loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sefue: Ripoti ya IPTL haijakamilika

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema si sahihi kuishinikiza ofisi ya CAG itoe ripoti hiyo, hivyo CAG apewe muda aifanye kazi hiyo kwa uhuru, weledi, na viwango.

Balozi alisema jana kuwa serikali haikuyapenda mashinikizo kuhusu ripoti hiyo na kwamba ofisi ya CAG inaamini kwamba itamaliza kazi hiyo kwa wakati, na kwamba ripoti hiyo itawasilishwa bungeni katika muda uliopangwa kwenye ratiba ya Bunge.

“Sikupenda kwa kweli hayo mashinikizo kwa CAG…kwa hiyo si vizuri kuwapa mashinikizo ya kisiasa au mashinikizo ya washirika wa maendeleo,” alisema Balozi Sefue baada ya gazeti hili kuhitaji ufafanuzi wake kuhusu masuala kadhaa yenye maslahi kwa taifa.

“Tumewapa kazi, ni vizuri tuwape muda wa kutosha ili waifanye kazi yao kwa weledi na watoe ripoti ambayo wao wenyewe wanaridhika kuwa imefikia viwango vyao, kwa hiyo haikuwa sahihi kuwapa mashinikizo ya kisiasa au mashirika ya washirika wa maendeleo kuwashinikiza watoe ripoti kabla haijawa tayari,” alisema. “Kwa sababu ukiwashinikiza unataka wafanye kazi kwa kuharakisha bila kuzingatia utaalamu,” alisema.

Oktoba 14 ofisi ya CAG ilisema ukaguzi huo maalum, unaofahamika kama Ukaguzi wa IPTL, unaendelea unaongozwa na Hadidu za Rejea (ToR) zilizotolewa na kisha kuridhiwa na Ofisi ya Bunge na Wizara ya Nishati na Madini.

“Ukaguzi huu unalenga kufanya uchunguzi wa kina ambao utatoa taarifa kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye akaunti maalumu ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusu ukaguzi huo,” ilisema taarifa hiyo kwa umma.

Kuhusu mmiliki wa IPTL, Balozi Sefue alisema; “Kwa maoni yangu naamini kwamba, ambao wanaweza kusema nani mmiliki halali wa IPTL ni Mahakama.”

Alipoulizwa kuhusu shinikizo la wabunge kutaka ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya kuchunguza unaodaiwa kuwa ni wizi wa fedha katika akaunti ya Escrow, kiongozi huyo wa Serikali alisema, jambo hilo lazima lifuate utaratibu.

“Ninavyojua mimi Takukuru kapewa kazi ya kuchunguza, kama tunavyojua hii kazi ya kuchunguza mambo ya Escrow, wanapoona kwamba kuna mambo ya hovyo kama vile rushwa au malipo ambayo hayakufuata utaratibu na upo ushahidi wanakwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na yeye akiona kwamba ushahidi uliopatikana unatosha kwenda mahakamani, basi Takukuru wanakwenda mahakamani kwa kushirikiana na DPP,” alisema.

Wabunge juzi walifahamishwa kuwa ripoti ya Takukuru, kuhusu kuchukuliwa kunakodaiwa isivyo halali kwa fedha katika Akaunti ya Escrow, haitajadiliwa bungeni.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akijibu Mwongozo wa wabunge kuhusu kujadiliwa kwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kuhusu sakata hilo.

Mwongozo wa awali kwa suala hilo, uliombwa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema) aliyehoji kutoonekana kwa ripoti ya Takukuru katika ratiba ya vikao vya Bunge na badala yake kuonekana ripoti ya CAG.

Ratiba mpya ya Bunge iliyotolewa juzi, inaonesha kuwa ripoti ya CAG kuhusu sakata hilo la fedha katika akaunti ya Escrow, itawasilishwa katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), Novemba 26, mwaka huu.

Akijibu Mwongozo huo wa Wenje na baadaye wa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kuhusu kwa nini ripoti ya Takukuru haitaletwa kujadiliwa bungeni, Ndugai alisema kwa mujibu wa sheria, Takukuru hawapaswi kuwasilisha ripoti yao bungeni.

“Waheshimiwa wabunge, Takukuru wao wakimaliza kazi yao, na wakibaini kuna makosa ya jinai, inachukua hatua moja kwa moja kwa kuwasiliana na DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka) na kuwafikisha wahusika mahakamani,” alisisitiza Ndugai.

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi