loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sarah Ramadhani: Ndoto za kushiriki Madola zayeyuka

Mbali na Ramadhani baadhi ya wanariadha wa kike wanaotesa katika medani hiyo hapa nchini ni pamoja na Jacline Sekilu, Zakia Mrisho, Mary Naali na Fabiola. Mwingine aliyewahi kutamba ni Restituta Joseph ambaye kwa sasa hafanyi vizuri kutokana na umri kukimbia.

Kutamba kwa Sarah:

Sarah amekuwa akifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo yale yanayofanyika kila mwaka nchini Brazil. Mwanariadha huyo amekuwa akitamba kuanzia mbio za kilometa 10, nusu marathoni na hata wakati mwingine marathoni kamili, ambapo amekuwa akifanya vizuri.

Tanzania imekuwa na tatizo la kuwa na wanariadha wachache wa kike licha ya kuwa na vipaji vingi, ambavyo vimeshindwa kuendelezwa kabisa. Katika mbio za hivi karibuni kabisa, Sarah alishiriki mbio za kilometa 10, ambapo alishika nafasi ya tatu nyuma ya Sekilu aliyekuwa wa pili na Mkenya Nancy aliibuka wa kwanza.

Baada ya Tanzania kunyanyaswa na Kenya katika mbio za nusu marathoni za Kilimanjaro, Sarah Ramadhani mwaka juzi aliitoa nchi kimasomaso baada ya kushika nafasi ya kwanza kwa kutumia saa 1:13.05 na kuwabwaga hata Wakenya. Mwaka huu, Mtanzania mwingine Sakilu aliibuka wa kwanza katika mbio hizo za Kilimanjaro Marathoni, ambazo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, alikuwa mgeni rasmi.

Kuanza riadha:

Sarah anasema alianza kukimbia riadha mwaka 2003 akiwa katika Klabu ya Zacharia Gwandu ya Team 100, ambako anakiri kuwa ndiko kuliibua na kukiendeleza kipaji chake. Anasema katika klabu hiyo akiwa chipukizi kabisa katika mchezo huo alikutana na wanariadha kama akina Mrisho, Sekilu, Neema Deemay, Zaituni Jumanne na Farida Gusi.

Anasema wanariadha hao aliowakuta ndio walikuwa wakimpa moyo hadi kumfanya hadi leo anaendelea kutimua mbio na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi katika mashindano mbalimbali.

Michezo ya Jumuiya ya Madola:

Ramadhani ni mmoja wa wanariadha ambao wamo katika orodha ya awali ya wachezaji wa Tanzania watakaoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 3, mwaka huu. Anasema katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola atashiriki katika mchezo wa mbio za meta 10,000, ambapo anatarajia kutoa upinzani kwa nyota akiwemo Dibaba wa Ethiopia.

Alipoulizwa kama anahofia kukimbia pamoja na akina Dibaba, Sarah Ramadhani huku akicheka anasema: “Aaah huko ndiko nitapata kipimo cha uhakika kwa kukimbia na akina Dibaba pamoja na wakali wengine.” Mwanariadha huyu tayari amewahi kushiriki mbio mbalimbali kubwa zikiwemo zile za nchini Italia, China, Brazil, Ufaransa na kwingineko.

Mwanariadha huyo mwenye mtoto mmoja wa kiume anayejulikana kwa jina la Aggrey Amon aliyezaa na mwanariadha Amani Ngoka, anasema kuwa mumewe amekuwa akimtia moyo sana katika shughuli yake hiyo ya riadha.

Kuondolewa Madola:

Wakati naandika makala haya zikaibuka taarifa kuwa Sarah amefungiwa miaka miwili na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF) kushiriki mbio zozote baada ya kubainika kutumia dawa za kusisimua misuli. Dawa hizo zilizopigwa marufuku michezoni katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa maarufu sana kwa wanamichezo licha ya kupigwa vita kila kona ya dunia.

Hata hivyo, pamoja na Watanzania wengi kutosikika kutumia dawa hizo, lakini ukweli ni kwamba wanariadha wetu wameanza kujiingiza katika shughuli hizo ili kusaka ushindi. Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui alisema kumekuwa na wimbi la wanariadha wanaotumia dawa hizo ingawa hakuwa tayari kuwataja kwa majina.

Pia, Nyambui alikiri kuwa Ramadhani kufungiwa miaka miwili kwa sababu ya dawa hizo ingawa alisema ana haki ya kukata rufaa endapo ataona hajatendewa haki. Hata hivyo, Nyambui alisema kuwa Ramadhani walipozungumza naye alisema hana mpango wa kukata rufaa na alikiri kutumia dawa hizo, lakini aliambiwa kuwa ni za kutibu malaria.

Nyambui alisema wana mpango wa kukutana na daktari na kuiandikia barua IAAF kuieleza kinagaubaga kuhusu suala hilo, kwani mwanariadha huyo alitumia dawa hizo baada ya meneja wake wa Brazil kumdanganya na yeye hajui lugha. Mbali na Michezo ya Jumuiya ya Madola, Sarah Ramadhani haruhusiwi kushiriki mashindano yoyote ya ndani na nje ya nchi na akikiuka kifungo hicho, anaweza kufungiwa maisha.

IAAF kuanzia mwakani itafanya mabadiliko ya adhabu hiyo, ambapo sasa mwanariadha atakayebainika kutumia dawa hizo atakuwa akifungiwa kwa miaka minne na akirudia tena, atafungiwa maisha.

Alisema kufungiwa kwa Ramadhani ni pigo kubwa kwa timu ya Tanzania inayotarajia kushiriki Michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola baada ya sasa kubaki na mwanariadha mmoja tu wakike, Jackline Sekilu. Sekilu na Ramadhani ndio wanariadha wa kike nchini waliokuwa wakitamba katika mbio za meta 5,000; 10,000 na hata nusu marathoni kwa upande wa wanawake.

Nyambui alisema sasa timu ya Tanzania itakuwa na mwanariadha mmoja tu wa kike katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 3 mwaka huu.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi