loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SHULE ZINAPOELEKEA KUFUNGWA...Muda wa kupambana na ukeketaji ni sasa

Safari yangu ilitokana na kuwepo kwa taarifa kwamba wiki chache zilizopita, yaani mwezi Desemba mwaka 2010 wakati shule zilipokuwa zimefungwa, ukeketaji ulifanyika wilayani humo kwa uwazi na hata mbele ya vyombo vya dola!

Vyombo vya habari vilionesha watu wakiandamana kwa makundi, wakipita mbele ya vituo vya polisi, na wengine wakitundika bendera kwenye miti mirefu katika sherehe ‘kubwa’ ya ukeketaji. Ndio, ukeketaji kule Tarime ni sherehe kwa jamii, watu wanasafiri kutoka mbali kuja kusherehekea ingawa ni mateso na ulemavu kwa mabinti.

Wakati nikiwa maeneo ya Nyamongo, nikiona mabinti wadogo wakiwa bado jandoni, nililalamikiwa na baadi ya watu wanaopinga ukeketaji kwamba vyombo vya habari, vyombo vya dola na wanaharakati hufika wilayani hapo baada ya matukio ya ukeketaji kufanyika.

“Nyinyi waandishi, wanaharakati na wanasheria mnapaswa kuja Tarime wakati wa maandalizi ya ukeketaji, hususan mwisho wa mwaka shule zinapokuwa zimefungwa ili kutibua mambo kuliko mnavyokuja kufuatilia matokeo wakati makosa haya ya jinai yameshafanyika,” aliniambia mkazi mmoja wa Nyamongo, Bahati Matiku, ambaye ni mpinzani mkubwa wa mila hiyo.

Matiku anaamini kwamba vita dhidi ya ukeketaji nchini inapaswa wakati wote na hususan miezi hii inayoelekea kwenye ufungaji wa mashule kwa sababu idadi kubwa ya wanaokeketwa ni mabinti wadogo wanaosoma shule za msingi na wachache sekondari. Matiku na wengine nilioongea nao, pengine walisema kweli kwani nahisi makala nyingi za kupinga mila hii mbaya ya ukeketaji zimekuwa zikiandikwa baada ya matukio ya ukeketaji kufanyika.

Sina hakika pia kama wanaharakati wameendeleza juhudi katika wilaya korofi zinazoendeleza mila hii potofu wakati wa maandalizi na kwa upande wa serikali sina hakika pia kama mengi yamefanyika kuanzia elimu hadi matumizi ya sheria katika kuhakikisha kwamba ukeketaji unakoma hapa Tanzania, hususan katika vipindi vya maandalizi kama muda huu.

Wakati niliambiwa kulikuwa na ngariba mmoja amefungwa pale Tarime mwaka 2010 huku kesi moja ikiwa inaendelea pia mahakamani wakati huo, Mwandishi Anthony Mayunga wa Serengeti aliniambia hajawahi kusikia kesi yoyote ya ukeketeji wilayani humo ingawa ukeketaji upo kila mwaka.

Lakini Yusuph Marare, mkazi wa Musoma Mjini ambaye amekuwa akifanya shughuli za ulimaji wa barabara katika baadhi ya vijiji vya Tarime alinijibu: “Ukeketaji ni tukio kubwa sana. Huwa ni maandamano ya watu wengi wakiwemo ndugu na waalikwa hata kutoka nje ya Tarime. Ni sherehe inayoandamana na kula na kunywa na mifugo mingi kuchinjwa.

Watu wanajaa ndani ya kilometa hata mbili... Katika wingi huo huku kituo cha polisi kikiwa na askari wasiozidi 10 watawafanya nini hawa. Na kwa kweli akiwepo askari wa kutaka kutibua jambo hilo, basi hatakaa salama, lazima ahame, vinginevyo ajiandae kugechwa (kukatwa mapanga). Lakini, kama nilivyodokeza hapo juu, sherehe hizi za kula na kunywa ni mateso kwa wasichana.

Mateso wanayoyapata mabinti hawa ni mengi kuanzia kwenye maumivu makali, kuuguza na wengine hufariki dunia na mbaya zaidi, binti anayefariki dunia katika tendo la ukeketaji maiti yake hutupwa mithili ya mnyama, kwa maana kwamba hazikwi kutokana na imani nyingine potofu kwamba maiti yake ni mkosi.

Yaani wakati tafiti za kidaktari zinaonesha kwamba vifo kwenye ukeketaji vinatokana na mshituko (shock) kwa sababu ya kuvuja damu nyingi, ama msichana kupata maambukizi (infections) kutokana na tendo hilo kufanywa kwa kutumia vifaa duni tena bila ganzi, bado jamii imeendelea kuamini katika suala la mila, mizimu na uchawi kuwa ndio sababu ya vifo.

Lucy Lazack Mrimi (aliyekeketwa mwaka 1992) aliniambia kwamba alikuwa anajifungua kwa matatizo na wauguzi wakamwambia kwamba ni sababu ya kukeketwa.

“Unajua niliwahi kuishi Kibaha (mkoani Pwani) ambako nilipata ujauzito wangu wa kwanza. Nilipata taabu sana wakati wa kujifungua na wauguzi katika hospitali ya Tumbi walinisimanga sana baada ya kugundua kwamba nimekeketwa... Nilipopata ujauzito wa pili (bado nikiwa mbali na Tarime), nilishikwa tena na kiwewe. Yaani wakati nahisi sijui kama nitajifungua salama nikawa ninawaza namna manesi watakavyonisema kutokana na kukeketwa…” Lucy anakiri pia kwamba kwa kukeketwa imempunguzia sana hamu ya kufanya tendo la ndoa na mumewe.

“Yaani sisi tuliokeketwa hadi ufike kilele inabidi mwanaume akuandae muda mrefu sana,” anasema. Kuhusu maumivu wakati wa kukeketwa, Lucy aliniambia kwamba ingawa alikeketwa tangu mwaka 1992, lakini hadi leo akikumbuka maumivu aliyoyapata anawasikitikia sana watoto wa kike wanaoendelea kukeketwa. Kuhusu maumivu wakati wa hedhi, Lucy anakiri kwamba wanawake wengi waliokeketwa hulalamikia maumivu makali wakati wa hedhi.

“Kwa wanaokeketwa wakiwa tayari wamevunja ungo, wapo wanaogundua kwamba walikuwa hawasikii maumivu ama kama yapo yalikuwa madogo lakini yaliongezeka baada ya kukeketwa,” anasema akiongeza kwamba hata yeye hupata maumivu lakini si makubwa sana.

Lakini Bahati Matiku anasema kwamba watu wengi hawajui madhara ya ukeketeaji zaidi ya maumivu wanayopata mabinti. “Ingawa wapo wanaojifungua salama lakini wengi waliokeketwa wanajifungua kwa matatizo lakini wananchi hawaelezwi kinachotokea hospitalini ili wajue kwa undani tatizo la ukeketaji,” anasema Matiku.

Lucy aliniambia kwamba ukeketaji unaandamana na matatizo mengi ya kisaikolojia ambayo jamii yake imekataa kuyapa nafasi na kuwafanya wananchi wauchukie kama vile mwanamke kuwa na maumivu ya kudumu, kuchukia tendo la ndoa na kujisikia kutotoshelezwa wakati wa tendo hilo.

Binti mwingine aliyetaka jina lake lisitajwe gazetini ili kulinda ndoa yake, aliniambia kwamba aliwahi kukaa Musoma Mjini ambako alikuwa anajisikia woga kufanya tendo la ndoa na mtu asiyetoka katika jamii inayokeketa.

“Unaweza kumpenda mvulana, sasa taabu inakuwa pale mnapopanga kwenda kufanya mapenzi. Unakuwa unahofia asigundue kwamba umekeketwa na unahakikisha hakushiki sehemu za siri. Hii ni kwa sababu unahisi akikushika zile sehemu atagundua uko tofauti kama alishawashika wale ambao hawajakeketwa. Kwa hiyo unafanya lile tendo ukiwa umeshaathirika kisaikolojia. Hauwezi kufurahia sana,” alisema.

Katika utafiti nilioufanya pale Nyamongo ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na uwepo wa mgodi wa dhahabu wa North Mara, mabinti wawili wadogo waliokeketwa na walioko kwenye ndoa, waliniambia kwamba ndoa zao ziko hatarini kwa sababu waume zao ni kama wamewakimbia.

Niliwekwa wazi kwamba wanaume wakishakutana na wanawake wasiokeketwa, kule wanawaita ‘wasagane’, basi huwakimbia waliokeketwa. Bahati Matiku, naye alinihakikishia kwamba mwanaume akishakutana na msagane, hunogewa zaidi kuliko aliyekeketwa.

“Unajua, huko nyuma sehemu kubwa hapa tulikuwa tunaishi Wanyamongo tupu, na wanaume walikuwa hawakutani mara kwa mara na wasagane, na hivyo walikuwa wanatulia kwenye ndoa zao, lakini siku hizi vijana wote wa kiume wanajua kwamba kutembea na msagane unapata furaha zaidi kuliko mwanamke aliyekeketwa ingawa kimila wanashauriwa kuoa waliokeketwa… Kwa kweli tutake tusitake hii mila imepitwa na wakati,” anasema Matiku.

Anasema uzoefu wake pia unaonesha kuwa vijana wengi wanaokwenda kutafuta maisha nje ya Tarime wakiwa tayari wameshaoa, wakishakutana na wasagane huwatelekeza kabisa wake zao. Karibu wote niliowahoji, hakuna aliyekuwa na taarifa kama kuna mtu aliyeambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi kutokana na ukeketaji, ingawa Matiku alisema tafiti zikifanywa vyema huenda hicho kikagundulika.

“Sasa hivi kila anayekeketwa hutakiwa kwenda na wembe wake mpya, lakini nina wasiwasi na yule ngariba anayewakeketa kama ananawa sawasawa kiasi cha kuweza kuwalinda wanaokeketwa na maambukizi, kwa sababu ni mtu mmoja anayekeketa watoto wengi kwa wakati mmoja,” alisema Matiku.

Zaidi ya wanawake 10 waliokeketwa niliowahoji, walikiri kufika kileleni wakati wa kujamiiana lakini kwa taabu na kwamba kama wapenzi wao si wavumilivu ‘huwaacha njiani’. Kwa mantiki hiyo, ukeketaji ni janga na muda wa kuhakikisha kwamba mipango ya uovu huo unatibuka ni sasa. Tusisubiri kuona umeshatokea ndipo tunaandika, tunakamata ama kupeleka elimu.

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi