loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shule nyingine ziige Sekondari ya Mwadui

Uamuzi wa uongozi wa shule hiyo, ambayo inamilikiwa na Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), hauna budi kutekelezwa kwa vitendo ili kurudisha heshima, nidhamu na maadili ya watoto. Lakini, pia ni vema na shule nyingine za sekondari na misingi, zinazomilikiwa na taasisi binafsi na Serikali, kuiga mfano huo.

Kuwepo kwa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), umeifanya dunia kuwa kama kijiji, tamaduni zimeingiliana kupitia kiganjani mwa yeyote mwenye kuweza kumiliki simu ya mkononi na maadili ya Mwafrika, yamekuwa shakani, hasa kutokana na kizazi hiki kuiga bila kujali athari za tamaduni za nchi za Ulaya na Marekani.

Tunasema ni vema shule nyingine, ziige shule hiyo ya Sekondari ya Mwadui, kwa kuwa muda mwingi wa mtoto anakuwa shuleni, iwe shule ya kutwa au bweni, ikilinganishwa na muda wa mtoto anapokuwa na wazazi wake.

Ni kutokana na ukweli huo, watoto wengi wanahitaji malezi kwa kiasi kikubwa kupitia kwa walimu wao, zaidi ya wazazi ambao wanakaa nao muda mfupi.

Hata hivyo, wazazi nao wa kizazi hiki, wamekuwa ‘bize’ sana na kutafuta ‘maisha bora ya familia’, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha za kuhimili maisha, inapatikana tena kwa kiasi cha kutosha, hivyo kuwafanya wasiwe na muda wa kufuatilia tabia za watoto wao, hasa wale wa kutwa kwa kuwa wa bweni wanakuwa mbali nao.

Kwa kuwa watoto wanaachwa kufanya maamuzi, wameangukia katika mikono ya mageuzi ya mawasiliano, ambayo hayana mipaka katika kutoa taarifa zisizojali umri, rika na tamaduni za jamii moja kwenda nyingine.

Kutokana na hali hiyo, watoto wa kiume wanaacha viuno wazi wakiita milegezo, kwa kuwaiga wale wasanii wa nchi za Ulaya na Marekani na wananyoa mitindo ya nywele ya kihuni, eti wanakwenda na wakati.

Watoto wa kike wanaacha wazi viungo nyeti vya mwili, wanajipaka vipodozi kuchubua miili yao, kusaka weupe na kuvaa viatu virefu ili wafanane na wazungu na kuwa na simu kubwa, zenye kufundisha kila aina ya uchafu.

Serikali wakati inaangalia jinsi ya kurekebisha hali hii, ni vema jamii yote inayohusika moja kwa moja katika malezi ya watoto, kuliona hili na kurudi kwenye misingi ya maadili.

Kama shule zitaweka misimamo, watoto wakapewa adhabu ikiwa ni pamoja na kuwarudisha nyumbani wale wakaidi, tunaamini katika malezi yale ambayo wao wanayaita ya kizamani, yanayoweza kurudisha heshima ya mtoto wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Hatukatai mabadiliko. Lakini, tunasisitiza hatuwezi kuacha mabadiliko haya, kuondoa maadili tuliyorithi kutoka kwa mababu zetu na kuingiza tamaduni za wenzetu, ambao kwao ni kitu cha kawaida.

Tuungane na Shule ya Sekondari ya Mwadui, kurudisha nidhamu ya watoto, kwani hawa ndio taifa la leo na kesho. Kuwaacha jinsi walivyo sasa, ni kutengeneza bomu, ambalo litalipuka muda si mrefu ujao.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi