loader
Dstv Habarileo  Mobile
PATRICK PHIRI: ‘Mtoro’ aliyegeuka mwokozi Simba

PATRICK PHIRI: ‘Mtoro’ aliyegeuka mwokozi Simba

Phiri amerudi nchini kwa mara ya tatu ajili ya kazi hiyo baada ya kuifundisha timu hiyo katika vipindi tofauti vya mwaka 2003-2005 na baadaye 2006-2008. Sasa anarithi mikoba iliyoachwa na kocha Zdravko Logarusic, raia kutoka Croatia aliyefutwa kazi Jumapili iliyopita kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na uongozi wa timu hiyo.

Awali, Phiri aliyetua nchini Jumatano wiki hii kuanza kibarua chake, pamoja na mwenendo wake mzuri ndani ya klabu hiyo katika awamu yake ya pili, alijikuta akiingia katika mgogoro na viongozi wa timu hiyo kutokana na tabia yake ya kwenda kwao mara kwa mara na hivyo kukwamisha programu za timu.

Suala hilo lililokuwa likisababisha hasira kwa viongozi hao hadi kumuonya kocha huyo. Lakini pia halikukosa utetezi wa Phiri kwa madai kuwa alikuwa akifanya hivyo kutokana na nafasi yake ya uchifu katika kabila lao, hatua iliyomlazimu kurudi nyumbani kwa ajili ya mambo hayo ya kimila.

Hata hivyo, uongozi wa Simba kupitia kwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Said Tully umesema bado wana kumbukumbu nzuri juu tabia hiyo ya Phiri na kuwa pamoja na mambo mengine, wameshalizungumzia suala hilo hivyo hakuna wasiwasi wowote. Tully amesema uongozi unatambua uwezo alionao kocha huyo ukiacha sababu zingine za nje, jambo lililowafanya kumrejesha ili kurudisha heshima yao.

Msimu uliopita, kikosi hicho cha Msimbazi kilijikuta kikiishia nafasi ya nne chini ya Logarusic aliyerithi mikoba iliyokuwa imeachwa na kocha mzalendo Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo.

Amewataka mashabiki wa timu hiyo kutulia katika kipindi hiki na kumuacha kocha huyo ili atekeleze jukumu alililopewa la kuitengeneza timu hiyo iliyopoteza imani za mashabiki wake kutokana na matokeo mabaya yakiwemo ya mchezo kati yake na Zesco United ya Zambia uliochezwa wiki iliyopita.

Amesema katika muda huo mfupi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, Phiri atapata wasaa wa kuwaangalia wachezaji wake ili kupata kikosi anachoamini kitamsaidia huku uongozi ukijiandaa kumsikiliza na kupokea ushauri atakaoutoa wa kupata kikosi bora kitakachotoa ushindani dhidi ya timu zingine.

Aidha, Tully anasema pamoja na wachezaji waliopo, pia wanaamini kocha huyo atatumia nafasi hiyo kuwaangalia wachezaji waliopo katika kikosi cha vijana cha klabu hiyo wakiwemo walioshiriki michuano mbalimbali, ikiwemo ya Rising Star ili kujiridhisha kama wapo watakaomfaa kuwaongeza katika kikosi chake au kuwakeka karibu na programu zake.

Pia anasema chini ya uongozi wa kocha huyo mpya wanaangalia namna ya kufufua upya programu ya timu ya vijana na kuangalia jinsi watakavyowatumia baada ya kuonekana kutopewa nafasi chini ya uongozi wa Logarusic, jambo lililoonekana kama kutaka kufifisha vipaji vya vijana hao.

Phiri anakuja nchini baada ya kuachana na Shirikisho la Soka la Namibia alikokuwa anafanya kazi kama Mkurugenzi wa Ufundi baada ya jina lake kuyapiku majina ya makocha wengine watatu; Waserbia Goran Kopunovic aliyeifundisha Polisi Rwanda na Milovan Cirkovic pamoja na Mdenmark Kim Poulsen.

Awali, matajiri wa Simba waliweka mezani majina ya makocha hao na la Phiri likiwemo, lakini mwishoni kupitia vikao mbalimbali vilivyofanywa na uongozi wa timu hiyo Phiri alijizolea kura zote.

Viongozi hao wa Simba awali walimjadili Poulsen huku baadhi wakimsifu kwamba akipewa Simba, ana uwezo wa kubadilisha nidhamu ya wachezaji na kuimarisha programu za vijana zilizovurugika katika kipindi cha hivi karibuni baada ya Logarusic kuingia klabuni hapo.

Logarusic alifutwa kazi Jumapili iliyopita kwa madai kuwa ni mkali, anawatukana wachezaji bila kujali. Katika mechi 13 za Ligi Kuu msimu ulipita, Simba ikiwa chini ya Logarusic imeshinda mechi tatu, sare tano na kufungwa tano baada ya kumrithi Kibadeni. Ikiwa umesalia muda mfupi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, Phiri anapewa jukumu la kurejesha matumaini mapya kwa wanamsimbazi.

Kocha huyo awali aliwaambia viongozi wa Simba kwamba hawezi kufanya uamuzi wowote wa kuja Tanzania mpaka ajadiliane na familia yake na imkubalie suala ambalo baadaye lilifanyika na hatimaye kutua nchini. Shauku kubwa kwa mashabiki wa Simba sasa ni kumwona Mzambia huyo akifanya vizuri akiwa timu hiyo ili kuondoa huzuni waliyonayo.

Huzuni hiyo inatokana na ukweli kuwa sasa wapo katika hali mbaya baada ya kuzidiwa utani na mashabiki wa Yanga baada ya kumnyakua kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo na kuja na wahezaji kutoka Brazil, na kutimuliwa kwa Logarusic.

Lakini wana matumaini hasa ukizingatia rekodi ya Phiri katika klabu hiyo ya Msimbazi. Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia, Chipolopolo ni kati ya makocha wanaopendwa na kukubalika kutokana na kazi yake nzuri. Phiri aliongoza Simba kunyakua ubingwa na kumaliza msimu wa 2009-10 bila kupoteza mechi hata moja.

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi