loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Natamani Mwigulu asaidiwe katika vita hii

Vita hiyo itakayokwenda sanjari na kuwakamata wafuja fedha za umma, ilitangazwa hivi karibuni jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alipokuwa katika ziara yake ya kikazi jijini Mwanza.

Katika vita hiyo, Mwigulu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) anasema kuanzia wakati huu Serikali itakuwa makini kwa kile alichokiita kuwa ni “Ulaji katika manunuzi ya umma,” akilenga zaidi hujuma zinazofanywa katika ununuzi wa magari ya umma, utengenezaji na vipuri vyake ambapo alikiri kuwa ununuzi na utengezaji huo unaligharimu taifa kwa vile umekuwa ukifanywa kwa mabilioni ya fedha.

Mwigulu alienda mbali zaidi na kushangaa kuona, Waziri akitumia gari lenye thamani ya Sh bilioni 270 kutoka nyumbani kwake kumpeleka ofisini na kueleza bayana kuwa kiasi hicho cha fedha kingeweza kujenga zahanati moja ambayo ingeweza kuwahudumia wananchi.

Kwa tafsiri ya Nchemba zahanati hiyo ingewasaidia akinamama wajawazito wanaojifungulia barabarani, wanaolazwa sakafuni wadini na wale wanaochangia kitanda kimoja wajawazito watatu. Kauli ya hii ya Nchemba ni kauli nzito inayohitaji uzalendo na nia njema ya kupigania rasilimali na fedha za umma, sio nia ya makala haya kupinga juhudi hizo za Nchemba bali ni kubainisha changamoto zilizopo katika kufanikisha vita hii.

Nilivyomsikia akiitoa kauli hiyo pale uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, binafsi nilimruhumia kwa sababu Nchemba aligusa eneo ambalo limekuwa ni mradi wa siku nyingi wa baadhi ya vigogo si katika halmashauri wala Serikali Kuu katika nchi hii.

“Serikali itakuwa makini katika kuondoa ulaji katika manunuzi ya umma, hasa magari ambayo yananunuliwa na kutengenezwa kwa gharama kubwa,” alisema Nchemba.

Kauli hii ni nzito inayohitaji uzalendo na upendo wa kweli, inayostahili kwenda kwa kizazi kinachowachukia watu wanaohujumu fedha na mali za umma, wanaokwepa kulipa kodi na kiwe tayari kuwaibua na kuwasema hadharani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake ili vita aliyoanzisha Mwigulu Nchemba iweze kufanikiwa.

Ni kauli pia inayowataka watendaji wa Serikali, kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi Serikali Kuu ‘kunia mamoja’ nikiwa na maana kuwa na mpango mkakati unaolenga kuokoa mamilioni ya fedha ambayo yamekuwa yakifujwa na baadhi ya watu. Mwigulu aligusia suala la upelekaji wa fedha za dawa na umeme kwa wananchi kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma hizo kwa wakati.

Lakini kwa suala la dawa kuna ucheleweshaji mkubwa wa dawa hizo kuwafikia wananchi kutokana na changamoto za kimfumo zilizopo ambazo hufanya Bohari ya Dawa nchini(Msd) kushindwa kufikisha vifaa tiba kwa wakati.

Kwa tafsiri ndogo juu ya kile alichokisema Nchemba dhidi ya magari ya umma na vipuri vyake, anaamanisha kuwa ununuzi huo umekuwa ukifanywa kwa mabilioni ya fedha, akilinganisha na hali halisi ya maisha ya Watanzania.

Alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakati fulani akishangaa kuona mtumishi wa umma akitumia kiasi kikubwa cha fedha pale anapotumia gari la Serikali tofauti na gari lake binafsi, hali inayoashiria kuwa mtumishi wa aina hiyo huongeza cha juu pale anapoenda kuchukua risiti halali za ununuzi wa mafuta ya ofisi.

Na mfumo huo wa ufujaji wa mali za umma umekuwa sugu kutokana na baadhi nya watendaji kutumia kigezo cha uwasilishaji (retirement) wa stakabadhi za matumizi. Kwa sisi tunaoandika habari za uchumi, mfumo huu umeingia hadi kwenye maisha ya wanasiasa.

Mfumo huo umerithiwa na baadhi ya watumishi kuanzia ngazi ya halmashauri hadi Serikali Kuu, kiasi kwamba ili uondolewe ni lazima vita aliyoanzisha Mwigulu Nchemba iwe ni vita ya watu makini walioapishwa kiapo cha utii cha kusimamia fedha za umma, vinginevyo itakuwa ni ngumu kuitekeleza.

Nasema hivyo kutokana na sababu zifuatazo, ni mara ngapi tumesikia taarifa za watumishi kulipwa mishahara hewa ambayo inatolewa na watendaji (wataalamu) wa Serikali tena bila ya hofu! Ni mara ngapi tumesikia ufujaji wa mabilioni ya fedha katika halmashauri zetu, ambapo taarifa huishia katika kuundwa kwa tume ambazo tena hupewa mabilioni ya fedha katika kuchunguza wizi uliofanywa na watumishi hao hao!

Hali hii ni sawa na mtu kuukata mti alioukalia mwenyewe maana ukianguka unaanguka na yeye. Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali inayohusu ukaguzi wa fedha za Serikali za miradi ya maendeleo inayoishia Juni 30 mwaka 2013, ambayo ilitolewa mwezi Machi mwaka huu inaonesha kuwa kumekuwepo na udhaifu mkubwa katika usimamizi wa fedha za umma.

Taarifa hiyo inaonesha kasoro zinazotokana na usimamizi wa fedha usioridhisha nchini kwa idara na taasisi zake zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika mwaka wa fedha wa 2011/12 mapungufu hayo yalikuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5 na katika mwaka 2012/13 yalifikia bilioni 18.8.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mapungufu kwa upande wa mchakato wa manunuzi ya umma, miradi mikubwa yote haikufuata kikamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 21 ya Mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005 kutokana na baadhi ya watendaji kutokuwa na kiwango stahiki cha kuielewa sheria hiyo na kanuni zake na hivyo kufanya baadhi ya matumizi ya fedha kutumika ndivyo sivyo.

Kwa mfano, ripoti inabainisha kuwa kinyume na kanuni Na. 68(5) ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004, halmashauri mbili zilinunua bidhaa, vifaa na huduma za gharama ya Sh milioni 19.2 kutoka kwa wazabuni wasiorodheshwa ambao walipitishwa na Wakala wa Manunuzi wa Umma (GPSA) bila ya bodi ya zabuni ya halmashauri husika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 13.3 zilinunuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa bila kushindanisha wazabuni kinyume na kanuni Na. 68(4) ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Na kiasi cha Sh milioni 48.1 kilitumika katika matumizi ambayo hayahusiani na malengo ya miradi. Hali hiyo ilisababisha halmashauri mbili pamoja na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa kubainika kutumia kiasi hicho cha fedha kwa malengo ambayo hayakusudiwa. Ripoti hiyo inabainisha kuwa kumekuwa na tatizo la kubwa la kutofuata matakwa ya vipengele vilivyoainishwa kwenye mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na wahisani.

Vipengele hivi husisitiza umuhimu wa kutii na kuzifuata sheria na taratibu za fedha na manunuzi, ambapo kwa ukaguzi uliofanywa mwaka jana jumla ya kasoro zilibainika kwenye masuala ya ununuzi zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 32 na Dola za Marekani USD 114,806 ambapo kasoro zilizoonekana katika usimamizi wa fedha zilikuwa na thamani ya Sh bilioni 19 na USD 3, 391, 816.

Kasoro zilizobainishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ndiyo ambayo Mwigulu kwa kushirikiana na viongozi wa Wizara yake, Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na watendaji wote wa wizara wanatakiwa kwa kutanguliza uzalendo waanze nazo, vinginevyo vita aliyoianzisha itakuwa ngumu.

Mwigulu atambue kuwa watu wanaofuja fedha na mali za umma hawakuanza leo wala jana, hawa ni watu walio na mizizi mikuu. Wanajua mbinu na wana mitandao mipana ya kuifanya kazi hiyo na ni watu wanaoungwa mkono na jamii pia.

Leo hii ni rahisi kusikia mtu anasifiwa pale tu ama anapokuwa ameajiriwa au kuteuliwa serikalini kwa muda mfupi, ama akajenga nyumba ya kifahari, kununua gari ama chochote kile ambacho kiko nje ya uwezo wake, huyo huitwa mwanamume wa shoka! “Fulani bwana jembe, umeona ghorofa alilojenga Masaki, Mbezi, Nyegezi, Ujiji, Shinyanga, Mbeya, Morogoro mji kasoro bahari, acha bwana lile ni jembe,” husikika wakitoa kauli za namna hiyo.

Wenzetu katika nchi zilizoendelea kiasi cha fedha za matumizi ya ofisi ya mtumishi na ya maendeleo huwekwa hadharani na wananchi hujua ni miradi ipi inayostahili kutengenezwa na kwa wakati gani na wako makini kufuatilia na kuhoji.

Na watumishi wa umma huwa tayari kuwajibika pale tu itakapothibitika kuwa fedha za umma zilizoidhinishwa chini ya idara, eneo ama wizara wanazoziongoza zimefujwa ama hazikutekeleza kwa ufanisi miradi ya maendeleo iliyokusudiwa.

Mtaalamu mmoja wa uchumi nchini Japan hivi karibuni, amenukuliwa na vyombo vya habari vya Magharibi akilia na kuwaomba radhi wananchi wa Japan, pale ilipothibitika alitumia kinyume fedha alizotengewa na serikali.

Nilipoamuangalia kupitia TV alikuwa ananilia kwa uchungu, kiasi kwamba mmoja wa wananchi wa Japan, aliyehojiwa alisema kuwa mtaalamu huyo anaweza kusamehewa kwa kitendo alichokifanya cha kufuja fedha hizo kutokana na jinsi yeye mwenyewe alivyokerwa nacho.

Uharibifu wa mali na fedha za umma, ni mfumo shirikishi ambao haumhusu mtu mmoja, kwa ufahamu wangu mdogo ni kuwa ili hundi ya serikali ya mabilioni ya fedha iweze kutolewa inahusisha watu wengi kwa ajili ya kuweka sahihi (Signatory), haiwezekani kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 5 kwa mfano kifujwe katika wizara au halmashauri na mtu mmoja ambaye hana mtandao wa kuufanya ufisadi huo.

Ni dhahiri kuwa ufujaji wa fedha huo hufanywa kwa njia ya kimfumo na mtandao na ndio maana nasema juhudi hizi za Mwigulu za kudhibiti vita dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma hasa kwa ununuzi wa magari lazima zifanywe kisayansi kwa kuwatafuta watumishi wa umma wenye uzalendo na mapenzi mema ya nchi hii.

Hivi ni nani hajui kuwa magari mapya ya serikali hutembea kwa muda mfupi na baadaye huwekwa kwenye ghala la serikali kwa madai kuwa gari limeharibika kwa kisingizio cha kukosa vipuri.

Kinachofuata baadaye ni gari kuuzwa kwa bei ndogo katika mnada wa Serikali na kibaya zaidi hununuliwa na wale waliokuwa wakilitumia gari husika. Hali hii inatuonesha kuwa vita hii aliyoanzisha Mwigulu inahitaji kuungwa mkono na watu wenye uzalendo na nchi yao na ndio maana nasema Mwigulu asaidiwe katika vita hii ngumu aliyoitangaza.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi