loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Real Madrid kuibua vipaji Tanzania

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alipozungumza na waandishi wa habari katika hafla ya pamoja kati ya wachezaji hao pamoja na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu iliyoandaliwa na Kampuni ya TSN Supermarkets iliyodhamini ujio wa timu hiyo.

Dk Mukangara alisema ujio wa timu hiyo ni faraja kubwa na jambo la kujivunia na kwa namna ya kipekee limesaidia kuamsha hisia za kimichezo kwa kila Mtanzania na kwamba ili kuendeleza hali hiyo itakuwa jambo jema kujengwa kwa kituo cha michezo kitakachojikita zaidi katika kuibua vipaji vya soka.

Bila kutaja ni lini kituo hicho kitakamilika na kuanza shughuli zake na ufundishaji wa soka, Dk Mukangara alisema malengo ni kuona jambo hilo linafanyika mapema iwezekanavyo hatua aliyosisitiza kuwa italeta chachu katika mchezo wa soka.

“Hii itakuwa Academy ya kwanza ya Real Madrid katika bara la Afrika, tayari tumeanza mipango hiyo na tunaamini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wapenda michezo tutaweza kufanikisha suala hilo tunaloamini kuwa litasaidia kuibadilisha ramani ya soka kwa taifa letu,” alisema Dk Mukangara.

Aliwataka wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, kampuni, taasisi na watu binafsi wenye mapenzi mema na kutaka maendeleo ya taifa lao kujitokeza ili kusaidiana na Serikali kufanikisha suala hilo alilosema kuwa litaiwezesha Tanzania kujitambulisha katika ramani ya kimichezo.

Akizungumzia ujio wa wachezaji hao ambao baadhi wameondoka nchini huku wengine wakitarajia kuondoka leo, Dk Mukangara alisema kwa kiasi kikubwa watasaidia kuitangaza Tanzania huku akisisitiza kuwa mipango ya Serikali ni kuona mchezo wa soka unakua siku hadi siku kutokana na mikakati iliyopo na inayoendelea kufanywa.

Timu ya wachezaji wakongwe wa Real Madrid mwishoni mwa wiki ilicheza mchezo wa kirafiki na timu ya wachezaji wa Tanzania waliowahi kuzichezea klabu mbalimbali na kuibuka na ushindi wa magoli 3-1, mchezo ulioshuhudiwa na maelfu ya Watanzania wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Endapo mpango wa kujenga kituo cha Real Madrid utakamilika, utakuwa wa pili baada ya kile cha Sunderland ambacho Waziri Dk Mukangara alisema ujenzi wake unaotarajiwa kujengwa eneo la Kidongo Chekundu utaanza wakati wowote baada ya taratibu kuikamilika.

Alisema kituo hicho kinachojengwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Umeme ya Symbion kama itakavyokuwa kwa Academy ya Real Madrid kitasaidia kuibua vipaji vya mpira kwa vijana mbalimbali wa Kitanzania na hivyo kuleta mabadiliko katika soka nchini.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi