loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba yaanza vita ugenini

Wekundu hao wa Msimbazi leo watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wakati ikianza mechi zake tatu za ugenini.

Mbali ya mechi hiyo, Tanzania Prisons itaanza mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Mgambo Shooting itaikaribisha Ruvu Shooting Mkwakwani, Tanga, Rhino Rangers itakuwa nyumbani Ali Hassan Mwinyi, Tabora dhidi ya Oljoro JKT na JKT Ruvu itacheza na Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba itakuwa ya kwanza kwa kikosi cha Zdravko Logarusic ugenini kati ya mechi zake tatu ndani ya siku 11 kuanzia leo kwani akimalizana na wakata miwa hao wa Manungu, Turiani, atakwenda Mkwakwani kuikabili Mgambo Shooting na Mbeya kuwavaa Mbeya City.

Kikosi cha Logarusic kilitua Morogoro tangu juzi, lakini kikiwakosa walinzi Nassor Chollo na Gilbert Kaze ambao ni majeruhi; Chollo akiendelea na matibabu ya nyonga ya kushoto huku Kaze kwa upande wake anaendelea na matibabu ya goti yanayomtaka kupumzika kwa wiki moja.

Lakini Logarusic alisema mbali na kuwakosa wachezaji hao, ana imani kuwa kikosi chake kilichobakia kitaendelea kufanya vema, licha ya kwamba wanatarajia kupata upinzani kutoka kwa Mtibwa Sugar kwa vile kila timu inazihitaji pointi ili kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo.

Alisema licha ya kutarajia upinzani, ana matarajio makubwa ya ushindi katika mchezo huo kwa vile amekiandaa kikosi chake kwa ajili ya kupambana katika kutafuta ushindi.

“Wachezaji wapo salama na wapo katika hali ya ushindi tayari kwa kuvuna pointi,” alisema Loga ambaye kikosi chake kinashika nafasi ya nne kikiwa na pointi 30, sita nyuma ya vinara Azam FC, tano kwa watani wao wa jadi, Yanga na Mbeya City katika nafasi ya tatu kwa pointi 31.

Simba inaingia uwanjani ikiwa imetoka kuirarua Oljoro JKT kwa mabao 4-0, ikiwa pia imeanza mzunguko wa pili kwa kuilaza Rhino Rangers bao 1-0, zote kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Logarusic atakuwa na kazi nzito ya kuwafunga vijana hao wa Mecky Maxime, ambao licha ya kuwa hivi sasa wanatofautiana nao kwa pointi tisa wakiwa katika nafasi ya tano, ni timu yenye wachezaji wazoefu na wamekuwa wakitoa upinzani kwa timu kongwe nchini.

Mtibwa Sugar iliyoanza mzunguko wa pili kwa kutoka sare na ndugu zao wa Kagera Sugar na kisha kufungwa na Azam FC, imesema wamejipanga vizuri kuondoka na pointi tatu.

Mechi ya mzunguko wa kwanza walifungwa na Simba mabao 2-0. Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema: “Tumeanza vibaya Ligi Kuu mzunguko wa pili baada ya kufanya vibaya katika mchezo uliopita, leo ni siku ya nne (jana) tunafanya mazoezi ya nguvu kwa ajili ya kubakiza ushindi.”

Kwa upande wa Prisons, itakuwa inaanza mzunguko wa pili baada ya mechi zake kuahirishwa ili kupisha matengenezo ya Uwanja wa Sokoine, na leo wanaanza na Coastal Union ambao mechi ya mwisho walitoka sare ya 0-0 na Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Prisons ni ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi tisa, wakati Coastal Union ni ya saba wakiwa na pointi 18, hivyo kila mmoja pointi tatu ni muhimu kwa ustawi wake katika ligi hiyo.

Rhino Rangers baada ya vipigo kutoka kwa Simba na Azam, itajirudia nyumbani kwa kuwaalika Oljoro JKT, huku wote kila moja ikiwa na pointi 11.

JKT Ruvu katika nafasi ya tisa na pointi zake 18, itakuwa mwenyeji wa Ashanti United ya 12 katika msimamo huo, ambayo inapigania maisha kuepuka kurejea Ligi Daraja la Kwanza.

TIMU ya Ruvu Shooting imeboresha kikosi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi