loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndonya, utamaduni wa Wagogo unaopotea

Kwa mujibu wa Chifu wa Makulu Dodoma, Ally Biringi, miongoni mwa mila na desturi za Wagogo zinazopotea kwa kasi ni ndonya sambamba na kuchanja chale usoni.

Anasema kwa miaka mingi, Mgogo alikuwa akitambulishwa kwa ndonya. Ndonya inavyopatikana Kuhusu jinsi ndonya inavyopatikana, Chifu Biringi anasema hutafutwa kikonyo cha mbuyu ambapo huwekwa kwenye moto na wakati unawaka kikonyo hicho huwekwa juu ya paji la uso mara moja tu na baada ya hapo ndipo ndonya hutokea.

Anazitaja sababu za kabila hilo kuweka ndonya kwamba mbali na utambulisho wao kimila ni imani kwamba hawaumwi ugonjwa wa macho. Ilikuwa inaaminika pia kwamba mtu mwenye ndonya, haumwi kichwa.

Anasema kimsingi mtoto akiwa bado mdogo kuanzia mwaka moja na kuendelea ndipo alikuwa akiwekewa ndonya ingawa hata mtu mzima angeweza kuwekewa kama alikuwa bado.

“Hiyo mila inatupwa kwani kwa sasa inaendelezwa na watu wachache sana,” anasema.

Aidha Wagogo walikuwa na mila nyingine ya kutoboa masikio kwa kutumia kitu cha chuma ambacho kwa Kigogo kilijulikana kama Mtozo Muhonelo.

Pia anasema utamaduni huo ulitumika kwa kuremba vibuyu au vipeyu. Baada ya kutoboa masikio anasema walikuwa wakivaa Mikubo ambayo huwa mfano wa mfuniko wa soda, vilivyopachikwa kwenye masikio.

Chifu Biringi anasema nguo za Wagogo ni kaniki na pendawagoli ambayo huwa ni nguo ya mistari mistari na kwamba Mgogo akivaa mavazi hayo huonekana ni Mgogo asilia. Kwa upande wa wanawake kulikuwa hakuna kusuka bali wengi wakipendelea kuchana nywele au kunyoa kipara.

Inaaminika kuwa unyoaji ulikuwa unapendelewa zaidi, hasa kwa kuzingatia kwamba Dodoma ni eneo kame.

Akizungumzia mila na desturi ya kuchanja chale kwa wanawake (malembwe) Chifu Biringi anasema ilikuwa ikimuongezea sura ya mvuto mwanamke.

Anasema tofauti na sasa, mwanamke aliyechanja chale alikuwa anaonekana kuwavutia wanaume kuliko asiyechanja. Pia kuvaa shanga shingoni na kiunoni ilikuwa kama urembo kwa wanawake.

“Shanga za kiunoni hutumika kama kumpa hamasa mwanamume na mwanamke asiyevaa shanga alikuwa haonekani kuwa na thamani kwa mwanamume,” anasema.

Anasema mbali na changamoto ya mila na desturi hizo kupotea lakini yeye kama mzee na kiongozi wa kimila wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha watu hawapotezi kabisa mila na desturi za Wagogo.

Ally Biringi ni mjukuu wa Chifu wa Wagogo Salehe Issa Biringi aliyeishi Makulu Dodoma ambapo baada ya kufariki alimwachia mikoba Ngalya Biringi ambaye alifariki mwaka 1972. Baada ya kifo hicho Ukoo ulimchagua Ally kuwa Chifu.

Hii ilikuwa Juni 1972. Kwa mujibu Chifu Biringi, chifu anatakiwa kuwa ni mtu anayependa watu, mshauri na awe anaipenda jamii yote pia asiye na majivuno. “Uchifu huu si wa kuchaguana.

Chifu akifa anapewa cheo hicho mtoto wake mkubwa ila kama ana akili timamu lakini kama mtoto mkubwa hafai anapewa hata mtoto mdogo. Ukimpa mtoto mkorofi uchifu si ataua Ikulu?” anasema.

Miongoni mwa mwa vitu alivyoachiwa ni pamoja na mawe ya tambiko yanayotumika kuita mvua pale mvua zinapochelewa kunyesha.

Kwenye mikoba aliyoachiwa kuna mashuka meusi ya kujifunika, mkia wa ng’ombe (mpuza), vyungu kwa ajili ya kuwekea dawa za asili na fimbo yenye kifundo kilichochongoka (nyolele), vitu ambavyo hutumika kwenye utunzaji wa mawe.

Pia kuna mawe jike na mawe dume lakini mawe jike yanakuwa na duara katikati wakati ya kiume yanakuwa ni makubwa na baada ya kuyaosha kwa kutumia mafuta ya kondoo ndipo shughuli za matambiko hufanyika.

Aidha tambiko la kuomba mvua limekuwa likifanyika kwenye kaburi la babu yao aliyefariki muda mrefu. Chifu Ally Biringi bado anatamani utawala wa kichifu kurudi tena nchini kutokana na jamii kupuuza baadhi ya mila hali inayopelekea kuongezeka kwa vitendo viovu ikiwemo mauaji.

Agustino Ndomu, Mgogo na mzaliwa wa Kijiji cha Sanza Wilaya ya Manyoni mkoani Singida anasema aliwekwa ndonya akiwa bado mchanga na hivyo alipopata fahamu akajikuta tayari ana ndonya.

Anasema alipouliza kwa nini Wagogo wanawaweka ndonya watoto wao wakiwa wadogo aliambiwa kuwa lengo ni kuwafanya wasisikie maumivu na kuwajengea ukakamavu. Ndomu ambaye ni Katekista wa Kanisa Katoliki la Bahi mkoani Dodoma anasema tangu wanakuwa alikuwa akiona watu wakiwekwa ndonya.

Anasema sababu nyingi za kuweka ndonya ilikuwa ni kinga dhidi ya ugonjwa wa macho kwa kuamini mtu akiwekwa ndonya mishipa haitaweza kupokea maradhi mengine.

Pia anasema ilikuwa ni utambulisho wa kabila kuwa ni Mgogo kwani Wagogo walikuwa wakitambuliwa kwa ndonya na lugha yao.

Hata hivyo anasema bado hajaona faida ya kuwekwa kwa alama hiyo na anahisi sababu ya kutoumwa macho si ya kisayansi.

“Mtoto wangu siwezi kumuweka ndonya kwa sababu sioni maana yake, sina mpango huo kabisa,” anasema na kuongeza kwamba hata yeye kama anagelipata fahamu na kukuta hana ndonya asingekubali kuwekewa.

Anasema kama ni kudumisha utamaduni basi anajitahidi kwa kuwafanya wanawe kuongea lugha ya Kigogo sambamba na Kiswahili. “Mtu atajulikana kuwa ni Mgogo kwa kuongea lugha hiyo na si kwa kuweka alama.

“Kama kuna madhara yatapatikana kwa mtoto kutowekewa ndonya si wanangu wangepata madhara kwa vile hawajawekwa ndonya?” Anahoji.

Pia anabainisha kuwa mila na desturi zinapotea kadri malezi yanavyokuwa ni kwamba muhimu kwa wazazi kuangalia jinsi ya kuenzi mila zilizo muhimu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuwafundisha lugha yao kwa faida ya vizazi vijavyo. Anasema bado Wagogo wana tamaduni za kuheshimu wengine na mpaka sasa utamaduni huo umekuwa ukiendelea.

“Wagogo wa zamani walikuwa wakipenda sana kuvaa nguo za asili hasa kaniki kwa wanaume lakini mambo yamebadilika kwani mavazi hayo hayavaliwi tena na hata kama yanavaliwa basi wanaovaa ni wazee,” anasema.

Anasema utamaduni wa Wagogo wa kucheza ngoma za Muheme, Mpana, Msunyunto na Nindo bado unaendelea ili kuenzi mila za kabila hilo.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi