loader
Picha

Serikali ipongezwe upandikizaji figo

Baadhi ya magonjwa ambayo yalionekana kuwa ni vigumu kuyatibu hapa nchini, ni yale ya moyo, ini na upandikizaji wake pamoja na figo.

Lakini kwa jitihada za serikali tayari kumeanzishwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), pamoja na uboreshaji wa vifaa na wataalamu kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kupata utaalamu zaidi kwa magonjwa yale yaliyoonekana kuwa ni magumu, ambayo ilibidi wagonjwa wasafirishwe hadi India ama nchi nyingine.

Habari njema zaidi ni kwamba, mwaka jana Novemba mgonjwa wa kwanza wa figo aliweza kupandikizwa figo hapa nchini katika hospitali ya Muhimbili kwa kusaidiana na wataalamu kutoka nchini India, hali yake hivi sasa inaendelea vizuri, kisha mgonjwa wa pili alifanyiwa upasuaji na kupandikizwa figo Machi mwaka huu katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma.

Kisha wiki iliyopita, wagonjwa wanne kati ya watano waliokuwa wameandaliwa walifanyiwa upasuaji na kupandikizwa figo katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jambo hilo ni faraja kubwa sana kwa Watanzania kwa sababu, wapo wagonjwa wengi wenye shida ya figo na ambao walikuwa hawana uwezo wa kwenda nje ya nchi kutibu, ama serikali haikuweza kuwapeleka wote kwa mara moja, hivyo kwa huduma hiyo kuanza kutolewa hapa nchini itasaidia kupunguza idadi ya vifo ambavyo vingeweza kutokea kwa kushindwa kupata tiba hiyo.

Si hivyo tu, bali Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema, kuanzia sasa kwa kila mwezi wagonjwa watano watakuwa wakifanyiwa upasuaji wa kupandikizwa figo, kwa kuwa tayari wagonjwa 60 wameshapimwa na kuonekana wana haja ya kupandikizwa figo idadi ambayo inaongezeka kila mara.

Profesa Museru pia amesema, baada ya mwaka mmoja ama moja na nusu jengo jipya litakuwa limeshakamilika ambalo mbali na huduma nyingine, kutakuwa na kitengo cha magonjwa ya figo, na kukamilika kwa jengo hilo, kutawezesha mgonjwa moja kufanyiwa upasuaji wa kupandikizwa figo kila siku badala ya watano ambao sasa imeanza kufanya.

Hivi sasa wagonjwa zaidi ya 200 wa figo wanatibiwa hospitalini hapo na 800 wanasafisha damu nchini.

Hali hii inaonesha kuwa tatizo ni kubwa hivyo wananchi wanashauriwa kubadili tabia ili wasipatwe na tatizo hilo na pale wanapobaini kuwa wanalo, wawahi hospitalini kwa vipimo zaidi.

Kwa upande wa hospitali ya Benjamini Mkapa imekuwa ikishirikiana na madaktari bingwa wa Tokushukai Medical Group, kutoka nchini Japan katika upasuaji na upandikizaji wa figo pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu hapa nchini.

Katika hospitali hiyo wataalamu hao kutoka Japan watakuwa wakija nchini mara nne kila mwaka kwa ajili ya upasuaji huo na kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu kwa kipindi cha miaka minne. Hivyo matarajio ni kwamba kwa mwaka wanatarajia wagonjwa 12 hadi 20 watafanyiwa upasuaji huo.

Kwa mkoa wa Dodoma, huduma hiyo imekuwa msaada mkubwa sana kwa wagonjwa wenye shida ya magonjwa ya figo Kanda ya Kati na majirani kwani kabla ya hapo iliwalazimu wagonjwa kusafiri umbali wa kilometa 600 mpaka 800 kuitafuta huduma hiyo Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo kuna kila sababu ya kuipongeza serikali kwa kuwa imewezesha kuokoa kati ya Sh milioni 80 hadi 100 kwa mgonjwa mmoja kwenda nje ya nchi.

MSIMU wa sikukuu za mwisho wa mwaka umewadia. Siku ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi