loader
Rose Muhando bado ‘anakamua’ Injili

Rose Muhando bado ‘anakamua’ Injili

Mwanadada huyo mzaliwa wa Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro, ni moja ya alama za muziki wa injili nchini, akifahamika kwa uwezo wake mkubwa wa kuimba na hivyo kujizolea mashabiki lukuki. Ni mmoja wa wasanii waliotoa mchango mkubwa katika kuufanya muziki wa injili nchini na hata nje ya mipaka ya Tanzania, ujipatie umaarufu mkubwa.

Nyimbo zake zimewavutia mashabiki wa ndani na nje ya Tanzania, kiasi kwamba akipanda jukwaani, anawainua maelfu ya watu waliokaa kucheza muziki huo ambao miaka ya karibuni, umetokea kupendwa. Kama hiyo haitoshi, msanii huyo hajachoka katika kutunga nyimbo hizo za kumsifu Mungu.

Sasa anakuja na albamu mpya atakayoizindua kesho Jumapili kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Ameipa jina la Kamata Pindo la Yesu. Ni albamu yake ya saba. Nyimbo zilizopo katika albamu hiyo mpya ya Rose Muhando ni Bwana Niongoze, Wewe Waweza, Usiniache, Nibariki, Muongo, Kwema, Kamata Pindo la Yesu na Facebook.

Msanii huyo kabla ya kupakua albamu hiyo inayozinduliwa kesho, anatamba na albamu yake ya Utamu wa Yesu yenye nyimbo saba, ambazo ni Utamu wa Yesu, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia. Mbali na Utamu wa Yesu, Rose Muhando pia amewahi kutamba na albamu za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawasawa, Kitimutimu, Mungu Anacheka, Wololo.

Pia amepata kung’ara katika wimbo wa Vua Kiatu, alioshirikiana na Anastazia Mukabwa wa Kenya. Muhando anasema amepania kufanya mambo makubwa kama alivyofanya alipozindua albamu zake zilizopita za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange SawaSawa na Utamu wa Yesu.

Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la Anglikana la Chimuli lililoko Area E, Dodoma, anasema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na kufanya mazoezi, pia amekuwa akifunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.

Anawaomba mashabiki wamiminike kwa wingi kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee kuona mambo mazuri aliyowaandalia katika uzinduzi huo na kuongeza kuwa kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwake.

“Mashabiki waje kwa wingi kuona uzinduzi wa Kamata Pindo la Yesu. Naamini watafurahia mambo mazuri na nyimbo zilizopo katika albamu hiyo,” alisema Rose Muhando aliyezaliwa mwaka 1976, Dumila, Kilosa. Anasema mbali ya kushuhudia akiimba albamu yake hiyo, lakini pia mashabiki watapata fursa ya kupata uhondo kutoka kwa waimbaji wengine wa muziki wa injili ambao ni maarufu kwa wapenzi wa muziki huo. Miongoni mwao ni Ephraim Sekeleti.

“Sekeleti ameniambia ana wimbo maalumu anauandaa kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wake, amenihakikishia atafanya mambo mazuri zaidi,” anasema Muhando katika mahojiano na gazeti hili. Waimbaji wengine ambao wameshathibitisha kushiriki uzinduzi huo ni Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, John Lissu, Sarah K na Bonny Mwaitege.

Pia mwimbaji huyo aliishukuru Kampuni ya Msama Promotions kwa jitihada zake katika kuhakikisha uzinduzi huo unakuwa mzuri na wa aina yake. Baada ya uzinduzi huo wa Diamond Jubilee kesho Jumapili, Rose Muhando atawapelekea uhondo mashabiki wake wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Baada ya uzinduzi huo ambao mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Rose Muhando anatarajia kuitambulisha albamu yake hiyo katika mikoa ya Tabora na Geita. Alisema albamu hiyo pia itatambulishwa mkoani Tabora Agosti 8, wakati siku inayofuata itatambulishwa mkoani Geita na Agosti 10 itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

“Naomba mashabiki wangu wa maeneo hayo wajipange kuona mambo mazuri niliyowaandalia,” alisema Muhando. Historia ya maisha ya Rose Muhando inaonesha kuwa alizaliwa mwaka 1976 kijijini Dumila, Kilosa mkoani Morogoro, kwa wazazi Waislamu. Rose ambaye ni mama wa watoto watatu, anadai kutokewa na muujiza wa Yesu Kristo wakati akiwa mgonjwa mahututi katika umri wa miaka tisa, akiwa amesumbuka kwa miaka mitatu bila kupona, baadaye kupona na kubadili dini kuwa Mkristo.

Alianza muziki akiwa mwalimu wa kwaya katika Kwaya ya Kanisa la Saint Mary’s la Anglikana Chimuli katika Manispaa ya Dodoma. Kulingana na ushuhuda wake, anasema sauti ilimtokea ikisema: “Mimi ni Yesu Kristo, nimekuponya, amka na nenda ukanitumikie.” Kimuujiza alipona maradhi yaliyokuwa yakimsumbua na ndio mwanzo wa kubadili dini na kuwa Mkristo.

Na huo ukawa mwanzo wake wa kuanza kumtumikia Yesu kuanzia katika kwaya hiyo ya Dodoma, na hadi sasa akiwa na watoto watatu, lakini hajaolewa, kwa kuwa kazi yake ni kumtumikia Mwenyezi Mungu. Watoto wake ni Gift Sheheba, Nicholas Winton na Maxmillian ambao wawili wanaelezwa kuwa wanapenda kuimba.

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi