loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba kuibukia kwa Yanga

Miamba hiyo ya soka inakutana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam huku kila mmoja akiwa na historia tofauti, alivyoanza kwenye ligi msimu huu. Ukizungumzia kisoka, Yanga ipo vizuri zaidi ya Simba na ina kila sababu ya kushinda mechi ya leo kwa vile timu hiyo inaonekana kuwa fiti zaidi ya mpinzani wake.

Licha ya kuanza ligi kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, Yanga ilisawazisha makosa na ikashinda mechi mbili mfululizo, dhidi ya Prisons iliyoifunga mabao 2-1 kabla ya kuifunga idadi kama hiyo ya mabao JKT Ruvu. Matokeo hayo ya mechi mbili, yanaifanya Yanga kujiamini zaidi na kuona ina kila sababu ya kumfunga Simba leo.

Kwa upande wa Simba, mpaka sasa haijakaa sawa, kwani imepata sare katika mechi zote tatu, tena zote ikitangulia kufunga na timu pinzani kusawazisha. Simba ilianza sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, ikatoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro na mechi ya tatu ilipata sare kama hiyo dhidi ya Stand United.

Matokeo ya mechi ya Stand ndiyo yaliyoichanganya Simba, kwani waliamini wataibukia kwa wageni hao kwenye ligi, lakini matokeo yake sasa ni tofauti. Simba ina kazi ya kujitutumua na kuibukia kwa Yanga, jambo ambalo kila mmoja anakiri kwamba ni gumu. Kujiimarisha kwa mechi ya leo, Simba ilienda Afrika Kusini, ambapo ilitarajiwa kurudi jana.

Ikiwa huko ilicheza na Orlando Pirates na kutoka sare ya bila kufungana kabla ya kufungwa mabao 4-2 na Wits University. Mechi ya mwisho ya kujipima nguvu ilichezwa Jumatano dhidi ya Jomo Cosmo, huko nako hakukuwa na matokeo ya kuridhisha kwani Simba ilichapwa mabao 2-0.

Kimtazamo, licha ya timu zote kuonesha makeke na kutumia fedha nyingi kwenye usajili kwa ajili ya ligi, Simba bado imeonekana kula hasara kwani usajili wake haujarudisha majibu ya kile ilichokikusudia.

Matokeo iliyoyapata katika mechi za mwanzo za ligi ni tofauti na matarajio ya mashabiki wengi wa soka, kwani baada ya kuingia madarakani Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu,’ matarajio ya kufanya vizuri na kuanza ligi kwa kishindo yalikuwa makubwa.

Matarajio hayo yalitiwa ‘ndimu’ na sera ya pointi tatu katika kila mechi ya Rais Aveva ambaye aliisisitiza alipokuwa akiomba kura. Pia Simba ilifanya vizuri mechi za kirafiki kujiandaa na msimu ilipopiga kambi Zanzibar, ilishinda mechi zote, na kutia matumaini zaidi ya kufanya vizuri.

Lakini hiyo imekuwa tofauti, sasa Simba inasaka ushindi kwa udi na uvumba na kwa nyakati tofauti kocha wake, Patrick Phiri na viongozi wa timu hiyo wamekamia kuibukia kwa Yanga leo. Lakini nini tatizo la Simba ikienda kuikabili Yanga leo? Inawezekana Simba ikawa inakabiliwa na tatizo la kuharibu usajili kwa kuacha wachezaji waliostahili na kusajili wasiostahili wakiwemo kama Raphael Kiongera.

Pengine hilo ni kutokana na mazoea ya klabu nchini viongozi kusajili timu badala ya kazi hiyo kuachiwa benchi la ufundi. Hasa Simba na Yanga ndizo zimekithiri usajili huo kwa lengo la kukomoana. Simba pia ilimtema beki Donald Mosoti katika dakika za mwisho za usajili ili kumuingiza Emmanuel Okwi.

Matokeo yake Simba haipo sawasawa kwenye nafasi ya beki na pengine Mosoti angesaidia hilo. Sio siri kwamba Okwi pamoja na kusajiliwa kwa mbwembwe nyingi na kuonekana kama kuizidi kete Yanga, lakini mchezaji huyo hajaisaidia Simba. Lakini kwa Yanga hali ni tofauti, imefanya usajili wake kwa umakini wa hali ya juu msimu huu ikimhusisha kocha wake mpya, Marcio Maximo.

Na hilo ndilo linaloisaidia Yanga kuwa na timu inayoeleweka na pengine kuipa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mechi ya leo. Lakini pamoja na yote, upo usemi kwamba mechi ya Simba na Yanga huwa haitabiriki, kwamba timu inaweza kuwa mbovu, lakini ikaibukia kwenye mechi ya watani. Hilo ndilo wanalotambia Simba na kujifariji kuhusu mechi ya leo.

Katika mechi ya Nani Mtani Jembe mwishoni mwa mwaka jana, Simba haikuwa vizuri. Yanga ikiamini itashinda ikajikuta ikichapwa mabao 3-1 yaliyofungwa na Amis Tambwe aliyefunga mawili na moja likifungwa na Awadhi Juma huku Okwi akiifungia Yanga bao la kufutia machozi.

Kwa uhalisia, katika mechi ya leo, Simba inauhitaji zaidi ya ushindi kuliko Yanga, ili kuepusha shari kama ilivyozoeleka kwa klabu hizo mbili pindi zinapofanya vibaya katika mechi mfululizo. Hata hivyo, katika mechi ya watani kama wasemavyo mashabiki wa timu hizo kwamba lolote linaweza kutokea, kwa maana ya Simba kushinda ama Yanga kushinda. Na isubiriwe filimbi ya Nkongo.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi