loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nyati: Wanyama wanaozaana wakati wa neema tu

Kuna nyati wa aina mbili. Nyati wa Afrika ambao ni wakali na wanaishi kwenye mbuga za wanyama. Nyati wa Asia ni wapole na wanaoishi katika makazi ya watu na hutumiwa kwa kazi mbalimbali kama ng’ombe. Wataalamu wa masuala ya wanyama wanasema nyati wa Afrika ambaye kisayansi anajulikana kama Syncerus caffer hawana uhusiano na nyati maji wanaopatikana katika bara la Asia.

Nyati ana urefu wa mita 1.7 kwenda juu na urefu wa mwili wake kutoka mkiani hadi kichwani ni mita 3.4. Uzito wa nyati unatofautiana kutokana na eneo wanaloishi ambapo nyati wa savana wana uzito wa kilo 500-900. Nyati dume huwa na uzito kati ya kilogramu 600 hadi 900 na kwa kawaida huwa mkubwa kuliko nyati jike ambaye uzito wake ni kati ya kilo 500 hadi 700.

Pia nyati wa savana huwa wa rangi nyeusi au kahawia nyeusi na pembe zao zimejikunja. Nyati wa msitu ni wadogo na kimo chao ni nusu ya kiwango cha nyati wa Savana. Nyati wa Msituni wana rangi ya kahawia nyekundu na pembe zao zimejikunja sehemu ya juu kuelekea nyuma.

Hata hivyo ndama wote wa Nyati wa msitu na wale wa Savana wanazaliwa wakiwa na ngozi nyekundu kisha kubadilika kadiri wanavyokua. Nyati wa Afrika ni wagumu kufuga kwa kuwa wana tabia hatarishi na isiyotabirika. Nyati ni miongoni mwa wanyama wanaohatarisha maisha ya binadamu. Nyati wa Afrika ni miongoni mwa wanyama maarufu katika kundi la wanyama wanaokula nyasi.

Anaishi katika eneo yenye maji mengi, maeneo yanayokumbwa na mafuriko, mbuga zenye nyasi ndefu pia katika misitu ya milima mikubwa ya Afrika.

Nyati anaweza kupatikana katika misitu ya milima na sehemu za miinuko, na wanapendelea kuweka makazi yao katika maeneo yenye mianzi mingi na vichaka hivyo ukibahatika kupita maeneo yenye pori unapaswa kuwa muangalifu dhidi ya nyati kwa kuwa hana huruma dhidi ya binadamu.

Kundi kubwa la nyati pia linapatikana katika mbuga na mapori yenye miti. Ingawa wanakunywa maji kila siku huweza kukaa mbali na vyanzo vya maji kisha kwenda kutafuta maji baada ya kula nyasi. Wataalamu wa masuala ya wanyama wanasema nyati anashikilia nafasi ya kwanza kwa kula kwa haraka kuliko wanyama wengine wote wanaokula nyasi barani Afrika.

Wakati wa kula hutumia ulimi na meno mapana kukata nyasi ndefu kwa haraka kisha kutafuna haraka hivyo huweza kula nyasi nyingi kwa muda mfupi. Kitendo cha nyati kula nyasi ndefu kinadhihirisha maajabu ya Mungu katika ugawaji wa chakula kwa kuwa wakati wa kula nyati hupunguza urefu cha nyasi katika kiwango kinachopendelewa na wanyama wengine ambao kwa asili wanakula nyasi fupi.

Hivyo katika mbuga yenye wanyama wengi, kila mnyama ana chakula chake, wengine wanauwezo wa kula nyasi ndefu tu, wengine nyasi fupi tu, wengine majani laini na wengine majani magumu yaliyochanganyika na mizizi au kamba kamba. Nyati hawapendelei kukaa maeneo ya wazi kwa muda mrefu, wakishakula wanajificha katika maeneo tulivu yenye ubaridi na mandhari ya kuvutia.

Nyati wana msimu maalumu wa kujamiiana ili watoto wazaliwe wakati wa mvua kipindi ambacho kina chakula kingi na majani malaini kwa ajili ya ndama. Nyati jike akipata joto huvutia madume mengi ila mafahali yenye nguvu ndio hupata nafasi kubwa zaidi ya kupanda jike.

Dume anayetaka kupanda jike huwa karibu na jike husika na hutumia pembe zake kuwapiga na kuwafukuza madume mengine kando. Nyati jike hupevuka na kuwa na uwezo wa kubeba mimba wakiwa na umri wa miaka mitano. Hubeba mimba kwa miezi kumi na moja na nusu.

Ili kuwalinda dhidi ya maadui ndama waliozaliwa hufichwa katika vichaka kwa wiki chache za kwanza wakitunzwa na mama zao kabla ya kujiunga na kundi kuu. Kwa ajili ya usalama ndama huwa katikati ya kundi kubwa la nyati. Uhusiano wa mama na ndama hudumu muda mrefu zaidi kuliko wanyama wengi wanaokula majani.

Hata hivyo wakati ndama mpya anapozaliwa uhusiano huo unaisha kwa kuwa mama hutumia pembe kumfukuza mtoto wake mkubwa ili aweze kulea mtoto mchanga. Nyati wa kiume huacha mama zao wanapokuwa na umri wa miaka miwili na kujiunga na vikundi vya mafahali wenye umri mdogo. Nyati wanaishi katika makundi katika mfumo wa ujamaa.

Ukubwa wa makundi hutofautina kutokana na mazingira. Makundi ya kawaida huwa na mbogo wa kike wenye uhusiano wa kinasaba. Kundi hilo hujumuisha nyati jike na watoto wa ukoo mmoja. Kwa kawaida kundi la nyati jike na watoto huzungukwa na makundi madogo ya madume ya cheo cha juu ambao ndio hutumika kama walinzi wakuu.

Madume ya kiwango cha kati na majike wa kiwango cha juu na walio wazee pia huwa kando ya kundi la kawaida. Madume vijana hujitenga na kukaa eneo la mbali kidogo kutoka eneo la dume anayetawala, ambaye anajulikana kutokana na ukubwa wa pembe zake. Mafahali wazima hushiriki katika michezo na wanapoingilia katika himaya kupigana na kuanzisha vita halisi.

Wakati wa mapigano fahali mmoja atamkaribia mwenzake akiwa ameweka kichwa chake chini na kusubiri mwenzake kufanya hivyo. Wakati mafahali wanapopigana hutumia pembe zao kutoboana. Ikiwa vita hiyo ni madhumuni ya kucheza mafahali husuguana uso na miili katika mchezo huo. Vita halisi huwa hatari lakini nadra na fupi.

Ndama pia wanaweza kucheza lakini ni nadra kwa nyati wa kike kucheza. Kama ilivyo kwa wanyama wengine wakubwa nyati hawana adui wengi. Adui mkuu wa nyati ni binadamu wenye tabia ya kuwinda nyati. Ingawa nyati wanauwezo wa kuua simba, adui wa pili ni simba. Simba wakiwa kwenye kundi kubwa huweza kumshambulia nyati mkubwa na kumuua.

Mamba wa Nile hushambulia ndama na nyati wazee wasiokuwa na nguvu pia chui na fisi mwenye madoa ni tisho kwa ndama wa nyati. Hata hivi kuna rekodi chache zinazoonesha kuwa fisi wenye madoa wana uwezo wa kuwinda na kuua nyati mkubwa. Nyati wanaushirikiano wa hali ya juu kuweka ulinzi kwa kila mmoja.

Wakati wanakimbizwa na wanyama wanaokula nyama kukaa pamoja kitendo kinachosababisha wanyama wala nyama kushindwa kuchagua nyati watakayemuangusha na kumla. Ndama hukusanyika katikati. Nyati atajaribu kumnusuru mwenzake aliyeshikwa. Ndama akikamatwa hutoa sauti ya juu kuita mama yake na nyati wengine ili kutoa msaada.

Baadhi ya wataalamu wana rekodi za ndama aliyeokolewa kutoka kwenye kinywa cha simba na mamba baada ya mapigano makali kati ya kundi la nyati dhidi ya simba na mamba aliyekamata ndama.

Nyati hukaa katika kundi wakati wa kupigana na wanyama wala nyama. Wamekuwa na rekodi ya kuwasumbua simba kwa masaa mawili, baada ya simba kuua nyati mwenzao. Watoto wa simba hukanyagwa na kuuawa na nyati. Makala haya yametayarishwa kwa kutumia taarifa mbalimbali huhusu wanyama zinazopatikana katika mtandao.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi