loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Nina mimba ya kiongozi Boko Haram’

Aprili 14 mwaka huu, zaidi ya wasichana 270 walitekwa usiku katika shule ya serikali kwenye eneo la Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria, na hadi sasa zaidi ya 200 hawajapatikana na haifahamiki walipo. Sikumshangaa mke wa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, Patience alipobubujikwa machozi wakati anazungumzia kutekwa kwa mabinti hao waliokuwa wakijiandaa kufanya mitihani.

Mke wa Rais Jonathan amewataka Boko Haram wawaachie wasichana hao kwa maelezo kwamba, kitendo chao ni cha kishetani na damu ipo mikononi mwao.

“Sisi wanawake ni mawakala wa amani, watoto ni wetu, na hatuwezi kukunja mikono wakati watoto wetu wamepotea,” anasema mama huyo. Wakati anazungumza na viongozi wa shule walipotekwa mabinti hao, Patience amesema, kwa damu inayomwagika Nigeria Mungu yupo. Kadhalika ametaka wadau washirikiane kuhakikisha wasichana waliotekwa wanarudi salama makwao.

Mabinti waliotekwa si wanawe na pengine si ndugu zake, lakini Patience ni mama, anafahamu uchungu wa kumpoteza mtoto katika mazingira kama ilivyotokea kwa wanafunzi hao waliolazimishwa kuwa Waislamu. Alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Bloomberg, Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, amesema, awali Rais Jonathan hakuamini kama ni kweli wasichana hao wametekwa.

“Kuhusu utekaji, kwa takribani siku 18 Rais hakuamini kwamba, wale wasichana walikuwa wametekwa. Kama Rais alipata taarifa ndani ya saa 12 na angewahi kulishughulikia, ninaamini wale wasichana wangekuwa wameokolewa ndani ya saa 24, si zaidi ya saa 48. Usisahau, wapo takribani wasichana 300,” anasema kiongozi huyo aliyestaafu mwaka 2007.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mstaafu, kulikuwa na uwezekano wa kuwaokoa wasichana kwa sababu ya wingi wao, kwa kuwa mchakato wa kuwahamisha kutoka walipotekwa ungeweza kuchelewa lakini hilo halikuwezekana kwa sababu Rais Jonathan hakuziamini taarifa kuwa wametekwa.

“Kwa bahati mbaya Rais hakuwa na uhakika ‘hivi ni kweli? Hizi ni njama za baadhi ya watu ambao hawataki niendelee kuwa Rais? Nani anafanya hivi?’ nadhani ilikuwa ni bahati mbaya kwa jambo lote hili,” anasema Obasanjo na kubainisha kwamba, baadhi ya mabinti waliotekwa huenda hawatarudi makwao kwa kuwa imechukua muda mrefu kwa Serikali ya Nigeria kushughulikia jambo hilo.

“Ninaamini baadhi yao kamwe hawatarudi, tutaendelea kusikia kuhusu wao kwa miaka mingi ijayo…kama ukiweza kuwarudisha wote itakuwa karibu na miujiza…unafikiri watakuwa wamewaweka pamoja hadi sasa?...kufanya vile, kuwachukua wasicha 200 kwa pamoja si jambo dogo,” anasema Obasanjo.

Uongozi wa jeshi la Nigeria umekaririwa ukisema kuwa umebaini walipo zaidi ya wasichana 200 waliotekwa shuleni lakini hawawezi kutumia nguvu kuwaokoa.

“Habari njema kwa wazazi wa wasichana ni kwamba, tunafahamu walipo lakini hatuwezi kuwaambia ni wapi. Je, tunaweza kwenda kwa nguvu walipo? Hatuwezi kuua wasichana wetu kwa kigezo cha kujaribu kwenda kuwarudisha,” anasema Alex Badeh, Mkuu wa Majeshi wa Nigeria.

Siku chache baada ya Rais mstaafu Obasanjo kuyasema hayo, amejitokeza msichana na kudai kuwa, Boko Haram walimteka kwa miezi 27 na sasa ana ujauzito anaodai ni wa kiongozi wa kundi hilo, Abubakar Shekau.

Msichana huyo aliyetajwa kwa jina la Meenah Dawah (jina lake halisi limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama) anasema alitekwa alipokuwa na umri wa miaka 17, na wakati alipokuwa kambini mafichoni, alifanya ngono na Shekau wakati alipotakiwa kuwaburudisha wapiganaji wa Boko Haram.

Msichana huyo anasema, kabla ya kutekwa, Boko Haram walimlazimisha ashuhudie wazazi wake wanavyouawa kwa risasi nyumbani kwao kijijini kwenye eneo la Konduga, kaskazini mwa Nigeria. Anasema, alipokuwa mateka, alikuwa anawatunza watoto wa makamanda na wapiganaji wengine wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa msichana huyo, wanawake waliotekwa wanabakwa, na kwamba alikuwa anatetemeka aliposikia wakipiga kelele wakati wanafanyiwa unyama huo. Kuna wakati anasema alishuhudia wakiteswa walipogoma kubadili imani zao. Anasema, mara kadhaa, baadhi ya viongozi wakuu wa kundi hilo walimwendea na wakamtaka awaburudishe.

Anadai kuwa, alifanya ngono na Shekau alipotakiwa kumburudisha. “Abu ana watoto wengi kutoka kwa wanawake tofauti,” anasema msichana huyo akimaanisha Shekau.

“Mjomba hawezi kunipokea vizuri kwa sababu anaona aibu kwa kuwa, baba wa mwanangu si tu bado ni utata lakini ni hatari kama ni wa Shekau,” anasema na kuongeza kuwa, mjomba wake ni ndugu yake pekee aliyebaki, wangine wameuawa. “Alikuwa anakuja kutoka kusipojulikana kama mzimu. Alionekana kuhamaki kila wakati na kutoa maelekezo. Ni mwanaume anayezungumza taratibu, ni kama ananong’ona.

Endapo unakutana naye kwa mara ya kwanza huwezi kumuogopa,” anasema msichana huyo na kuongeza kuwa, muda mfupi baada ya kuishi mafichoni alibaini kuwa, kila baada ya Shekau kunong’ona na wenzake, jambo fulani la hatari lilitokea mahali fulani nchini Nigeria.

“Aliwahi kuniuliza kama nilikuwa tayari kupigana kwa ajili ya kitu fulani, nikamjibu hapana. Aliniambia ningeweza kuwa mpiganaji na mtumwa. Sikutaka kuongea naye jambo ambalo lingemkwaza, hata neno moja ambalo kwake si sawa angeweza kuniua,” anasema. “Nilidhani alikuwa anakunywa pombe au kutumia kitu fulani kabla ya kuja.

Mtu angeweza kugundua kuwa labda alipoteza askari wake au kitu fulani hakikuwa sawa,” anasema msichana huyo na kubainisha kuwa majukumu yake yalibadilika kulingana na kambi alipokuwa na ilikuwa ni tabu kwake kuhama akiwa amembeba mtoto mgongoni. Anasema, kuna baadhi ya kambi za Boko Haram zilizopo mafichoni zenye huduma za maji, umeme na vifaa vya elektroniki zikiwemo televisheni.

Kwa mujibu wa msichana huyo, baadhi ya wanawake walikuwa wanakwenda Maiduguri kununua mahitaji wakifuatana na kamanda au makaman- da wawili na walitumika pia kwenye uvamizi na mauaji. “Nilitumwa kuzungumza na watu, walikuja nyuma yangu na kuanza kuua,” anasema.

“Baadhi yetu sisi wasichana tulibeba bunduki na mara kadhaa mabomu. Kulikuwa na msichana alilazimishwa kubeba mabegani kifaa cha kutupa bomu la kutupwa na roketi na tulikuwa na wanaume wachache kwenye ile kambi,” anasema. Kwa mujibu wa msichana huyo, alifanikiwa kujiokoa wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia kambi ya Boko Haram alipokuwepo, akajeruhiwa kwa risasi, akaachwa afe.

Imefahamika kwamba, hivi karibuni madaktari katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Ualimu Maiduguri kilichopo jimbo la Borno walifanikiwa kuondoa risasi kwenye mguu wa msichana huyo.

Kwa mujibu wa msichana huyo, kabla wazazi wake hawajauawa kwa risasi kijijini kwao, baba yake mzazi alikuwa na mpango wa kumpeleka akamalize elimu ya sekondari ya wasichana kwenye shule ya serikali iitwayo Shaffa kwa kuwa wana ndugu huko lakini aliuawa aliposhambuliwa wakati anatoka sokoni.

“Nafahamu nina uwezo mkubwa darasani na nipo tayari kusoma lakini nitaanzia wapi?” anasema. Msichana huyo ni miongoni wa waathirika wengi kutokana na ukatili wa Boko Haram unaofanywa Nigeria kwa mgongo wa dini. Tangu walipotekwa wasichana shuleni, wananchi wakiwemo wanaharakati wamekuwa wakiandamana kuishinikiza Serikali ya nchi hiyo iwatafute na kuwarudisha wakiwa salama.

Rais Jonathan hataki serikali yake ishutumiwe kwa kilichotokea kwa wasichana hao. Anasema, waandamanaji wawalaumu magaidi wa Boko Haram na siyo serikali. Awali kulikuwa na taarifa zilizodai kuwa, wanafunzi waliotekwa wamefichwa kwenye msitu wenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 60,000 lakini sasa inadaiwa kuwa, wametawanywa kwenye maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na nje ya Nigeria.

Rais Jonathan anasema, tukio la kutekwa kwa wanafunzi wa Chibok limemgusa sana, na kwamba, si sahihi kumtuhumu kuwa hajafanya juhudi za kutosha kuwaokoa.

“Ilikuwa lazima nikae kimya kuhusu juhudi za jeshi, polisi na wachunguzi kuwatafuta wasichana waliotekwa na kundi la magaidi la Boko Haram Aprili kutoka mji wa Chibok… Ukimya wangu tunavyoendelea na kazi ya kuwatafuta umetafsiriwa vibaya na wakosoaji wanaosema hatuwajibiki na ni udhahifu,” anasema Rais Jonathan.

Kwa mujibu wa Rais Jonathan, amekuwa kimya kuhusu jambo hilo ili kutoathiri uchunguzi. “Serikali yangu, walinzi wetu na watu wa usalama wametumia kila rasilimali, hawajaacha na hawataacha mpaka wasichana warudi nyumbani na waliowateka wafikishwe kwenye mkondo wa sheria.

Kwa amri zangu, majeshi yetu yamefanya juhudi kubwa kuwasaka hawa wauaji misituni Kaskazini ya Jimbo la Borno kwenye makao yao,” anasema. “Moyo wangu unauma kwa sababu ya hawa watoto waliopotea na familia zao. Mimi ni mzazi, na ninafahamu ni kiasi gani inaumiza, hakuna kitu cha muhimu zaidi kwangu kuliko kuwatafuta na kuwaokoa mabinti wetu,” anasema kiongozi huyo wa Nigeria.

“Tangu mwaka 2010, maelfu ya watu wameuawa, wamejeruhiwa, wametekwa au kuhama kwa lazima kwa ajili ya Boko Haram wanaotaka kuishinikiza nchini na kuweka aidelojia yao kwa Wanigeria wote. Serikali yangu imedhamiria kufanya hilo lisiwezekane. Hatutasalimu amri kwa wanavyotaka magaidi hawa,” anasema. Imeandikwa kutoka vyanzo mbalimbali.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi