loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Siku ya Mashujaa itumike kujenga uzalendo wa Taifa

Ni muhimu kwa sababu siku ambayo Taifa huwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania. Maadhimisho haya huambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo dua na sala maalumu kutoka kwa viongozi wa madhehebu ya dini wakiwaombea mashujaa waliopoteza maisha sanjari na kuiombea nchi amani.

Shughuli ya Siku ya Mashujaa hupambwa na gwaride maalumu la vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama na majeshi yetu hupata fursa ya kuonesha umahiri wao katika shughuli za kijeshi. Hakika kwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ni kielelezo kingine cha heshima na utaifa wa nchi yetu, muendelezo wa historia ya nchi, tulikotoka Taifa na tulipo sasa.

Shughuli nyingine ambayo hufanywa siku ya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa nchini ni uwekaji wa silaha za jadi, ngao na mkuki na uwekaji wa maua zoezi ambalo katika ngazi ya Taifa, hufanywa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Shughuli hiyo pia hufanywa na viongozi wengine ambao huteuliwa kutokana na nyadhifa zao.

Viongozi hao ni wazee, mabalozi, Mkuu wa majeshi na mameya wa miji na majiji. Siku hiyo ya Mashujaa pia huadhimishwa katika ngazi za mikoa ambapo Mkuu wa Mkoa na baadhi ya viongozi wa kisiasa huweka silaha, ngao na mashada kwenye minara iliyopo mikoani katika kuadhimisha siku hiyo.

Siku hii muhimu huambatana na viongozi wakuu wa nchi kutembelea maeneo ya kumbukumbu ya kihistoria na makaburi walimozikwa mashujaa na wapigania uhuru wa Tanzania pamoja na kutoa otuba maalumu za kuwahakikishia wananchi amani na utulivu na usalama wa mipaka ya nchi kutoka kwa Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.

Wakati siku hiyo inapoadhimishwa vikosi vyetu vingine vya ulinzi huwa viko tayari kwenye mipaka ya nchi kwa ajili ya kufanya ulinzi makini wa nchi yetu. Jambo la kujisifia katika nchi yetu ni kuwa Tanzania imeendelea kuwa ni kisiwa cha amani katika Bara la Afrika, kutokana na kuwa na mshikamano, upendo na umoja mambo ambayo yamekuwa ni tunu ya taifa hadi hivi sasa.

Siku hii ya Mashujaa pia hutumiwa na nchi yetu katika kuendelea kujenga mahusiano kwa baadhi ya nchi za Afrika na dunia kutokana na Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kupigania ukombozi wa baadhi ya nchi katika Bara la Afrika. Nchi hizo zilizofanikiwa kupata uhuru kupitia mikononi mwa Tanzania ni Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola na Afrika Kusini.

Juhudi hizi za Tanzania kupigania uhuru wa nchi hizo zilizoratibiwa kwa karibu na hayati Baba wa Taifa, Mwl Julius Nyerere na hayati Amaan Abeid Karume zimeendelea kuijengea heshima ndani na nje ya nchi.

Shughuli zote za kupigania uhuru wa nchi zilizofanywa na waasisi wa taifa letu zilitokana na nchi yetu kuwa na jeshi imara ambalo halikutetereka ambalo limeendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya jeshi na zaidi uzalendo wa nchi yao.

Watanzania tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kujivunia hazina na tunu tuliyo nayo ya jeshi letu imara, umoja na mshikamano wa kitaifa ambao tunaendelea nao hadi leo hii. Jijini Mwanza maadhimisho hayo yalifanyika katika eneo la Mviringo wa makutano ya barabara ya Kenyata, Makongoro na Nyerere kama ilivyokuwa kwa maeneo na mikoa mingine nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, aliweka ngao, silaha za jadi na maua kwenye mnara wa hayati Baba wa Taifa ulio katikati ya Jiji.

Viongozi wengine walioweka ngao, maua na silaha za jadi katika mnara huo kwa ajili ya Siku hiyo ya Mashujaa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Anthony Diallo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Francis Mkambenga, viongozi wa madhehebu ya dini yaliyoko jijini na Mzee Nyambita Nyakutonya (83) ambaye ni askari aliyepigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Kilichonikuna katika maadhimisho hayo hadi kuandika makala haya ni kutaka kuishauri Serikali iyatumie maadhimisho haya katika kuujenga uzalendo wa taifa, ambao kwa hivi sasa hauzungumzwi zaidi hasa kwa vijana ambalo ndilo kundi kubwa kwa sasa, vijana hawa ni wenye umri kati ya miaka 10-24 ambao ni asilimia 31 ya watu milioni 45 sawa na vijana milioni 14.

Wakati wa maadhimisho haya yafanyike matamasha ya kuwajengea vijana uzalendo kuanzia Jeshi la Kujenga Taifa na wale walioko mikoani na wilayani ili waendelee kuipenda na kuijua zaidi nchi yao. Kuna watu katika nchi hii, ambao naamini hawaijui vizuri nchi yao. Hawa wanaijua kinadharia tu na ndio maana utakuta ni maarufu katika kubeza hata kukosoa mambo ya msingi yaliyofanyika katika nchi.

Hawa utasikia wakisema “ Nchi hii bwana hakuna kitu kilichofanyika,” wakati sio haba kuna mambo mengi na ya msingi yamefanyika ya kimaendeleo sio haba. Ujenzi wa miundombinu, vituo vya afya, hospitali za mikoa na wilaya, ujenzi wa shule za sekondari na mambo mengine mengi ambayo endapo nitayaorodhesha hapa itanichukua muda.

Kwa mfano baadhi ya mafanikio hayo ni ujenzi wa miundombinu. Nani hajui kuwa ilimchukua mtu siku tatu kutoka jijini Mwanza kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa basi, lakini leo hii mtu anatumia siku moja. Kuna faida kubwa kwa Mtanzania wa leo kujivunia uzalendo wa nchi yake. Uzalendo huu utatokana na kuifahamu vizuri nchi yake!

Kama haijui vizuri sio rahisi kuisemea katika mambo ya msingi ya nchi. Badala yake (hasa vijana) watabaki kubeza kila kizuri kinachofanywa katika nchi hii kwa kisingizio cha siasa. Mimi nadhani siasa iliyo bora ni ile ya kutanguliza uzalendo wa nchi sanjari na kuifahamu vizuri, haijalishi una itikadi gani ya dini na uko katika chama gani cha siasa.

Kama alivyosema jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa alipohojiwa na waandishi wa habari, askari mstaafu alivitaka vyombo vya habari kuyasema mambo yote ya msingi ya kimaendeleo yaliyopatikana badala ya kuyabeza.

“Andikeni pia mambo ya msingi yaliyofanywa na viongozi wa nchi yetu, akiwemo Rais Jakaya Kikwete haya ni mambo ya msingi kuyafanya lakini msiandike kwa kupotosha ”, alieleza mzee Nyakutonya. Naamini wakati wa maadhimisho haya yaende sanjari na vijana kwa mikoa yote nchini na katika vyuo vyetu nchini wafundishwe uzalendo na mapenzi ya kuipenda nchi yao.

Kijana akiifahamu dhana ya uzalendo, zipo faida muhimu kwake yeye na kwa taifa. Kijana akiijua vyema nchi yake, rasilimali za taifa, kuwa na mshikamano na upendo na kuwa tayari kuilinda, kuipenda na kuitetea nchi yake ndani na nje ya nchi atakuwa amekuwa na uzalendo wa kitaifa. Hivyo ni wakati muafaka sasa maadhimisho haya yatumiwe katika kuujenga uzalendo na utaifa wa nchi yetu.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi