loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

NIVA: Aeleza alivyoanza na mtaji wa Sh 200,000

Kampuni hiyo kwa mara ya kwanza mwaka jana ilitoa tuzo kwa wasanii wanaofanya nao kazi. Baadhi ya waigizaji waliamini kwamba kuchaguliwa kwake, katika tuzo hiyo iliyofanywa na Steps ni kama hujuma ya baadhi ya watu kutaka kuwapandisha wasanii fulani na kuwashusha baadhi ya wasanii kisanaa, jambo ambalo Niva analipinga.

Akizungumza na gazeti hili msanii huyo, ambaye nyota yake inazidi kung’ara kila kukicha, anaeleza siri ya mafanikio ya kazi zake. Anasema hawezi kuongelea zaidi suala la rushwa kutendeka katika kumfanya kuwa mwigizaji aliyeuza sana mwaka jana, kwa kuwa anaamini juhudi zake ndizo zinazomfanya kuwa alipo.

“Nilianza kazi kwenye mazingira magumu sana, watu wanaposema nimependelewa, ” anasema. Anasema kwa mara ya kwanza alianza sanaa kwa mtaji wa shilingi laki mbili, aliyopewa na mama yake kama sehemu ya mtaji wa kuanzia maisha. Fedha hizo anasema alifikiria jinsi ya kuandaa kazi yake ya kwanza, jambo ambalo lilimuwia vigumu kutokana na kiasi kidogo cha fedha alichonacho.

Anasema alijaribu kutafuta msaada ili kufanikisha kukamilika kwa kazi yake, lakini ilikuwa ngumu, ndipo akaamua kuanza kazi kwa kiasi hicho cha fedha. Filamu ambayo aliamua kuanza nayo ni Mtoto wa Kitaa, ambayo alihisi ingeweza kukabiliana na bajeti ndogo aliyokuwa nayo.

Anasema, aliitumia laki moja kwa kumlipa msanii wa kike Ndombagwe Mesayo, ‘Thea’ aliyecheza filamu hiyo, msanii mwingine ni Flora Mvungi hakumlipa sababu alishawahi kucheza filamu yake bure. “Flora hakutaka nimlipe hivyo akawa amenisaidia katika bajeti yangu ya kufanya kazi yangu,” anafafanua Niva.

Baada ya kukubaliana na wasanii, Niva anasema, mpigapicha Hassani Mbagoni, ambaye ni rafiki yake aliamua kujitolea kufanya naye kazi hiyo bila malipo. Lakini hata hivyo anasema filamu hiyo haikuweza kukamilika kutokana na kuhitajika fedha nyingi za kuiendeleza, hali iliyopelekea kuishia katikati.

“Nilikuja kukwama sababu sikuwa na fedha zozote za kuweza kulipia baadhi ya huduma, na hapo ndipo nikaamua kuomba msaada kwa ajili ya kuikamilisha,” anaeleza Niva. Anasema, alikuja kukamilisha filamu hiyo baada ya kuomba msaada wa watu wengine, hadi ilipoingia sokoni kiasi cha kufanya vizuri na watu wakaanza kumjua katika tasnia hiyo.

Fedha alizozipata kupitia filamu hiyo, anasema zilimwezesha kumudu kutengeneza filamu nyingine kwa gharama ya Sh milioni sita. Filamu hiyo aliita Tabu ya Kuoleana.“Nilijitahidi kufanya kazi nzuri, ambayo ingeweza kuniweka sehemu nzuri katika tasnia ya filamu, jambo ambalo ndio lilikuwa lengo langu,” anasema.

Baada ya kufanya vizuri kwa filamu ya Tabu ya Kuoleana, ndipo akatoa filamu ya Mkali Mo, ambayo alitumia Sh milioni tano, akiwa amemshirikisha mfalme wa filamu za vichekesho Amri Athumani ‘King Majuto’. Anasema, filamu hiyo ambayo ilisambazwa na kampuni ya Tuesday Kihangala Distribution, ilimweka sehemu nzuri kiasi cha kampuni nyingine kumhitaji.

“Nilianza kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya watu kutaka nifanye nao kazi, jambo ambalo kwangu lilikuwa kama neema,” anasema Niva. Baada ya kukamilika kwa filamu hiyo, ndipo alipoungana na mchumba wake Najma Mohamed, kutengeneza filamu Gubu la Mume.

Filamu hiyo ilifanya vizuri kiasi cha kutangazwa kama filamu iliyofanya vizuri kwa mwaka 2013, na kutikisa wasanii wakongwe. Anasema baada ya hapo ndipo alipoingia mkataba wa kufanya kazi na kampuni ya usambazaji wa filamu Tanzania, Steps Entertainment. “Baada ya kufanya vizuri kwa kazi yangu hiyo, ilianza kunipa matumaini kwamba mashabiki wananikubali na ndipo nikafanya kazi nyingine,” anasema.

Kazi nyingine aliyoamua kuifanya kwa kipindi hicho ni Tabu Kiboko ambayo imeendelea kuwepo hadi sasa wakati anajiandaa kutoa kazi yake nyingine ya Najuta Mie. Anasema, tangu alipoanza sanaa hadi sasa alipofikia, sanaa imemuwezesha kufanya mambo mengi, kiasi cha kutotegemea kazi nyingine zaidi ya filamu.

Hivi sasa anasema anaendesha maisha yake, kwa kumudu kulipa pango la nyumba anayoishi na kulea familia yake. Anasema, sanaa imemuwezesha kununua usafiri, ambao kwa kiasi chake unamsaidia katika maisha yake na safari zake za hapa na pale. Pia anasema sanaa imemwezesha kuheshimika na hata kujulikana zaidi na watu ambao mara ya kwanza hakutegemea kuonana nao.

“Nasema sanaa imenisaidia sana, kwa kuwa sikutegemea kuishi maisha ambayo naishi sasa,” anasema. Anasema, lengo kwa sasa ni kufanya kazi nyingi zaidi na kuliteka soko la filamu, hivyo anasema anazidi kufanya juhudi kutimiza lengo lake. Huyu ndio Niva, mzaliwa wa Tandale, Dar es Salaam. Anasema, alianza sanaa mwaka 2000 akiwa na kundi la Safina.

Mwaka 2004 aliachana na kundi hilo na kuanzisha kundi lake la Kiburugwa, lakini hakuweza kudumu nalo, ndipo akajiunga na kundi la Datemba. Lakini mwaka 2005 alihama kundi hilo na kujiunga na kundi maarufu la Shirikisho Afrika Sanaa Group, lakini alikuja kushindwa katika mchujo wa kuendelea kubaki katika kundi hilo.

Ndipo mwaka 2006 alipojiunga na kundi la Tuesday Kihangala Production, linaloongozwa na Tuesday Kihangala 'Mr. Chuz'. Anasema hapo ndipo alipoibuka na umaarufu mkubwa, katika igizo la Jumba la Dhahabu, ambapo liliwatoa wasanii wengine kama Mzee Chilo na Rado. Kwa sasa Niva ni msanii anayejitegemea akifanya kazi zake mwenyewe.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin ...

foto
Mwandishi: Mohamed Musa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi