loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simu, mitandao ya kijamii 'vinavyowatafuna' wanafunzi

Kwa uchache nchi hizo ni pamoja na Marekani, China, Japan, Uingereza, Ujerumani, Urusi, Ufaransa na zinginezo.

Uvumbuzi wao umekuwa na msaada mkubwa kwa watu wote duniani ikiwa ni pamoja na wananchi wa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwemo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba nchi nyingi zinazoendelea haswa za Kiafrika, zimeendelea kuwa wapokeaji wakubwa wa teknolojia zinazovumbuliwa kutoka katika nchi hizo.

Miongoni mwa vitu ambavyo vimevumbuliwa na nchi hizi ni pamoja na vyombo vya usafiri kama vile magari, ndege na meli, mbali na mitambo inayotumika viwandani. Wavumbuzi hawa hawakuishia hapo, bali wameendelea kuvumbua vifaa vya mawasiliano kama vile simu na kompyuta.

Maendeleo ya teknolojia yaliwezesha pia kutoka kwenye matumizi ya simu za mezani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma hadi simu za mkononi ama kutoka kuitumia kompyuta kwa mahesabu hadi kuwa chombo muhimu cha mawasiliano.

Katika nyanja ya mawasiliano ambayo makala haya yatajikita zaidi, uvumbuzi wa hivi karibuni ambao unalenga kurahisisha mawasiliano ni pamoja na mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, instagram, whatsapp na nyinginezo.

Kama kawaida yetu Watanzania, tumenyoosha mikono yetu na kuvipokea vitu hivyo kwa mikono miwili.

Hakuna anayeweza kubisha juu ya ukweli kwamba, ugunduzi huu umekuwa na msaada mkubwa kwetu, katika kuwasiliana na kupashana habari, hususan kwa wakazi wanaoshi maeneo yanayopata umeme, zaidi mijini.

Leo hii imekuwa ni rahisi sana kwetu kuweza kufanya mawasiliano na watu mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kupitia njia hizi za mawasiliano, tofauti na zamani ambapo mawasiliano yalikuwa ni shida kubwa kwa wengi, si Tanzania tu bali hata katika nchi zilizoendelea kabla ya kuvumbuliwa kwa teknolojia hizi.

Kuna wakati ilikuwa inamchukua mtu zaidi ya mwezi mzima kutoa ujumbe kutoka Kigoma kuupeleka Lindi ama kutoa ujumbe Dar es Salaam kuupeleka Moshi.

Siku hizi kukitokea msiba, ni sekunde chache tu wahusika nchi nzima na hata nje ya nchi wanaweza wakawa wameshapata habari, tofauti na zamani ambapo njia iliyoonekana rahisi ni kutumia matangazo ya vifo ya redio.

Pamoja na manufaa mkubwa yanayopatikana kupitia njia hizi za mawasiliano, kwa wanafunzi imeanza kuwa ni changamoto zake, mintarafu suala zima la masomo na maadili. Unapozungumzia twitter, facebook, instagram na whatsapp kwa mzee wa kijijini aliyeko Liyegama, Kilombero, ama yule anayelima tumbaku kule Tabora anaweza asikuelewe.

Lakini ukirudi mjini, hususan kwa wanafunzi, ni wachache ambao hawaelewi kwa vile wengi wanajihusisha sana na mawasiliano hayo ya kisasa.

Pengine utafiti wa kina ukifanyika unaweza ukaonesha kwamba wanafunzi wa Tanzania, ndio wadau wakubwa wa matumizi ya mawasiliano ya aina hii, yaani simu za mkononi na mitandao ya kijamii.

Siku hizi vyuoni watu wanatumia muda mwingi sana kutuma meseji, kutumiana picha, kuongea na wenzi wao kupitia simu, facebook na kadhalika.

Hatusemi kuwa ni vibaya kwao kutumia njia hizi rahisi katika kuwasiliana, la hasha! Tatizo ni aina ya matumizi yao kwa hizo simu na hiyo mitandao ya kijamii.

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa mwanafunzi kutumia zaidi ya saa sita katika kipindi cha usiku kuongea na simu ama 'kuchati' kwenye facebook, mambo ambayo wakati mwingine hayana faida, mintarafu suala zima la masomo.

Leo hii mitandao mingi ya simu hapa nchini imekuwa ikitoa huduma ya meseji kwa gharama nafuu zilizopewa majina kama kujirusha, kucheka na kadhalika.

Kwa watu walio 'bize' maofisini meseji hizi za bei nafuu zinaonekana ni nyingi mno na wengi hawatumii hata robo yake lakini kwa wanafunzi wa kitanzania kwao ni kazi ndogo kuzimaliza kwa siku moja! Kwa lugha nyingine ukitaka kuona namna vidole vinavyoongea tembelea vyuoni.

Uchunguzi wangu unaonesha kwamba mwanafunzi wa Tanzania yupo tayari kutumia siku nzima ya Jumamosi ama Jumapili kwa kutuma na kupokea meseji kutoka kwa kwa rafiki zake.

Yupo tayari kupoteza muda wake mwingi sana kwa 'kucheza' kwenye facebook kuliko anavyoutumia kwenye masomo.

Hali hii haijitokezi kwa wanafunzi wa ngazi ya chini peke yake yaani shule za msingi na sekondari tu, bali hata wale walio katika ngazi ya vyuo. Swali la kujiuliza ni pamoja na hili.

Ni kitu gani kinachojadiliwa na wanafunzi hawa mpaka kutumia muda wao mwingi kiasi hicho kwa 'kuchati' na hasa kwa kuzingatia kwamba wao wenyewe husema “ni vigumu kwa watu wa jinsia moja kutumia zaidi ya nusu saa wakitumiana meseji?”

Ukimuona mtu anatumia zaidi ya saa nzima kuongea na simu usiku, basi jua mazungumzo hayo yanahusisha watu wenye jinsia mbili tofauti. Kwa tafsiri ya haraka haraka, watu wa jinsia mbili tofauti wanapodumu zaidi ya saa nzima, tena usiku kuzungumza, mazungumzo hayo yatakuwa yanahusu mapenzi tu.

Kwa namna hii inaonekana kwamba, wanafunzi wengi wa Tanzania wamekuwa wakishughulishwa sana na kujadili mapenzi badala ya masomo.

Yaani imekuwa rahisi kwa wanafunzi kukesha muda mwingi wa usiku wakitumia simu kuchati, kupigiana ama mitandao ya kompyuta kuliko wanavyotumia muda huo kwa kusoma ama kupekua vitabu maktaba.

Badala ya uvumbuzi huu kusaidia mawasiliano ya kimaendeleo zimezua balaa ya kurahisisha mawasiliano ya mahusiano ya kimapenzi, ambayo mara nyingi hayana faida kwa mwanafunzi.

Katika uchunguzi wangu ni nadra kuona mtu anauliza maswali yahusuyo masomo kupitia facebook ili kuyajadili ama kupitia simu bali masuala ya mahusiano.

Mimi nadhani kama wanafunzi watabadilika na kutumia mawasiliano hayo kwa ajili ya kusaidiana masomo hakika tutaona mafanikio yake baada ya muda mchache tu.

Hivi wanafunzi hatujiulizi kwamba, kadri maendeleo ya sayansi na teknolojia yanavyozidi ndivyo na elimu yetu inavyozidi kushuka! Leo hii imefikia mwanafunzi badala ya kujibu mtihani, yeye anamchora mchezajii wa mpira wa miguu, Messi ama anaandika mistari ya nyimbo za Bongofleva.

Hii ni kwa kuwa vitu hivyo ndivyo anavyoviona sana akiwa kwenye mitandao badala ya masomo. Wakati mwingine tusiilaumu Serikali kwamba haiboreshi elimu wakati wanafunzi tunakalia 'kuchati'.

Haipendezi kuona kwamba Watanzania tumekuwa wazuri wa kuiga mabaya badala ya yale mazuri. Tuliiga kushusha suruali zetu chini ya makalio, na leo hii tunaiga kutumiana picha chafu kupitia simu zetu.

Tuige yale mazuri kwa maendeleo yetu wenyewe na ya taifa letu. Wakati tunaomba Serikali ijitahidi kuboresha elimu kwa kutupatia walimu bora, maktaba, maabara na vitabu na sisi tuache kupoteza muda kwa 'kuchati' na kutumia picha ambazo hazina maadili.

Tukumbuke tunapopata neema ya kusoma, tuifanyie kazi kabla ya kuikosa kwani Waswahili husema umuhimu wa kitu mara nyingi huja pale tu mtu anapokikosa.

Ni vyema tukakumbuka kwamba, neno “ningejua” huja kipindi ambacho mwanadamu ameshaharibikiwa na jambo.

Ni vyema kila mmoja wetu akatekeleza majukumu yake kama mwanafunzi kwa kusoma kwa bidii badala ya 'kuwekeza' katika masuala ya mahusiano kupitia mitandao ya simu na kompyuta ambayo haina tija.

Mwandishi wa makala haya ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Habari .

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Ally Bakari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi