loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Pombe inavyoharibu maadili kwa watoto

Mambo mengi yanaweza kuua nguvu kazi katika jamii fulani, moja wa mambo hayo ambayo makala haya yatajikita zaidi kwayo ni matumizi ya pombe haramu majumbani.

Pombe inayonywewa kama kiburudisho, isipochungwa vyema, hususan pombe haramu, inaweza kuua nguvu kazi ya taifa na kuwa na jamii isiyokuwa na maadili, hali inayochangia uchumi kutokukua kwa kasi.

Zipo aina mbili za pombe, moja ni ile inayotengenezwa kiwandani ambazo viwango vya ubora wake vimethibitishwa kihalali, na ya pili ni ile ya kienyeji inayotengenezwa bila ubora, na kuthibitishwa na shirika linalohusika na viwango vya ubora wa bidhaa nchini (TBS).

Matumizi ya pombe haramu yanadhoofisha jitihada za uzalishaji zinazohimizwa kuanzia na serikali za mitaa hadi serikali kuu, hali inayotishia kuwa na jamii yenye watu dhoofu kiafya na kiuchumi.

Wilaya ya Moshi Vijijini ni miongoni mwa wilaya saba za mkoa wa Kilimanjaro, ambayo kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2012, ina jumla ya wananchi 466,737.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa msaada wa mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF), umebaini kuwa watoto wengi wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa na biashara haramu inayofanywa na wazazi wao majumbani katika wilaya ya Moshi.

Miongoni mwa maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi ni kata ya Arusha Chini, ambayo ni moja ya kata 31 za wilaya ya Moshi. Kata hii inayo matukio mengi ya utengenezaji wa pombe za kienyeji majumbani.

Pombe zinazotengenezwa majumbani na kuuzwa katika kata hiyo ni pamoja na rozela, mabobo na gongo.

Baadhi ya aina hizi za pombe zisizopimwa, zimekuwa zikiingizwa kutoka maeneo ya kata jirani za New Land, Kahe, Kiyungi na Msitu wa Tembo. Kutokana na baadhi ya wazazi kuuzia pombe hizo majumbani, watoto hao hugeuka kuwa wahudumu mara baada ya kutoka shuleni.

Sheria ndogo za vijiji vilivyopo chini ya Halmashauri ya wilaya ya Moshi sehemu ya 17 inayozungumzia udhibiti wa pombe haramu na dawa za kulevya, inatoa mamlaka kwa viongozi husika kuchukua hatua.

Sehemu hiyo ya 17 kifungu cha kwanza kinasema kwamba serikali ya kijiji itakuwa na uwezo wa kumkamata na kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejihusisha na upikaji na unywaji wa pombe haramu.

Pia katika sheria hiyo kifungu cha tano, kinasema ni marufuku kumwajiri mtoto yeyote ambaye hajafikia umri wa miaka 18 na kwamba anayepatikana kwenda kinyume na sheria ndogo hii anafikishwa mahakamani na kutozwa faini ya Sh 50,000.

Ofisa mtendaji wa kata ya Arusha Chini, Koelly Shayo, anakiri kwamba biashara ya pombe haramu inayofanyika majumbani mwao inachangia watoto kuathirika katika malezi na kukosa haki zao za msingi.

Anasema kata ya Arusha Chini yenye jumla ya kaya 2,792, wananchi wake wengi huishi kwenye kambi za Kiwanda cha kuzalisha sukari cha TPC, ambapo kampuni hiyo imetenga maeneo maalumu ya kufanya biashara, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakikiuka na kufanya biashara hiyo majumbani.

Anasema katika kata yake, tatizo la biashara ya pombe haramu majumbani limekithiri na lina athari kwa watoto, kwani wapo wanaojikuta wakinywa katika umri mdogo.

Moja ya matukio ya kushangaza na yanayochangiwa na pombe anasema ni lile la mwaka mwaka 2012 ambapo wanafunzi 31 walikamatwa baada ya kukutwa wakilawitiana.

Anasema wanafunzi hao wadogo walikuwa wakisoma katika shule za msingi za Arusha Chini, Langasani na Dr Omary wa kuanzia darasa la kwanza hadi la sita.

Shayo anasema jambo baya zaidi, kati ya wanafunzi hao mmojawapo alikuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), lakini baada ya vipimo walionekana hakuna aliyepata maambukizi hayo.

Kwa mujibu wa Shayo wakati wa kuwahoji watoto hao, baadhi walisema wamejifunza baada ya kuona wakubwa zao wakifanya mapenzi, mara baada ya kulewa wakiwa nyumbani kwao.

"Kwa vile katika kata hii kuna watu wanafanya biashara ya pombe haramu majumbani, wateja wanakaa hadi kitandani na wanapozidiwa na mahaba wanafanya uchafu huku watoto wanashuhudia," anasema Shayo.

Anabainisha kwamba kutokana na biashara hiyo, watoto wengi wamekuwa wakiathirika kwa kukatisha masomo, mimba za utotoni na kukosa lishe bora, hali inayochangia ongezeko la watoto wa mitaani.

Anasema biashara hiyo imekuwa ikifanyika hadi nyakati za usiku, ambapo watoto wanashindwa kulala wakisubiri wateja waondoke, kutokana na wateja wengine hukaa kitandani kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya msingi Langasani, Goodluck Kimambo, anakiri kuwapo kwa changamoto kubwa ya watoto kuathirika na biashara ya pombe haramu zinazofanyika majumbani mwao, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu.

Kimambo anasema Shule ya Msingi Langasani ina jumla ya wanafunzi 344, na kwamba kuwepo kwa tatizo kubwa la watoto kufanya mapenzi na wengine kulawitiana, kunatokana na malezi wanayoyapata katika maeneo wanayoishi.

Anasema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiathirika na biashara ya pombe za majumbani kutokana na kukosa muda wa kulala kwa kuwa baadhi ya wazazi huwatumia kama wahudumu.

"Biashara ya pombe inayofanyika majumbani zinaharibu sana watoto, kiwango cha elimu kinashuka, wengine wanakatisha masomo kwa kukosa ada, lakini kubwa zaidi ni tabia chafu zinazofanywa na watoto baada ya kuiga kwa wakubwa wanapolewa na kufanya vitendo vya ajabu machoni mwao," anasema Kimambo.

Mkuu wa Shule ya Msingi ya Arusha Chini, Suzan Elihaki anasema watoto ambao wazazi wao wanajishughulisha na kutengeneza na kuuza pombe haramu majumbani, wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na wanafunzi wasiokuwa na maadili.

Elihaki anasema shule yake ina jumla ya wanafunzi 485, ambapo changamoto kubwa iliyopo ni utoro, pamoja na wazazi kutokuwa tayari kulipa ada na kuwapa watoto wao vifaa vya masomo.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za Langasani, Arusha Chini na Dr Omary waliozungumza na mwandishi wa makala haya wanakiri kushuhudia matendo machafu yanayofanywa na wakubwa wakishalewa, hali inayowafanya kuona ni jambo la kawaida.

Mmoja wa wanafunzi hao (majina hayajatajwa kutokana na maadili) anasema nyumbani kwao wanatengeneza na kuuza pombe za rozela na mabobo, na kwamba mara nyingi baada ya kutoka shule husaidia kuhudumia wateja.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Aiwinia Mlay, anasema pombe zinazotengenezwa majumbani, zimesababisha baadhi ya wanafunzi kukosa maadili.

Gazeti hili pia likazungumza na mmoja wa watengenezaji na wauzaji wa pombe haramu ya rozela na mabobo, na kukiri kuwapo kwa ukiukwaji wa haki za watoto, lakini akasema ni kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

"Sisi wenyewe hatufurahishwi na mambo haya, watoto wanajifunza tabia chafu zinazofanywa na walevi hapa nyumbani. Lakini utafanyaje kama kipato ni kidogo na unataka ule na wanao?" Akahoji.

Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Moshi, Pruncen Furaha, anakiri ofisi yake kupata taarifa za watoto wa shule za msingi Arusha Chini, Dr Omary na Langasani kulawitiana na kwamba baada ya kufuatilia tukio hilo, waligundua baadhi ya watoto hao wamejifunza tabia hiyo chafu majumbani mwao kupitia matendo ya walevi.

Anasema hatua walizochukuwa ni kuanzisha kamati za ulinzi wa mtoto, ambazo zitakuwa na jukumu la kubaini watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, na kufuatilia matukio ya utengenezaji na uzaji wa pombe haramu.

Kamanda wa polisi mkoa wa kilimanjaro, Robart Boaz, anasema jeshi la polisi limekuwa likifanya msako mara kwa mara katika sehemu ambazo zinatengeneza na kuuza pombe haramu, ambapo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo.

Anasema kwa mwaka jana kuanzia mwezi Januari hadi Desemba kulikuwa na jumla ya kesi 46, ambapo jumla ya lita 360 za pombe haramu zilikamatwa, huku wanaume 60 na wanawake 23 wakikamatwa kutokana na kufanya biashara hiyo. Kamanda Boaz anasema juhudi za kupambana na utengenezaji na uzaji pombe haramu zinaendelea, kwa kushirikiana na viongozi wa vitongoji, vijiji, na kata kupitia kamati zao za ulinzi na usalama.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Arnold Swai

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi