loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndugai ampiga mpinzani wake fimbo kichwani

Mgombea anayedaiwa kupigwa fimbo kichwani na tumboni, Dk Joseph Chilongani alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa alikolazwa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema Dk Chilongani alifika juzi kituo cha Polisi Kongwa akilalamika kuwa wakati wakiwa kwenye mkutano wa kujinadi kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea ubunge wa jimbo hilo, alipigwa fimbo kichwani na tumboni na Ndugai na alipewa Pf3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa hospitali.

Alisema uchunguzi unaendelea kukamilisha kwa kupata maelezo ya watu waliokuwa kwenye eneo la tukio na jalada litatumwa kwa wakili wa Serikali. “Ndugai amehojiwa na anaendelea na shughuli zake kama kawaida,” alisema.

Alisema yaliyotolewa ni malalamiko tu na kinachofuatiwa ni uchunguzi wa tukio. Kamanda Misime alisema alipata fursa ya kumtembelea Chilongani jana hospitali ya Kongwa na akamueleza kuwa hali yake inaendelea vizuri.

“Natokea hospitali Kongwa, yupo hapo na nimeongea naye hana jeraha lolote wala uvimbe,” alisema Awali, akizungumza na gazeti hili jana, mdogo wa mtia nia huyo, Michael Chilongani alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni katika kata ya Ugogoni mjini Kongwa wakati wakiwa kwenye kampeni ya kujinadi kwa wanachama ambao watapiga kura za kuamua nani awe mgombea wao wa ubunge kwa tiketi ya CCM.

Alisema ndugu yake huyo alipigwa fimbo kichwani na tumboni na kusababisha kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa mbili ambapo alikimbizwa kituo cha polisi kwa ajili ya kupatiwa fomu namba tatu na kisha kupelekwa hospitali. Ndugai anadaiwa kufanya vurugu hizo baada ya mgombea aliyetangulia kujinadi kwa wanachama, Simon Katunga kuzungumzia ubadhirifu wa fedha katika halmashauri na kwamba akipata nafasi atapambana na walaji hao.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa kabla ya Dk Chilongani kujeruhiwa kwa fimbo na mgombea mwenzake alitaka kumpiga fimbo hiyo mgombea mwingine aliyejinadi kuwa atakomesha ubadhirifu katika halmashauri ambapo kamati ya ulinzi iliwahi kumzuia.

Shaaban Kihimba ambaye amekuwa akizunguka na wagombea katika kata za Jimbo la Kongwa alisema Ndugai amekuwa akizunguka huku akiwa ameshika fimbo na kwamba baada ya kuona ameshindwa kumpiga Katunga aligeuka upande wa kulia na kumkuta Dk Chilongani akichezea simu hivyo alidai kuwa anamrekodi na kuanza kumshambulia kwa fimbo kichwani na tumboni hadi kupoteza fahamu.

Lakini, jana mchana mdogo wa Dk Chilongani alisema: “Baada ya fahamu kumrudia majira ya saa moja na nusu usiku, kaka alidai anasikia maumivu makali kwenye paji la uso pamoja na kichwani huku akipata shida kuzungumza.”

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa CCM mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba alisema kwa sasa yupo Kondoa Vijijini na kwamba tukio hilo naye amelisikia na hajalishuhudia. Alisema anashangazwa na vitendo vya wagombea vinavyoendelea hivi sasa na kwamba havikubaliki.

Alisema vikao vya kamati ya nidhamu vitakaa na kuchambua malalamiko na kuangalia namna ya kuchuja wagombea. Ndugai ambaye kitaaluma ni ofisa wanyamapori, alilitwaa Jimbo la Kongwa mwaka 2000, hivyo amekuwa bungeni kwa miaka 15 na sasa anaomba kuendelea kwa muhula wa nne.

Juhudi za waandishi wetu kumpata Ndugai kwa njia ya simu zake zote mbili za mkononi kujibu tuhuma dhidi yake hazikuzaa matunda kutokana na simu hizo kuzimwa.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imempandisha kizimbani ...

foto
Mwandishi: Grace Chilongola na Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi