loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Serikali: Msivamie maeneo ya jeshi

Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Job Masima wakati akifunga maadhimisho ya 32 ya Siku ya Kamandi ya Anga yaliyofanyika jijini hapa kwenye uwanja wa ndege.

Maadhimisho hayo ambayo yalikwenda sambamba na maonesho ya zana za kijeshi yamefanyika kwa muda wa siku sita ambapo Masima anasema yametoa fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuwa karibu na Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania(JWTZ).

Alisema maonesho hayo yalikuwa na lengo la kuwaonesha Watanzania ili waweze kujua kamandi hiyo inavyofanya kazi na kuonesha utendaji wa kazi wa Jeshi la Anga kwa ujumla. Masima alisema uwepo wa kamandi hizo unawadhihirishia Watanzania kwamba wapo salama katika maeneo mbalimbali ya anga hapa nchini.

“Hii ni fursa nzuri kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla kutambua umuhimu wa uwepo wa Jeshi la Anga hapa nchini na kutambua utendaji wake wa kazi katika kusaidia Taifa la Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo alisema baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya jeshi bila kujua yametengwa kwa sababu maalumu.

“Niwaombe wakazi wa Jiji hili kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya jeshi mkoani hapa, na mtambue kwamba hayakuachwa kwa ajili ya kujifurahisha bali yapo kwa sababu maalumu,” alisema na kuwaomba wananchi kushirikiana na jeshi hilo.

Alisema maonesho hayo ya Kamanda ya Anga yameinua ari kwa vijana kuipenda na kuitumikia nchi yao katika suala zima la ulinzi. Pia aliwataka vijana kusoma masomo ya sayansi ili waweze kuwa marubani wazuri kama wale waliokuwa wakifanya maonesho uwanjani hapo na kwamba baada ya maonesho hayo wananchi wametambua hawawezi kutenganishwa na jeshi hivyo watoe ushirikiano.

Katika mahojiano na Mkuu wa Majeshi (mstaafu), Meja Jenerali Robert Mboma kuhusu maadhimisho hayo alisema Kamandi ya Anga imekuwa na maendeleo makubwa.

foto
Mwandishi: Grace Chilongola, Mwanza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi