loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Profesa Maghembe: Uhaba wa maji utabaki historia

Kupitia Wizara ya Maji, Serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya maji hapa nchini. Hii yote ni katika kutekeleza sera ya maji ambayo inasema kila mwananchi angalau asiishi umbali wa mita 400 kutoka eneo la maji yanakopatikana. Katika mahojiano na mwandishi wetu, Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe anaeleza mafanikio yaliyopatikana tangu alipoteuliwa kushika wizara hiyo.

SWALI: Serikali kupitia Wizara ya Maji imekuwa ikitoa kipaumbele kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na ya kutosha. Kwa sasa upatikanaji wa maji ukoje nchini, Mheshimiwa Waziri?

JIBU: Upatikanaji wa maji nchini kote naweza kuugawanya katika mafungu matatu; fungu la kwanza ni upatikanaji wa maji kwenye miji mikuu ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa maji vijijini na tatu ni upatikanaji wa maji katika miji midogo na miji mikuu ya wilaya.

Sasa katika miji mikuu ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam wastani wa upatikanaji wa maji ni asilimia 88, yaani katika watu 100 watu 88 wanapata maji kama ilivyoelezwa kwenye sera ya maji, lakini ziko tofauti kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine maana huo ni wastani.

Kwa mfano, hivi sasa Jiji la Dar es Salaam upatikanaji wa maji ni asilimia 60 na miji mingi ambayo ni makao makuu ya mikoa ukiacha ile ambayo ni siku za karibuni tu imefanywa mikoa kwa maana ya Njombe, Geita, Mpanda, na Simiyu, upatikanaji wa maji unafika asilimia 95, wastani wake. Kwa hiyo katika miji mikuu ya mikoa hivyo ndivyo hali ilivyo.

Katika vijiji, maeneo ya vijijini upatikanaji wa maji bado uko chini. Mwanzoni ilikuwa inajulikana kwamba upatikanaji wa maji vijinini ni kama asilimia 63 lakini baada ya kuangalia upatikanaji wa maji kwa undani na kujumlisha miradi ambayo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ya miji lakini haifanyi kazi, tukagundua mwaka jana mwanzoni kwamba upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini kwenye maeneo ya vijijini ni kama asilimia 40 hivi.

Hivi sasa kuanzia mwezi Juni mwaka jana na mpaka sasa tumeongeza upatikanaji wa maji huko vijijini kwa asilimia tisa, kwa maana sasa tumetoka wastani wa asilimia 40 hadi kufikia 49. Mategemeo yalikuwa kwamba kufikia Juni mwaka huu tungekuwa tumefika asilimia 55 na hadi kufikia mwezi Desemba mwaka kesho 2015 tutafikia asilimia 74.

Yapo matumaini kwamba lengo hilo litafikiwa. Sasa katika maeneo ya miji mikuu ya wilaya na miji midogo kama Mombo, na miji mingine kama Muheza, Korogwe, Mwanga, Magu, Lamadi, Chato, Makambako, Tunduru, Namtumbo na Mbinga, miji midogo ya namna hiyo upatikanaji wake wa maji ni mgumu sana.

Ni wastani wa asilimia 51.5, kutokana na hali hiyo mwaka huu tumechukua hatua ya kwanza ya kuhakikisha kwamba tunabadilisha hali hiyo, lengo la sera ya maji ilikuwa kwamba ifikapo mwaka 2015 katika miji hii tuwe tumefikia asilimia 55.

Lakini lengo letu ni kwamba kuanzia mwaka huu mpaka mwisho wa mwaka 2015 tunataka tufikie asilimia 70, kwa hiyo mwaka wa fedha ulioanza Juni mwaka huu tumetenga fedha ili kuipatia maji miji midogo 48 na tunataka katika hiyo miji hiyo 48 wastani wa upatikanaji wa maji ufikie asilimia 80.

Kwa hiyo tukiongeza mwaka ule unaofuata, miji mingine 48 au 50 tuna uhakika kwamba tunaweza kupata hata hilo lengo ambalo tumelisahihisha kutoka asilimia 55 na kufika asilimia 80.

SWALI: Ingawa kuna watu ambao kazi yao ni kuponda, lakini Watanzania wengi wanaona juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwapatia maji. Ni ipi tathmini yako tangu ushike wizara hii?

JIBU: Labda niseme hivi kwamba ni jambo la kutia faraja kama Watanzania wanaona juhudi kubwa ambazo tunafanya kuwapelekea maji. Maji katika maeneo ya vijijini na maeneo mengi ya mijini bado ni tabu hasa miji ile ya wilaya, miji mikuu ya wilaya na miji midogo.

Sisi tumedhamiria katika kipindi hiki kisichozidi miaka miwili ya utawala wa Rais Kikwete ambacho kimebaki, tufanye mabadiliko makubwa kabisa ili wale watakaopokea Wizara ya Maji kutoka kwetu au Rais ajaye atakapokuwa anapokea nchi kutoka kwa Rais Kikwete, apokee nchi ambayo haina matatizo makubwa ya maji kama ambavyo Rais Kikwete alipokea.Hayo ndio malengo.

Kwa hiyo tunataka kuleta mageuzi kabisa katika hali ya upatikanaji wa maji hapa nchini ili kuhakikisha tatizo hili sasa linakuwa ni dogo si kama ambavyo tumelipokea.

SWALI: Unazungumziaje utekelezaji wa sera ya maji hapa nchini?

JIBU: Sera ya maji inasema kila mtanzania, aishi angalau akiwa mbali sana na maji isizidi mita 400. Sasa hili la upatikanaji wa maji majumbani haya ndio malengo ya sera. Lakini malengo ya sera pia yanaeleza kwamba rasilimali za maji lazima tuweze kuzilinda ili miradi hii ambayo tumeijenga kupeleka maji nyumbani, mijini na vijijini iweze kuwepo kesho na tuweze pia kuwarithisha wajukuu zetu, hilo la kwanza.

Lakini la pili ni kuhakikisha kwamba maji yanakuwepo kwa ajili ya umwagiliaji kwani ni kitu muhimu katika kukuza kilimo chetu ambacho muda mwingi kimekuwa kikitegemea mvua. Malengo ni asilimia 80 ya matumizi ya maji yawe kwa ajili ya kumwagilia mashamba, kwa hiyo maji yale ya umwagiliaji yanatakiwa yawepo ili kukidhi mahitaji ya watu ambao wanaendelea kuongezeka katika nchi yetu.

Na jambo la tatu, ni kuhakikisha kwamba maji yanayotumika katika kuendeleza viwanda yanapatikana. Maji yanatakiwa katika viwanda vya saruji, viwanda vya kutengeneza nguo, kusindika ngozi, viwanda vya kusindika mazao ya chakula, katika kuzalisha umeme, na katika uchumi kwa ujumla, katika madini, katika maliasili, maji kwa ajili ya wanyama pori nk.

Maji haya yanakuwepo leo, kesho na kuweza kurithisha vizazi vijavyo. Jambo la nne ni kuhakikisha kwamba viumbe ambao wako kwenye nchi yetu na viumbe vile ambavyo sehemu moja ya maisha yake inatumika kwenye maji na sehemu nyingine ambayo wanaishi kwenye nchi kavu, viumbe hao wanaweza kuishi na kuzaliana na hata kuongezeka kuliko walivyokua huko nyuma, ili nchi yetu iendelee kuwa nchi ambayo inahifadhi bioanuai kuliko nchi nyingi duniani. Hayo ndio malengo ya sera, na kwa ujumla malengo haya tunataka tuyafikie.

SWALI: Mheshimiwa Waziri, tungependa utueleze miradi ya maji mikubwa ambayo umeisimamia na mafanikio yake yanaonekana kwa Watanzania.

JIBU: Iko miradi mikubwa kadhaa ambayo tunaendelea kuisimamia. Iko ambayo imekamilika na iko mikubwa ambayo bado. Miradi ambayo ni mikubwa ni ile ambayo inahudumia watu wengi, na miradi ya namna hiyo kwa kawaida iko kwenye miji yetu mikuu. Katika miji mikuu ni pamoja na programu ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam, ambao utagharimu Shilingi trilioni moja na bilioni mia mbili.

Hivi sasa tunajenga bomba kubwa la maji kutoka Ruvu pale Bagamoyo kuja mpaka kwenye Chuo cha Ardhi pale Dar es Salaam, mradi huu una sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni mtambo wa kuchuja na kutibu maji ambao tayari tumeujenga na mtambo huo umegharimu dola za Marekani milion 37 sawa na bilioni 50 za Kitanzania.

Sehemu ya pili ni kujenga bomba ambalo linaleta maji. Mtambo ulioko pale Mtoni umekamilika na bomba la maji limeshakuja ambalo lina urefu wa kilometa 55.5. Tayari tumeshalilaza zaidi ya kilometa 40 tumebakiza kama kilometa 15, kisha maji ya kutosha yataingia mjini. Tunategemea kwamba ifikapo mwisho wa Juni mwaka huu tayari bomba hilo litafikisha maji pale Chuo Kikuu cha Ardhi.

Na gharama ya hili bomba ni Shilingi bilioni mia moja na kumi na nane za Tanzania na fedha hizi zinatolewa na Serikali ya Tanzania. Zile za kujenga mtambo, Shilingi bilioni 50 zimetolewa na Serikali ya Marekani kupitia mradi wa changamoto za Milenia (MCC). Hivi sasa pia niseme tu kwamba baada ya kukamilisha hiyo miradi miwili maji yatakayokua yanaingia Dar es Salaam, kuanzia kwenye kile kichoteo cha Ruvu Chini yatakuwa mengi kuliko ilivyo sasa.

Wakati huohuo tunajenga mtambo mwingine wa kuchuja maji pale Ruvu Darajani kama unakuja barabara ya Morogoro na fedha tutakazotumia kujenga pale ni dola za Marekani milioni 40 ambazo ni kama bilioni 65 za Tanzania. Mkandarasi ameshaanza kazi, lakini hiyo inajengwa pamoja na mtambo wa kuchuja na kutibu maji.

Pamoja na kazi hiyo tunalaza bomba kubwa kutoka pale Ruvu Darajani kuja mpaka Kibamba ambapo tutajenga tangi kubwa la maji na kutoka pale Kibamba tutajenga matoleo ya kuleta maji mpaka pale Kimara na hili litaongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni
82 za sasa hadi lita milioni 196.

Sasa tukishakamilisha hii miradi miwili ule wa Ruvu Juu na Ruvu Chini tutakuwa na maji yanayozidi lita milioni 450 ambayo ndio mahitaji ya sasa ya Jiji la Dar es Salaam. Lakini lengo letu sio kukidhi mahitaji ya sasa tu, tunataka kukidhi mahitaji ya sasa na miaka 20 mbele, kwa hiyo tumechimba visima kule Kimbiji na eneo la Mpera na kutoka kule tutaleta maji yanayofikia mita za ujazo mia mbili na sitini milioni.

Kwa hiyo ukijumlisha maji ya Ruvu na visima ambavyo tunachimba katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, kufika mwezi Juni mwaka 2016 tutakuwa tumefikisha Dar es Salaam mita za ujazo zaidi ya milioni 720, hizi zinatosha mahitaji ya Dar es Salaam, kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2032.

Huo ni mradi mmoja mkubwa sana kati ya miradi hiyo na hivi sasa tumeanza kuchimba visima kule Kimbiji. Visima 20 tumeanza kuvichimba na tumekamilisha visima 8 kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya maji yaliyoko chini katika eneo lile kwamba yanatokea wapi na kwamba tutakapokuwa tunasukuma maji mengi kutoka mle hali ya maji katika eneo hilo itakuaje.

Lakini pia tunajifunza kwamba maji yale ubora wake upo hivyo hivyo tunavyojua sasa au unaweza kubadilika kadri ambavyo tunayasukuma. Utafiti huu ni muhimu kwa ajili ya watumia maji hayo sasa na miaka 20 hadi 30 ijayo. Huo ni mradi wa kwanza, lakini pia tunayo miradi mikubwa katika miji mbalimbali.

Tunamradi mkubwa wa maji ambao unatekelezwa mjini Musoma. Katika mradi huo tunatumia Shilingi bilioni 79 katika Mji wa Musoma peke yake kwa ajili ya kuchota maji kutoka Ziwa Victoria, kuyachuja na kuyagawanya kwa wananchi. Mradi huu umetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 40 sasa.

Tunatekeleza mradi wa maji pia katika mji wa Bukoba. Hapa tunatumia zaidi ya Shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kutoa maji Ziwa Victoria na kuyasambaza katika Mji wa Bukoba. Mbali na miji ya Bukoba na Musoma hivi sasa tunajiandaa kutekeleza mradi mkubwa kuwapatia watu maji katika maeneo ya vilima jijini Mwanza.

Watu ambao unaweza kuwaona wanakaa kwenye milima na kwenye mawe juu jijini Mwanza ni vigumu sana hata kuchimba vyoo.
Kwa hiyo tunataka kuwatengenezea maji salama yawafikie huko huko vilimani. Tunataka kuwatengenezea utaratibu wa kuondoa uchafu ndani ya nyumba zao na uchafu wa vyoo ili waweze kuondoa uchafu katika maeneo ya milimani.

Lakini huu ni mradi mkubwa ambao utatumia Euro milioni 105 ambazo ni sawa ni Shilingi bilioni 220. Sasa fedha hizi pia zitatumika kuwapatia maji wananchi wanaokaa Lamadi ambao ni mji mdogo, Magu, Misungwi, Sengerema na Nansio na kuhakikisha kwamba miji hii yote inapata maji safi na salama.

Sasa nje ya hiyo tunatekeleza mradi wa maji mkubwa pale Tabora, tunatekeleza pia mradi mkubwa wa maji pale Singida ambao umekamilika, na tunatekeleza miradi mikubwa miwili ya maji pale Dodoma; mradi wa kukipatia maji Chuo Kikuu cha Dodoma na kuondoa maji taka kutoka chuo hicho ambao unagharimu Shilingi bilioni 28 na mradi wa kuleta maji mjini Dodoma.

Pale Dodoma upatikanaji wa maji umeshuka na kufikia asilimia 74 kutokana na ongezeko la watu na vyuo. Tunataka kuongeza kiwango hicho kizidi mahitaji ya pale ili Mji wa Dodoma ambao umepangwa kuwa mji mkuu uweze kuwa na maji mengi ya kutosha ya kufanya watu wahamie huko.

Pale Morogoro, tunajenga chujio la maji kule Magadu na zaidi ya hapo tumekamilisha mradi wa maji Iringa, tumekamilisha mradi wa
maji Mbeya, tunatekeleza mradi wa maji Songea na tunatekeleza miradi ya maji, Lindi, Sumbawanga na Mtwara. Hii ni miradi mikubwa
sana ambayo inaendelea kutekelezwa.

Ndio maana nilikuwa nakwambia itakapofika mwishoni mwa mwaka kesho 2015 miji hii mikubwa tutakuwa tumefikisha zaidi ya asilimia 95 ya upatikanaji wa maji. Hii ni kusema kwamba miji hii mikubwa itakuwa inapata maji safi na salama pengine kupita miji yote hapa Afrika.

SWALI: Pamoja na kuwa na jitihada kubwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati, bado wananchi
wanawanyooshea vidole watendaji kwa kukwamisha jitihada hizo. Una wito gani kwa watendaji wa aina hiyo katika wizara yako?

JIBU: Nataka niseme tu kwamba, kulikuwa na urasimu mkubwa sana wa utekelezaji wa miradi ya maji katika wizara, miradi yote
hasa ile ya vijijini ilikuwa haitekelezwi mpaka kwenye wilaya, wametangaza, upande wa kandarasi wanaopendekezwa, washauri halafu walete wizarani wapeleke na Benki ya Dunia kisha Benki ya Dunia iseme hatuna tatizo ya ninyi kuwachagua wasimamizi hawa na
wizara nayo iseme hatuna tatizo na ninyi kumchagua mkandarasi huyu na utaratibu huu ulikuwa unachukua muda mrefu sana.

Kutokana na hilo miradi mingi ilikuwa haitekelezwi na wilaya zilikuwa zinapokea hela nyingi zinawekwa kwenye akaunti lakini watu hawana maji. Hatua moja ambayo nimeichukua pale wizarani ni kufuta huo urasimu.

Baada ya kufuta huo urasimu tulitoka kwenye wilaya 12 ambazo zilikuwa zimeruhusiwa na huo urasimu tukafikia wilaya zote 132 katika utekelezaji wa miradi na sasa baada ya wilaya zingine mpya kuongezwa utekelezaji ukaongezeka mpaka kwenye wilaya zote mpya ambazo zimeongezwa.

Kitu ambacho nataka nitoe kama wito kwa watendaji wote ni kwamba wafuate usanifu uliofanywa na kupitishwa na wataalamu
wasiwe na mradi ambao usanifu na kazi inayotakiwa kufanywa imekadiriwa kuwa Shilingi milioni mia tatu halafu wakatangaza mradi wakampa mkandarasi anayetaka kutekeleza kwa Shilingi bilioni 4, yaani kumpa mkandarasi mkataba ambao unazidi rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Nimekutana na wakurugenzi wote wa wilaya, nimekutana na wakuu wote wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa, wahandisi wote
wa mikoa pamoja na wakuu wote wa mikoa na kuzungumza ni jinsi gani tuongeze nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maji na
tumekubaliana kwamba miradi itekelezwe kwa haraka.

Kwa sababu wizara imewekwa kwenye mfumo wa utekelezaji wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kwa sababu wote
tumekubaliana na tuna lengo moja na kila mkuu wa mkoa ana miradi yake ambayo ina malengo na muda wa kutekelezwa, na kila mkuu wa wilaya ana miradi yake aliyoambiwa hii ni lazima ikamilike kwa kipindi kilichowekwa ni matumaini yangu kwamba kila mmoja
atatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kila mmoja amepewa orodha ya miradi yake, kila mtu anatakiwa kupambana kuhakikisha miradi yake inatekelezwa na inakamilika.
Nataka nikuhakikishie kwamba katika Wizara ya Maji, kila mtu anaelewa kwamba BRN yake ni nini. Kuna uelewa wa moja kwa moja wa mia kwa mia, kila mtu anajua jukumu lake, kila mtu anajua kazi yake ni nini na kila mtu anajua kazi yake inahitajika iwe imekamilika na inahitajika lini na iwe na ubora wa namna gani.

Kwa hiyo kutokana na uelewa wa namna hiyo, uelewa wa kila mmoja kujua wajibu wake bila shaka miradi inatekelezwa kama
ilivyopangwa. Hivi sasa tunatekeleza miradi 1600 pamoja na matatizo ambayo tunakumbana nayo kwani wakati mwingine fedha hutoka kwa polepole sana. 

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi