loader
Dstv Habarileo  Mobile
NSSF yajitosa kupambana na zana duni wachimbaji wadogo

NSSF yajitosa kupambana na zana duni wachimbaji wadogo

Kufikiwa kwao huko kunaashiria kufikia ukomo wa adha ya muda mrefu ya kutumia zana duni na kukosa uhakika wa matibabu wanapoumia kazini pamoja na mafao ya uzeeni. Hali hiyo inatokana na kuanzishwa kwa Mpango wa Hifadhi ya Jamii kwa wachimbaji wadogo ambao pamoja na mambo mengine, unalenga kuwawezesha kupata mikopo ya vitendea kazi.

Chini ya mpango unaoitwa ‘Madini Scheme’ ulioanzishwa na NSSF, wachimbaji wadogo watapata fursa ya kupata mikopo ya vitendea kazi, hivyo kuboresha utendaji wao tofauti na sasa, ambapo wengi wanatumia zana duni kama sululu na majembe.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori, anasema wachimbaji wadogo kwa miaka wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira hatarishi na kutumia zana duni, hivyo kusababisha washindwe kupata tija na kuchangia kikamilifu katika pato la taifa.

Anasema mpango wa Madini Scheme unalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo ya riba nafuu ya kununulia vitendea kazi kwa ajili ya kuboresha kazi zao.

“Wachimbaji wadogo hawajafikiwa na mpango wa hifadhi ya jamii, hivyo NSSF tumeona ni vyema sasa tuweke utaratibu wa kulifikia kundi hili muhimu katika uzalishaji ili wanufaike na mafao tunayotoa katika hifadhi ya jamii na kupata mikopo ya riba nafuu ya vitendea kazi,” anasema Magori.

Anaongeza, “Tanzania ina watu milioni 44, milioni 23 kati yao ndiyo nguvu kazi ya taifa ambapo kati ya hao wachimbaji wadogo ni milioni nne. Hili ni kundi kubwa katika uzalishaji ambalo halipaswi kuachwa bila utaratibu maalum wa hifadhi ya jamii”.

Magori anabainisha kuwa, mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Shirikisho la Wachimbaji Wadogo (FEMATA), Wizara ya Nishati na Madini na NSSF ambapo tangu kuzinduliwa mwezi Mei mwaka huu jumla ya wachimbaji wadogo 7,000 wameandikishwa katika mpango wa Madini Scheme.

Anasema kuna sababu nyingi za kuanzisha mpango huo ikiwemo kuwakinga wachimbaji wadogo dhidi ya majanga kwa kuwapa mafao yote yanayotolewa na shirika hilo kama pensheni ya uzee, ulemavu, urithi na mafao ya muda mfupi kama uzazi, kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi, msaada wa mazishi na mafao ya matibabu.

“Kwa asili ya kazi zao wachimbaji wadogo wapo katika hatari ya kuumia au kupata magonjwa yatokanayo na kazi, hivyo sisi tuna mafao ya kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi. Mchimbaji mdogo akijiunga na mpango huu anakuwa na uhakika wa matibabu,” anasema Magori.

Anafafanua kuwa utekelezaji wa mpango huo kwa sasa umejikita katika mikoa yenye wachimbaji wadogo kama Simiyu, Geita, Mwanza na baadaye utaenea nchini nzima. Ofisa mwingine wa NSSF, Salim Khalfani, anasema Madini Scheme ni utaratibu ambao unalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kufaidika na hifadhi ya jamii.

“Tayari tumeandikisha wachimbaji 7,000. Lengo letu katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili ijayo kufikia wachimbaji wadogo milioni mbili,” anasema. Anasema mpango huo pia unalenga kusaidiana na serikali kupunguza umasikini kwa jamii, kujenga kizazi kisicho tegemezi kwa kutoa pensheni ya uzee, urithi na ulemavu.

Kwa mujibu wa Khalfani, hatua hiyo itanusuru kipato ambacho wangetumia katika matibabu badala yake watumie kipato hicho kujiendeleza kiuchumi.

“Kazi ya uchimbaji madini inategemea nguvu alizonazo mhusika, na hatuwezi kuwa na nguvu wakati wote hasa anapokuwa mzee uwezo wake wa kufanya kazi ngumu kama hii hupungua, lakini mchimbaji mdogo akijiunga na mpango wa Madini Scheme ataweza kupata mafao ya pensheni atakapokuwa mzee na kushindwa kufanyakazi hiyo,” anasema Khalfani.

Anasema mpango huo pia unawaunganisha wachimbaji wadogo watambue kwamba wapo kwenye ajira yenye tija kwao na kwamba wana wajibu wa kuithamini, kuiendeleza ili ilete tija kwa mchimbaji mmoja mmoja na taifa kwa jumla. Kuhusu nani anaweza kujiunga na mpango huu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Magori anasema wachimbaji wadogo waliojiunga katika vyama vya wachimbaji wa mikoa au vyama vingine vya ushirika wenye leseni na wasio na leseni wamekaribishwa.

“Wengine wanaoweza kujiunga na mpango huo ni mchimbaji mmoja mmoja alimradi awe na uhakika wa kuchangia shilingi 50,000 kila mwezi, kiasi ambacho ndicho kilichopo katika makubaliano kati ya NSSF na shirikisho la wachimbaji wadogo,” anasema Magori. Anaongeza, “Wote wanaojishughulisha na biashara zote za madini ikiwemo wanunuzi wa madini, usafirishaji, uongezaji thamani, uuzaji na yale yote yanayotokana na madini ambao hawapo katika mfumo rasmi wanahusika na mpango wa Madini Scheme”.

Mbali na hayo Magori anaeleza kuwa, wengine wanaoguswa na mpango huo ni pamoja na wale wote wanaojihusisha na utoaji wa huduma katika maeneo ya wachimbaji ambao wamejiajiri wenyewe.

Akizungumzia mpango wa Madini Scheme, Kassimu Milambo ambaye ni mchimbaji mdogo wa dhahabu katika machimbo ya Kibangile katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro anasema utasaidia kuwakomboa wachimbaji wadogo kwa kuwezesha kupata mikopo ya kununua zana bora na kupata mafao ya hifadhi ya jamii ikiwemo matibabu.

“Nimekuwa nikichimba dhahabu kwa miaka 20 sasa, sikuwahi kusikia hata siku moja kuwepo utaratibu wa kuwaingiza wachimbaji wadogo katika mfumo wa hifadhi ya jamii kama huu wa Madini Scheme, kwa kweli utatusaidia sana hasa tunapopata maradhi,” anasema.

Anasema wachimbaji wadogo wengi wapo katika janga la kuambukizwa magonjwa ya kifua kutokana na aina ya zana duni wanazofanyia kazi.

“Katika utaratibu wa Madini Scheme, wachimbaji wadogo watapata faida kama tatu hivi, moja kupata mikopo ya kununulia vitendea kazi na hivyo kuboresha utendaji kazi wao na watapata mafao ya matibabu na pensheni ya uzeeni. Haya ni mambo muhimu kwa ajili ya kujenga uchumi wa taifa,” anasema Milambo.

Ili kuboresha shughuli za uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi huyo wa Uendeshaji anatoa mwito kwa wachimbaji wadogo na watoa huduma kujiunga na mpango wa ‘Madini Scheme’ ili wapate fursa ya kupata mikopo ya kununua zana za uchimbaji, kupata mafao ya matibabu na pensheni ya uzeeni.

Kwa upande wake, Salim Khalfan anatoa rai kwa wachimbaji wadogo kuchangamkia fursa hiyo inayowahakikishia maisha bora ya sasa na ya baadae ili kupanua wigo wa mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa.

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi