loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

NEC itaamua hatma uandikishaji -Pinda

Amebainisha kuwa kutokana na hali ilivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio itakayotoa ratiba kamili kuhusu hatma ya upigaji kura ya maoni.

Aidha, katika mgogoro na mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea, amewataka wafungue maduka yao kwa kuwa tayari Serikali imeanza kushughulikia na kuyafanyia kazi malalamiko yao.

Akizungumza bungeni jana mjini Ddodoma wakati wa kuhitimisha shughuli za mkutano wa 19 wa Bunge, alisema Serikali inatambua kuwa muda uliobaki kufikia siku ya kupiga kura ni mfupi, lakini Tume ndiyo yenye mamlaka kwa sasa ya kutoa ratiba kamili kuhusu tukio hilo.

“Tunatarajia Tume itatoa taarifa ya Ratiba itakayotumika kutuwezesha kukamilisha zoezi la uandikishaji pamoja na kutoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa Kura ya Maoni. Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisisitiza.

Alisema Serikali kwa upande wake, imehakikisha fedha yote kwa ajili ya ununuzi wa BVR 8,000 zimelipwa kwa NEC na matarajio ni kwamba kazi ya kuandikisha katika mikoa mingine itaanza na kuendelea kwa kasi.

Pia, alisema wakati tume inajitahidi kufikia malengo hayo, Serikali inaendelea na mipango ya kuelimisha wananchi kupitia redio, televisheni, magazeti mbalimbali kuhusu umuhimu wa Katiba inayopendekezwa ili kila mwananchi aielewe vizuri na kuweza kuipigia kura kwa matakwa yake mwenyewe bila kurubuniwa muda utakapofika.

Alisema tume hiyo imelenga kuandikisha wapiga kura milioni 21 na inakadiriwa kutakuwa na vituo 36,164, kila kituo kitaandikisha kwa siku saba hadi 11 kutokana na idadi ya watu na vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili hadi saa 12 jioni.

Akizungumzia suala la mgogoro wa wafanyabiashara Pinda, alisema katika kushughulikia suala hilo, Serikali ilikutana na wafanyabiashara hao na kukubaliana kuwa kwa sababu Serikali imeonesha nia ya kushughulikia malalamiko na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ni mgomo huo ukasitishwa.

“Serikali inathamini sana mchango wa wafanyabiashara katika kukuza Uchumi na kuchangia mapato ya Serikali. Napenda kuwahakikishia wafanyabiashara na wananchi wote kwamba, Serikali ipo tayari kukaa pamoja na wafanyabiashara kuzungumzia changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka,” alisisitiza.

Akizungumzia suala la mauaji ya watu wenye ulemavu (albino), alisema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kiuchunguzi na kiupelelezi na kuwakamata wote wanaohusika na mauaji hayo yaliyojirudia tena nchini na kuwachukulia hatua za kisheria.

Alisema kwa sasa jumla ya watuhumiwa 181, wakiwemo Wanaume 171 na Wanawake 10 walikamatwa na kuhojiwa, kati yao watuhumiwa 133 walifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi.

“Chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Aidha, Matukio 41 kati ya 43 yametokea katika Ukanda wa Ziwa na Magharibi, kwani hadi sasa yametokea matukio 13 ya Mauaji Mwanza, Kagera matukio sita (6), Tabora matukio matano (5), Mara matukio manne (4), Geita matukio manne (4), Kigoma matukio Manne (4) Simiyu matukio matatu (3) na Shinyanga matukio mawili (2)” alisisitiza.

Mahakama ya Kadhi

Kuhusu Mahakama ya Kadhi, alisema katika Mkutano wa 18 wa Bunge Serikali ilikusudia kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na sehemu ya tano ya muswada huo, ilikusudia kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu.

Alisema muswada huo ni miongoni mwa Miswada minne ambayo haikupata nafasi ya kujadiliwa na Bunge.

“Serikali itatumia fursa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua uelewa juu ya maudhui na madhumuni ya Muswada huu”.

Pia, Waziri Mkuu alitoa pole kwa ajali zilizotokea na maafa yaliyotokana na mvua katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Kahama mkoani Shinyanga.

Kizaazaa Kura ya Maoni Mapema jana, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuvunja kikao cha asubuhi cha Bunge majira saa nne, baada ya wabunge wa vyama vya siasa vya upinzani kugoma mijadala mingine isiendelee hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, atakapotoa kauli juu ya mustakabali wa uandikishwaji wapiga kura na hatima ya kura ya maoni.

Wabunge hao, pamoja na kujibiwa na Spika kuwa suala hilo, litatolewa maamuzi wakati Waziri Mkuu akihitimisha hoja ya kuahirisha Bunge, waligoma kukaa na wote wakasimama bungeni, na kuanza kuimba wakiwa wamewasha vipaza sauti huku wakigonga meza wakitaka hoja yao ijibiwe kwanza.

Chanzo cha vurugu kilianza pale, Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo (CCM), alipoomba mwongozo wa Spika, akitaka Bunge hilo lisitishe shughuli zilizopangwa na kujadili suala la kura ya maoni na namna ya kutengeneza Katiba ya mpito kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Katika hoja yake hiyo, Jafo alisema kutokana na hali ilivyo ya uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura, ni wazi kura ya maoni haiwezi kufanyika Aprili 30, kama ilivypangwa.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi