinda mara nyingi zaidi ya Simba ambayo ushindi wake mkubwa iliyoupata mara ya mwisho ni msimu uliopita ambapo ilishinda mabao 5-0 dhidi ya mpinzani wake huyo.

Rekodi hizo zinaonesha Simba iliinyanyasa Yanga kuanzia Julai 8, 2007 katika mechi iliyofanyika uwanja wa Jamhuri Morogoro ambapo Simba ilishinda kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 kwenye muda wa kawaida katika mchezo huo, Mkenya Moses Odhiambo ndiye aliyeanza kuifungia Simba dakika ya pili kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa Saidi Maulid dakika 55.

Oktoba 24 mwaka 2007 Simba iliifunga tena Yanga bao 1-0 mechi hii ilifanyika tena uwanja wa Jamhuri katika mchezo huo bao la Simba lilifungwa na Ulimboka Mwakingwe lakini Yanga ilijitutumua na kuambulia suluhu katika mechi iliyochezwa Aprili 27 mwaka 2008. Mwaka huohuo, Oktoba 26 Yanga walipata ushindi wakiwa wanakutana na Simba kwa mara ya kwanza kwenye uwanja mpya wa Taifa, Ben Mwalala wakati huo akifunga bao hilo.

Timu hizo zilikutana tena Aprili 19, mwaka 2009 ukiwa ni mchezo wa kufungia msimu Simba ilipambana na kufanikiwa kupata sare ya mabao 2-2 mabao yao yakifungwa na Ramadhani Chombo na Haruna Moshi ‘Boban’ huku yale ya Yanga yakifungwa na Mwalala tena na Jeryson Tegete.

Hizo ni baadhi ya mechi chache zilizopo kwenye rekodi za Simba na Yanga katika kipindi hicho cha miaka saba japo katika mchezo wa soka rekodi haina nafasi sana na inategemeana na maandalizi ya timu namna ilivyojiandaa pamoja na aina ya wachezaji iliyokuwa nao.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi