loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rai ya Dk Shein ifanyiwe kazi

Tunaamini rai aliyoitoa Rais wa Zanzibar ichukuliwe kama mkakati, kwa kuwa Tanzania tunao wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali na wamefanya tafiti nyingi, ambazo kama zingeweza kuwafikia walengwa na kufanyiwa kazi, tungekuwa tumepiga hatua kubwa kimaendeleo na kisekta.

Zipo tafiti nyingi zilizofanywa na wataalamu mbalimbali hapa nchini, zimeishia kwenye makabati na hazifanyiwi kazi, zaidi ya kutumiwa na wataalamu hao, kufanikisha tafiti nyingine.

Nchi zote zilizoendelea, zimetumia tafiti za wataalmu mbalimbali, zikawekwa mezani, zikachambuliwa na hatimaye kusaidia kuweka mikakati ya kiutendaji. Nyingi ya tafiti hizi, zimekuwa zikiishia kuwasilishwa kwenye kongamano, warsha na semina.

Baada ya hapo, hutelekezwa kwenye makabati, jambo ambalo haliwezi kutusaidia kuleta maendeleo.

Tukirudi kwenye rai ya Rais Shein, anasema matokeo ya tafiti nyingi kuhusu kilimo na mifugo, ambavyo ndivyo msingi wa sherehe ya Nanenane, inayoadhimishwa na wakulima na wafugaji, na ambayo yameletwa katika maonesho hayo, hayana budi kufikishwa kwa walengwa hao.

Alisisitiza kwamba tafiti hizi ni za msingi katika maendeleo ya taifa, hivyo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ‘Matokeo Makubwa Sasa, Kilimo ni Biashara’, utekelezaji wake hauna budi uzingatie umuhimu wa tafiti katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuzifanyia kazi changamoto na kwamba zinakwamisha kufikia lengo la kaulimbiu hiyo.

Alitaka wananchi ambao wamepata nafasi ya kushiriki maonesho hayo, kutumia nafasi hiyo kubadilishana uzoefu, wakitumia wataalamu wa kilimo, uvuvi na ufugaji, wakiwamo wadau wengine.

Pia, alikumbusha kwamba kwa Tanzania Bara pekee, sekta ya kilimo inachangia asilimia 24 ya pato la taifa na pia inatoa ajira kwa asilimia 80.

Kwa mantiki hiyo, kilimo kama ambavyo kimekuwa kikisemwa ni uti wa mgogo kwa taifa hili, ni lazima kiwe cha kisasa kinachoendana na ushauri wa kitaalamu ili kiweze kukidhi matakwa ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Zipo tafiti nyingi ambazo zinaonesha kwamba kilimo cha umwagiliaji, ambacho kinaepusha utegemezi wa mvua za msimu. Tuna mito na maziwa.

Tunao uwezo wa kuwa na kilimo cha mwaka mzima. Tuna maeneo mengi ambayo wafugaji wanaweza kuyatumia kufuga kwa faida.

Kama tafiti zitaondolewa kwenye makabati na kupelekwa kwa walengwa, zikatumika vyema, ni ukweli usiopingika kwamba, Tanzania ina nafasi ya kuondokana na lindi la umasikini, kwa kuwa asilimia kubwa ya watu wake, wanaangukia katika kilimo, ufugaji na wavuvi.

Na kama hivi ndivyo, basi tuzingatie rai ya Rais wa Zanzibar, Dk Shein. Tutumie tafiti zilizopo na zijazo, kujikwamua na kukabiliana na umasikini uliopo sasa.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi