loader
Dstv Habarileo  Mobile
'Nilikeketwa ili nisomeshwe na wazazi '

'Nilikeketwa ili nisomeshwe na wazazi '

Alikuwa akitoa ushuhuda huo kwenye maadhimisho ya kupinga siku 16 za ukatili yaliyoandaliwa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la Kivulini kwa kushirikiana na jeshi la polisi na wanaharakati wengine. Ukeketaji ni hali ya kukikata kabisa moja ya viungo vya msichana kutoka katika sehemu za uke wake.

Anapofanyiwa ukeketaji huaminika kuwa mwanamke kamili aliyeondolewa mkosi na ambaye anastahili kuolewa. Wakati anafanyiwa ukatili huo, Esta alikuwa anasoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Rebu, ambapo mara baada ya kukeketwa, anasema alipata maumivu makali ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi.

Anasema alikubali kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba na alikuwa na hamu ya kuendelea na masomo, lakini akapewa masharti na wazazi wake kuwa ili aendelee na masomo lazima akeketwe.

“Sikuwa na jinsi, nilijua ningeenda kukumbana na maumivu makali na kwa sababu nilikuwa napenda shule ilinibidi nikubali kukeketwa,” anaeleza. Ukeketaji unafanyikaje?

Anasema aliamshwa saa 11.30 alfajiri akiongozana na mama yake na wanawake wengine watatu, ambapo alikwenda kuungana na wasichana wenzake waliokuwa kwenye orodha ya kufanyiwa ukeketaji, na kupelekwa mtoni kuogeshwa!

“Tuliogeshwa na kupewa maneno ya ujasiri ili tusilie wakati wa kukeketwa,” anasema na kuongeza kuwa Ngariba alilipwa kiasi cha Sh 10,000 kwa kila msichana aliyekeketwa (kwa wakati huo). Esta anasema kuna eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo na msichana hushikwa mikono yake kwa nyuma na mama aliyekeketwa.

“Baada ya kufika eneo lile, tulitangaziwa na ngariba kuwa kila mmoja awe na wembe wake, ambao ndiyo aliutumia kukeketa, ” anasema.

Anachokumbuka siku hiyo ni kujikuta tayari amekwishakeketwa huku akitokwa na damu nyingi na maumivu makali. Anasema baada ya kukeketwa, wasichana wote waliwekwa katika uangalizi wa akina mama wasaidizi wakiwemo baadhi ya ngariba, huku wakiwapatia dawa za kienyeji wale wanaovuja damu ili isiendelee kuvuja.

“Nilishindwa kula, nilikunywa uji tu, siku ya pili nilipata maumivu makali baada ya kuamshwa asubuhi kwenda kuogeshwa,” anaeleza.

Anasema msichana anapotoka jandoni, inambidi ashiriki tendo la ndoa na mwanaume ambaye amefanyiwa tohara kama ishara ya kukubali kuwa binti aliyekeketwa kuwa mwanamke kamili na anayestahili kuolewa. Msichana aliyekeketwa huitwa 'omonke'.

Anaiomba serikali, asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike, na kwa ngariba wapewe elimu ya kutosha dhidi ya madhara ya ukeketaji.

“Wengi huku Tarime wanafanya hivyo, wakijivunia kutekeleza mila, lakini pia ngariba bado hawajapata elimu ya madhara ya ukeketaji, naiomba serikali na wadau wengine watoe elimu zaidi juu ya madhara ya ukeketaji,” anasema na kuongeza kuwa wanaamini wakimkeketa mtoto wa kike huleta baraka katika familia. Ni madhara gani aliyokumbana nayo?

Anasema baada ya kuketwa aliumia sana na aliathirika kisaikolojia, ikiwemo kuzomewa na wasichana wa rika yake ambao hawakuwa tayari kukeketwa.

“Siku niliyokeketwa, nilipata shida sana, nilikuwa na hofu hata wenzangu walikuwa wananicheka, hata nilipopona nilichukua muda kurudi shule, niliathirika sana,” anasema. Madhara mengine aliyoyapata ni pamoja na kuchanika sehemu zake za siri, kutokana na kuketwa na ana wasiwasi kama atajifungua salama siku za baadaye.

“Mimi nahisi hata wakati wa kujifungua, nitapata matatizo, naomba wazazi wetu wabadilike waanze kwenda na wakati na watambue kuwa wanapotufanyia ukeketaji wanatufanyia ukatili wa kijinsia na kilema cha maisha,” anasema.

Anasema kuna uwezekano wa wasichana wanaokeketwa kupata virusi vya Ukimwi, kutokana na kukeketwa na ngariba mmoja, ambaye hukeketa zaidi ya wasichana 50 kwa siku.

“Kwa vile huwa peke yake, na anakeketa wasichana kwa mara moja, ni rahisi kueneza ukimwi,” anasema. Atoa onyo kwa wazazi na polisi Esta ambaye anasema atawazuia wadogo zake wa kike Neema na Happy wasikeketwe. Anawataka wazazi kuacha ukeketaji kwa madai ya kutokuwa na faida kibaolojia kwa watoto wa kike.

“Wazazi wetu waachane na mila potofu, mila hizi hazitujengi bali zinatubomoa na kutufarakanisha na jamii ya watu wengine,” anasema. Anasema matarajio yake ya baadaye ni kusomea uandishi wa habari ili aweze kufanya kazi na jamii kwa kuielimisha ili iache matukio hayo ya ukatili wa kijinsia.

“Nitasomea utangazaji, nitafanya kazi kwa bidii na natamani niwe kama Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba. Nampenda jinsi anavyowahudumia wanawake,” anasema.

Analitaka jeshi la polisi liwasaidie wasichana wanaokeketwa kwa kuwakamata ngariba na kuwafikisha mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake kwa vile wanaokeketwa huachiwa kilema cha maisha.

Anaitaka jamii ya Wakurya kuwaendeleza watoto wa kike kitaaluma zaidi badala ya kuwaoza wakiwa katika umri mdogo, na hivyo kushindwa kuhimili kutunza familia.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime- Rorya, Emmanuel Mkoma anasema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau wengine wilayani Tarime, limeanza kutoa mafunzo ya tohara mbadala yatakayoiwezesha jamii kutambua athari za ukeketaji kwa mtoto wa kike.

“Lengo la mafunzo hayo yatakuwa ni kutoa elimu kwa jamii, ambapo watoto wa kike watapewa elimu ya malezi ya afya zao itakayowasaidia wasikeketwe, msisitizo wake ni kuielimisha jamii ione madhara ya ukeketaji na kadri siku zitakavyokwenda naamini jamii itaachana na ukeketaji,” anasema Ofisa Uhamasishaji na Utetezi kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Kivulini lililo jijini Mwanza, Khadija Liganga anasema kumkeketa mtoto wa kike ni kumfanyia ukatili wa kimwili, ambao kwa baadaye utamletea madhara wakati wa kujifungua.

Anaitaka jamii ya Wakurya wilayani Tarime kuachana na ukatili huo kwa mtoto wa kike, ambaye kwa mujibu wake anapokeketwa huozwa katika umri mdogo na kupoteza ndoto zake za maisha.

“Naomba mtoto wa kike aendelezwe kielimu ili hatimaye aweze kutimiza ndoto zake na asifanyiwe ukatili wa kukeketwa kwani una madhara makubwa kiafya, wakati wa kujifungua,” anahitimisha Liganga.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi