loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba yamalizana na Maguli, Kwizera, Kisiga

Wachezaji hao ni Elias Maguli wa Ruvu Shooting aliyesaini mkataba wa miaka miwili, Shaban Kisiga aliyewahi kucheza Simba, Azam na Mtibwa Sugar mkataba wa mwaka mmoja na Mrundi Pierre Kwizera aliyekuwa akikipiga katika timu ya AFAD Djekanou ya Abidjan nchini Ivory Coast ambaye amesaini miaka miwili.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wachezaji hao wataanza kuonekana kwenye viwanja vya Simba tayari kwa maandalizi ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2014/15 unaotarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia Septemba 20, mwaka huu.

“Tumechelewa kufanya usajili kwa sababu unahitaji umakini, tumefanikiwa kwa hao na bado tunaendelea na mazungumzo na wachezaji wengine. Kamati ya Usajili iko makini inafuatilia ili kutekeleza yale ambayo kocha amependekeza,” alitamba Kaburu.

Kuhusu Mkenya Paul Kiongera ambaye pia alifanya mazungumzo ya awali ili kuitumikia klabu hiyo, Kaburu alisema hilo liko chini ya Kamati hiyo ya Usajili.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Maguli alisema mashabiki wa Simba wategemee kuona vitendo vyake kwani atashirikiana na wenzake kuisaidia kutwaa ubingwa wa ligi.

“Nashukuru kwa kujiunga na Simba naahidi kwamba kazi yangu itaonekana uwanjani tutakapoanza msimu,” alisema Maguli, mfungaji namba mbili wa Ligi Kuu msimu uliopita akiwa na mabao 14.

Kwa upande wake, Kisiga alisema anashukuru kurudi tena Simba, na ana imani itafanya vizuri msimu ujao. Kwa upande wake, kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Pierre Kwizera alitua jana mchana akiwa na matumaini kibao ya kuisaidia Simba msimu ujao.

Kwizera aliyewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam saa nane mchana, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya, leo saa 5 asubuhi, atasaini mkataba na Simba. Hata hivyo, awali Kaburu aliwaambia waandishi wa habari kuwa amesaini tayari mkataba huo.

Kwizera alisema matarajio yake ni kusaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na hatimaye kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.

“Naijua Simba ni timu kubwa, lakini kwa hivi karibuni haijaweza kushiriki mashindano ya kimataifa hivyo nitacheza kuhakikisha timu inafanya vizuri ili kukata kiu ya mashabiki,” alisema Kwizera ambaye katika msimu uliopita, alikuwa mchezaji pekee wa kulipwa wa Academie de Foot Amadou Diallo- Djekanou ambayo pia inajulikana kwa jina la AFAD Djekanou.

Mchezaji huyo atakuwa wa nne kwa wachezaji wa kigeni huku akisubiriwa Paul Kiongera kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Wachezaji wa kigeni waliopo Simba ni mabeki Mkenya Donald Mosoti, Mganda Joseph Owino na mshambuliaji Amisi Tambwe wa Burundi.

Mbali na wachezaji hao, wengine ambao walishasajiliwa ni Mohamed Hussein kutoka Kagera Sugar, Michael Mgimwa aliyekuwa akikipiga Thailand na Hussein Sharrif aliyekuwa Mtibwa Sugar.

(Habari hii imeandikwa na Grace Mkojera na Rahel Pallangyo).

KLABU ya Simba  imetambulisha  mashindano mapya ya Super  Cup, ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi