loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali inastahili pongezi kwa kuvuka lengo usambazaji umeme

Kwamba, iliazimiwa iwe imesambaza umeme kwa asilimia 30, lakini tayari imeshasambaza kwa asilimia 36, huku Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini nchini, Profesa Sospeter Muhongo akitamba kuwa, kufikia mwaka kesho ambao utakuwa mwisho wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010, wana jeuri ya kusambaza hadi asilimia 50!

Kwa hili, sisi wa HabariLeo tunapenda kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa iliyofanya ya kutekeleza ahadi za chama tawala ahadi ambazo ilizitoa katika Ilani yake ya uchaguzi wakati inaomba ridhaa ya wananchi ya kupewa fursa nyingine ya kuiongoza nchi mwaka 2010.

Kupongeza huko tunakufanya kwa kuamini msemo wa Kiswahili wa zamani kabisa msemo ambao mantiki yake ni kuuweka huru moyo na maarifa ya maisha, “Mnyonge Mnyongeni, Lakini Haki yake Mpeni”.

Msemo huu wa Kiswahili wenye maana kubwa katika maisha ya kila siku, msemo ambao maana yake ni pana zaidi hasa katika jamii ambayo ustaarabu wa kushukuru ni ada ya kila siku, ndio unatupa nafasi ya kusema kwamba heko Serikali kwa kutekeleza ilani ya chama tawala.

Tunasema hivyo kwa kuwa katika juhudi za kuleta maendeleo suala la upatikanaji wa nishati ni muhimu hasa nishati rafiki kwa mazingira na usambazaji huu wa kasi unaonesha nia ya Serikali kuwawezesha wananchi wake kiuchumi na kuboresha mazingira.

Kutokana na kauli ya Serikali kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba usambazaji wa umeme unaweza kufikia asilimia 50 ya wananchi wote wa Tanzania ifikapo mwakani kwa sababu umeme sasa unasambazwa kwa kasi isiyokuwa ya kawaida, Watanzania wana haki ya kujivunia Serikali yao na kuipongeza kwa kuhakikisha inatekeleza ahadi.

Kwa maneno mengine, kauli ya kuvuka lengo na kutaka kupangiwa lengo lingine ya Profesa Muhongo aliyoitoa mbele ya Rais Jakaya Kikwete mjini Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma anakoendelea na ziara yake, inatakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kwamba juhudi za Serikali za Matokeo Makubwa Sasa zinatoa tija zaidi kwa wananchi waishio vijijini.

Ingawa tunasema mnyonge mnyongeni na haki yake mpeni, tunaishauri Serikali kukaza uzi na kutobweteka na mafanikio hayo ili yawe endelevu na kuwezesha Watanzania kuona dhamira safi ya Chama Tawala katika kuhudumia wananchi wake katika suala la umeme.

Kwa kuunganisha kwa kasi wananchi kwa umeme, tena kwa bei nafuu ya Sh 27,000 tu ambayo kila mtu anaweza kuimudu baada ya kuuza majogoo mawili au matatu tu, tunaamini Watanzania watakuwa wa kisasa zaidi, wakiishi kisasa, tofauti na staili ya kuendesha maisha sambamba na kuharibu mazingira kutokana na kugeuza miti na kuni kama vyanzo vya nishati.

Ndiyo maana tunasisitiza kuwa, kwa hili Serikali inastahili pongezi, lakini pia utendaji huu wa Wizara ya Nishati na Madini utumike kama kioo kwa wizara nyingine zinazopaswa kufanya kazi usiku na mchana katika kutimiza ndoto za Watanzania za kuona nchi yao inakuwa na ustawi wa hali ya juu wa maisha na kiuchumi kwa ujumla.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi