loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rushwa itaimaliza soka ya Tanzania

Mambo hayo manne yako nyuma ya pazia ambayo shabiki au mpenzi wa soka ni ngumu kuyagundua kwa sababu hayapo wazi wazi na yote yanafanyika kwa kificho sana.

Hayo mambo kwanza kwa wachezaji kudanganya umri, uchawi au ushirikina, wachezaji walio wengi kutumia dawa za kuongeza nguvu hasa bangi na rushwa yaani kununua mechi au kuuza mechi au hata waamuzi kupewa kitu kidogo ili kuibeba timu fulani yaani kuisaidia kupata ushindi kwenye mchezo husika.

Hili suala la rushwa kuwemo kwenye ligi ya Tanzania limeanza kusemwa tangu muda mrefu na limeshika kasi siku za hivi karibuni ambapo wadau wengi wamekuwa wakilalama kuhusu kupenyezwa mlungula ili kupata ushindi na wengine wanasema hata baadhi ya waamuzi wamezoea kupokea kitu kidogo na hadi wengine wanaomba wapangwe kwenye mchezo wa timu fulani ambao anajua hawezi kukosa kitu kidogo.

Kipindi cha nyuma kulikuwa na kitu kinaitwa uzalendo yaani timu mwenyeji ilikuwa lazima ashinde na watu walikuwa wanajua baadhi ya viwanja fulani huwezi kupata ushindi ukiwa timu ngeni. Viwanja kama Ilulu mkoani Lindi na timu yao ya Kariakoo, iliaminika ni ngumu kushinda hapo Lakini hivi sasa sio uzalendo tena, bali ni kitu kidogo.

Naweza kusema kwa kipindi kama cha miaka sita hadi nane hivi wapenda soka wamekuwa wakilalamika kuwa kwenye ligi ya Tanzania kuna dalili ya kitu kinachoitwa rushwa, lakini wahusika wapo kimya tu kama hawalioni au hawalisiki vile. Inakuwa ngumu kuligundua suala hili kwani ili kuthibitisha unahitaji ushahidi wa wazi wazi na umshike muhusika na hapo ndio utafanikiwa kwa sababu wahusika wenyewe wanafanya uovu huo kwa siri sana.

Walengwa katika suala hili la kulihujumu soka letu ni wachezaji wenyewe, waamuzi na viongozi wa timu mbalimbali ambao ndio wanasemekana ni vinara wa kuwashawishi wachezaji au waamuzi kupokea huo mlungula ili kuzibeba timu zao kupata ushindi. Kwa wachezaji ni kwamba anapewa rushwa ili acheze chini ya kiwango ili kuipa nafasi timu pinzani kushinda mchezo husika huku akijua kufanya hivyo ni kosa la jinai na kulidhalilisha soka, ila yeye hajali hilo.

Kwa waamuzi, wenyewe wanapewa fungu hilo au rushwa hiyo ili kuionea timu fulani na kuibeba nyingine ili ipate matokeo mazuri uwanjani na wahusika wakuu wanaofanya uchafu huo ni viongozi ambao wapo mbele na ukiwaona inakuwa ngumu kuamini kama kweli ni wao wanaofanya unyama huo kwenye soka la Tanzania na kila siku wanaongoza kupiga kelele eti soka la Tanzania linashuka.

Litapandaje au litakuwaje hilo soka la Tanzania wakati wewe kiongozi unatoa rushwa ili kuipa ushindi bandia timu yako na kuifanya iwe bora wakati haina ubora wowote. Wadau wengi wanasema rushwa hiyo inapenyezwa sana hasa kwenye kipindi kama hiki cha lala salama ya Ligi Luu Tanzania Bara yaani hapa rushwa nje nje ili kuibeba timu fulani iwe bingwa au ikwepe kushuka daraja.

Na wakati mwingine kuna kupanga matokeo yaani timu kwa timu zinajipangia zenyewe matokeo kabla ya hata kuingia uwanjani yaani wanakuwa washajua leo tukafungane ngapi ngapi au mchezo huu tukatoke sare ili timu zenu ziwe kwenye nafasi flani na kuweza kuimaliza timu nyingine.

Wadau wengi wanapiga kelele na hasa ukiingia kwenye mitandao ya kijamii hivi sasa kila shabiki wa soka analalamika rushwa inatumika kupanga matokeo kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara.

Sasa hapa ninajiuliza hivi Shirikisho la Soka Tanzania halisiki haya yanayosemwa au hawajui nini kinatendeka nyuma ya pazia? Kama kwao TFF inakuwa ngumu kuyafanyia kazi, basi itakuwa vyema kama wakilipeleka kwa wahusika ili walifanyie kazi. Najua itakuwa ngumu ila katika kuliokoa soka la Tanzania sasa inabidi ufanyike uchunguzi wa kina maana hali inakuwa ngumu na kuendelea kuliacha ni kama kulipeleka soka letu kuzimu.

Ni kweli wanalipeleka soka letu kuzimu maana wanatupangia matokeo ambayo hayastahili kuwepo na kuwaaminisha watu au mashabiki kuwa timu zao zina ubora, lakini ukweli wa mambo haupo hivyo. Timu ambazo zinatuhumiwa katika hilo la kutoa rushwa ni zile zenye uchumi mzuri ambazo mara nyingi zinapigana vikumbo kwenye kuwania mataji na huko ndiko wengi wanasema kunatoka rushwa kubwa kuliko kwenye kupigania kutokushuka daraja.

Na hapa ndio ninajiuliza maswali mengi kuliko majibu hivi inakuwaje timu inanunua wachezaji kwa fedha nyingi na kuwalipa mamilioni ya shilingi, lakini mwisho wa siku eti wananunua mechi hizo akili au matope. Wanaajiri makocha wa kigeni kutoka Ulaya na kuwalipa fedha nyingi wakati ubingwa wenyewe wanaoutaka wanajua fika wataupata kwa kununua mechi, huo si wendawazimu?

Ni bora wakaacha kabisa kuwaajiri makocha hao hata hao wachezaji wa kigeni si hawana maana tena kama mnajua fika kwamba rushwa ndio inawapa heshima kwa mashabiki wenu.

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Simba, Dan Mrwanda ambae kwa sasa anacheza soka la kulipwa Vietnam, anasema anahisi hivyo kuwa kuna dalili ya rushwa kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na baadhi ya mambo ambayo yanatia shaka kuwa kuna mlungula ndani yake.

Lakini anasema anakosa uthibitisho kamili wa moja kwa moja katika hilo, lakini akasema itakuwa vyema ukafanyika uchunguzi ili kupata ukweli katika hili na kama ni kweli, basi liweze kukomeshwa.

Mrwanda anawanyonesha kidole viongozi wa klabu kwa kusema kama kuna rushwa, basi wao ndio wahusika wakuu na kutoa mwito kwa Jeshi la Polisi na Takukuru kuingilia kati kuinusuru soka ambayo inaonesha dalili za rushwa na kuwakatisha tamaa watu wenye nia njema ya kuwekeza kisoka Tanzania. Kiujumla rushwa ni mbaya kwenye soka.

Kumbukeni kuwa rushwa ndio iliyoishusha heshima Ligi Kuu ya Italia, Serie A ambayo imekuwa ni ya kawaida tu kutokana na tuhuma za rushwa na kupanga matokeo. Hivi sasa mechi kubwa nchini Italia ya wapinzani wa jadi wa mji wa Milan yaani AC Milan na Inter Milan imekuwa ni kama mechi ya kawaida tu kutokana na tuhuma hizo za rushwa.

Hivyo tuwe makini ama sivyo huko tunakoenda mechi ya Simba na Yanga itakuwa kama mechi ya Inter Milan na AC Milan yaani itakosa mvuto kwa sababu watu watakata tamaa na watajua kila kitu kimepangwa sasa wakafanye nini uwanjani.

Rushwa kwenye soka madhara yake ni makubwa sana na suluhisho ni kama alivyosema Mrwanda ni kwa Polisi na Takukuru kuingilia kati suala hili ambalo likiachiwa, tunalimaliza soka letu. Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania anayesoma China, akipatikana kwa simu ya mkononi: +8615180191494, email: evancemhando@gmail.com, Instagram : mo1188.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Mo van der Mhando

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi