loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serengeti Boys, Taifa Stars hakuna kisichowezekana

Serengeti Boys itakuwa jijini Johannesburg kuikabili Afrika Kusini (Amajimbos) katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Vijana Afrika.

Katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya kutofungana, hivyo ushindi leo utaivusha Serengeti Boys katika raundi inayofuata ya michuano hiyo.

Kwa ujumla, kutokana na kiwango kilichooneshwa na timu hiyo inayofundishwa na Hababuu Ali Omar, hakuna shaka kuwa uwezo wa kuishinda Afrika Kusini ni mkubwa, na hasa kama wachezaji watatulia na kucheza zaidi ya walivyocheza mechi ya kwanza.

Hatuna sababu ya kutilia shaka uwezo wa timu hiyo, hivyo tunaamini wakifuata vyema maelekezo ya mwalimu wao, wataibuka na ushindi leo na kuwapa raha Watanzania wapenzi wa michezo nchini.

Wakati Serengeti Boys itakapokuwa imemaliza kazi yake leo jioni, kaka zao Taifa Stars watakuwa na kazi nzito kesho mjini Maputo nchini Msumbiji.

Stars iko Maputo kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2015 dhidi ya wenyeji, Msumbiji ‘Black Mambas.’

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili inafanyika kesho huku Stars ikiwa imelazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza Julai 20, mwaka huu.

Kwa msingi huo, Taifa Stars itaingia uwanjani ikifahamu kuwa ni ushindi tu utakaoihakikishia kusonga mbele katika hatua ya mwisho ya makundi kupata timu za kwenda Morocco mwakani.

Kama ilivyo kwa Serengeti Boys, Stars imeandaliwa vizuri ikiwamo kukaa kambini jijini Mbeya na kisha kupiga kambi ya siku mbili nchini Afrika Kusini.

Chini ya udhamini wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Stars iko katika hali nzuri, hivyo watakuwa na kazi moja ya kuhakikisha wanapata ushindi kesho.

Kwa jinsi timu ilivyocheza katika mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ni imani yetu kwamba wanao uwezo wa kupata ushindi ugenini na hilo linawezekana kama kila mmoja akitimiza wajibu wake uwanjani kulingana na maelekezo ya kocha.

Ni imani yetu wachezaji wa Taifa Stars watatumia maelekezo ya kocha wao vizuri na kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kuwapa furaha Watanzania.

Hakuna shaka kwa nini Taifa Stars isipate ushindi ugenini kwa sababu katika soka, hakuna mahali ambako ushindi haupatikani kama timu itakuwa imejiandaa vizuri na kutumia nafasi zake vizuri uwanjani kufunga mabao.

Tunazitakia kila la heri Serengeti Boys na Taifa Stars, tukiamini kwamba zinao uwezo mkubwa wa kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi