loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Saa 26 ndani ya Ziwa Nyasa na Mv Songea

Wapo baadhi ya viongozi wa Serikali, mikoa yote miwili ya Mbeya na Ruvuma waliomshawishi na kumkatisha tamaa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana kwamba safari hiyo sio salama na hakuna meli bora ya kumsafirisha yeye na msafara wa watu 40 hivi.

Kinana akasema, lazima safari hiyo itekelezwe kama meli ni mbovu basi ifanyiwe matengenezo. Na kwa sababu zilikuwa meli mbili Mv Iringa na Mv Songea alishauri yoyote ifanyiwe marekebisho lakini safari ni lazima.

Siku chache kabla ya safari ya majini ya saa 26 kufika, Novemba 23, meli ya Mv Iringa ilikuwa juu ya mawe, hivyo fundi kutoka Mwanza aliletwa chini ya himizo kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe.

Meli ilitengenezwa na kufanyiwa marekebisho yaliyogharimu fedha, nyingi anasema Nahodha wa meli hiyo mzoefu kwa zaidi ya miaka 30, Tomas Faya. Safari ya kwenda kupanda meli siku hiyo ilianzia Lituhi, Nyasa ambako tulikuwa na ziara jana yake ya kukagua mto Luhuhu, kuzungumza na wananchi katika jimbo la Mbinga Magharibi la John Komba tukalala huko.

Asubuhi tulianza safari saa 1.30 kwenda Mbambabay umbali wa kilometa 110, saa nne na dakika kadhaa tulipanda meli ya Mv Songea kwenda Kyela, umbali wa siku moja na saa mbili.

Msafara huo uliongozwa na Katibu Mkuu CCM Abdulrahaman Kinana, lakini ulikuwa pia na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro na Nape Nnauye anayeshughulikia Itikadi na Uenezi, pamoja watendaji wa Ofisi ya Chama Lumumba na waandishi wa habari 14 hivi, kati yao wawili wasichana.

Watu wa Nyasa, walitupungia mikono wakishangaa uamuzi wa kupanda meli iliyochoka, wakatusindikiza kwa kupanda ngarawa mbili ndani ya maji umbali wa kilometa tano hivi, wakatuacha tukipasua mawimbi ziwani. Walituacha kwenye maji, lakini walipita nchi kavu kwenye barabara kila kituo meli iliposimama, Liuli, Njambe na Mkili walikusanyika wakishangilia kwa matawi, bendera, ngoma na mganda, ambao Nyasa ndio asili yake ukitokea Malawi.

Meli ilipita na kusimama vituo 12, vichache vikubwa ni pamoja na Lundu, Nsungu, Ndumbi, Manda, Lupingu, Nsisi, Libondo, Lumbila, Matema, Itungi na Kiwira Kyela bandarini. Baada ya kuvuka kituo cha Lundu, bahari ilichafuka, maji yakasimamisha ukuta, meli ikayumba yumba.

Hofu ikatanda kwenye meli, mawimbi yalizidi kuwa makubwa. Waliokataza safari hiyo, wakailaani safari, wakaomba wasingekuwamo kwenye msafara au wasingekuja kwa meli isipokuwa wangezunguka kwa barabara kutoka Nyasa hadi Kyela umbali wa kilometa 600 hivi. Hofu iliongezeka kadiri mawimbi yalivyokuwa yakiinua meli na kutua chini.

Wenye kuapa waliapa kutorudia safari za majini. Wengine walijifariji kwamba siku ya kufa hata ukifichana chini ya uvungu wa kitanda utakufa tu, hivyo kama imeandikwa kufa kwa meli kupinduka basi, hiyo ndiyo siku yake. Meli ikayumba, watu wakayumba yumba, wakapepesuka na kujishikilia kwenye kuta za meli, nguzo na kujishika kwa wengine.

Wengine wakajilaza sakafuni, wakihofu kuanguka, kutokana na upepo kuwa mkali. Wenye hofu zaidi wakawa wakilalama, wakijifionya na kujiuliza kama safari hiyo itakuwa salama, kwani hata nusu ya safari ilikuwa bado.Wakahofu kwamba hicho ndicho kifo alichowachaguliwa Mungu.

Kazi nzuri ya Nahodha, Tomas Faya ilisaidia kupunguza hofu, kutokana na umahiri wake wa kukata mawimbi na kurekebisha vipimo na mwendo ili kuyadhibiti. Wakati Faya akiendelea kukata mawimbi, manahodha wengine walikuwa kati yetu wakitufariji na kutuelekeza namna ya kuvaa makoti ya kuogelea ili kama ikitokea zahama au tufani basi tujiokoe kwa kuyavaa.

Hofu ya wasafiri wengi wakiwamo wa msafara wa Kinana ilitokana na hasa meli yenyewe kuwa kuu kuu, ambayo ilianza kutumika miaka 41 hivi iliyopita, hali yake na muundo wake, ulitisha zaidi.

Abiria Juma Haule, na wengine wenye uzoefu wa mawimbi makubwa, walijaribu kuwashawishi waandishi wa habari kwamba hilo ni wimbi ‘cha mtoto’ yaani dogo walidhani wanawadanganya.

Wengi walihangaika kwa kutembea huku na kule ili mradi muda huo wa zahama upite. Kuyumba kwa meli hiyo, kulitokana na kupita kwenye mkondo wa maji ya mto Ruhuhu yanayoingia ziwani na kutengeneza nguvu kubwa inayosababisha kuyumba kwa meli na mawimbi makubwa kutengenezwa.

Kitambo, hali ya hewa ilibadilika mawimbi yakapungua ukubwa na unene, meli ikaendelea kugongwa na mawimbi madogo, ndipo hofu ya msafara wa Katibu Kinana ikatulia, wakakaa kitako kupata chakula na kunywa.

Licha ya kunywa na kula, bado kwa umoja wao walikesha wamekaa, na kutokana na uchache wa magodoro, tulilala kwa zamu kwa kupokezana. Hakuna mtu aliyebahatika kulala usiku wote, usiku kati yetu aliamushwa kwenda kukesha na mwingine alale.

Abiria wengine, walijaa eneo la kati, chini na wengine wakaa mahali inapowekwa mizigo na kulala juu yake, wakishangaa msafara wa Kinana wanajishughulisha ama kupiga picha, kuandika matukio na kazi nyingine nyingi. Alfajiri ilipofika, kila mtu alishangilia kutokana na hofu ya kusafiri kwenye maji na meli iliyochoka na yenye hali duni na isiyo na uhakika wa kufika. Hiyo ilitokana na kusikia kwamba imetoka matengenezo siku chache zilizopita.

Saa tano hivi, tuliingia Kyela, tukiwa salama ndani ya Mv Songea, lakini wengine wakiapa kutosafari majini tena na wengine wakishangilia ushujaa wa Kinana kutaka tusafiri na meli, kitendo kilichoonesha kujishusha kulingana na watu wa kawaida.

Kwa sasa Mv Songea ndiyo meli pekee inayofanya safari ikati ya Mbambabay, Nyasa na Itungi sasa haitumiki sababu ya kujaa mchanga na majani kufunika, imehamishiwa Kiwira, wilayani Kyela.

Meli hiyo ina uwezo wa kuchukua abiria 200 na watendaji 13 pamoja na mizigo isiyozidi tani 200, inafanya safari mbili kwa wiki, Jumapili na Alhamisi kwenda Kyela.

Meli hiyo haikuundwa kwa ajili ya abiria, hayati Baba waTaifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikwenda kuomba meli Yugoslavia, mara baada ya Rais wa zamani wa Malawi, Dk Kamuzu Banda kuzuia meli yake kuja upande wa Tanzania. Nyerere alipata meli tatu mwaka 1974, ambazo mbili kati yake, ni Mv Songea haikuwa ya abiria bali ilikuwa ya kusafirisha mizigo. Ilisafirisha mizigo hadi mwaka 1989, ambapo kutokana na meli moja kugonga mwamba Kikombo na kuzama.

Wakazi wa Ludewa waliitungia wimbo, meli ilipozama, wakiililia kwa kuikosa meli hiyo. Kwa bahati mbaya zaidi kituo cha Kikombo kilifungwa kutokana na kuzama meli hiyo mahali hapo baada ya kugonga mwamba.

Ikabaki Mv Iringa pekee ambayo ilizidiwa kutokana na mizigo na abiria kuwa wengi, ndipo Shirika la Reli Tanzania, kabla ya kuanzishwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kuanzishwa likaibadili meli hiyo na kuwa ya abiria.

Kilichofanyika ni kutengeneza mabenchi ya kukalia, eneo la kati la meli, ndilo hasa yamebandikwa mabenchi na mengine yamebandikwa ukutani na mengine yameungwa ungwa maeneo ambayo yasingetakiwa kuwa nayo. Kutokana na kuwa yuko Yugoslavi iliundwa kwa ajili ya mizigo, upande mmoja wa eneo chini likabaki kuwa la kupikia, kulala wahudumu kati yao 13, upande mmoja abiria wa daraja la tatu wakakaa.

Kutokana na utulivu, baridi na hali ya kutokuwa na bughudha hapo panaitwa saluni, wakimaanisha mtu anayetaka kufanya kazi, kupumzika bila utulivu hata wa mawimbi ya meli akae huko.

Meli hiyo ina madaraja mawili tu la tatu ambalo kuna maeneo mawili ya chini na kati na daraja la juu ambako wanalala manahodha na meneja pamoja na watendaji. Kutokana na hali mbaya ya meli hiyo, Rais Jakaya Kikwete ameahidi kununua meli kubwa ya kuwasaidia wananchi wa Kyela hadi Nyasa.

Waziri wa Uchukuzi, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amewahakikishia wananchi wanaotumia ziwa hilo kwamba meli ya ahadi ya Rais inatengenezwa Korea Kusini na meli nyingine inatengenezwa kwa msaada wa Serikali ya Denmark.

Kutengenezwa kwa meli mbili hizo kubwa na zenye kasi, kutaifupisha safari haitakuwa tena ya saa 26, bali inaweza kuwa ya saa 16 au hata pungufu.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi