loader
Picha

Stamico yatangaza neema

Chini ya mkakati huo wa kuhakikisha linajiendesha kwa faida, wachimbaji wadogo watawezeshwa mashine za kisasa za uchimbaji na kuhakikisha wazawa pia wanawekeza kwenye rasilimali za taifa kwa faida.

Kadhalika, mkakati mwingine ni kuhakikisha shirika hilo linajiendesha kwa faida na kupeleka fedha Hazina, badala ya kutegemea Serikali kuliendesha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Mhandisi, Edwin Ngonyani alisema hizo ni kazi mbili muhimu anazotaka kuzifanya ndani ya shirika hilo na kuhakikisha linajiendesha lenyewe bila utegemezi wa Serikali kuanzia miaka miwili ijayo.

“Nimeanza kazi rasmi hapa Juni mosi mwaka huu, kazi zangu kuu ni mbili na ndizo nitakazohakikisha zinatekelezwa, moja ni kurekebisha shirika, liwe linapeleka fedha Hazina, hii tabia ya mashirika ya Serikali ya kuchukua fedha Hazina itakoma kwa shirika hili, na mbili ni kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini,” alisema Ngonyani.

Alisema kwa miaka miwili kuanzia sasa, shirika hilo litaomba kuwezeshwa fedha na Serikali kama mtaji na baada ya hapo litajiendesha na litapeleka fedha Hazina na hiyo inawezekana kupitia miradi yake mingi iliyoanza na mingine itakayoanza uzalishaji hivi karibuni. Wachimbaji kuula

Akizungumzia mkakati kwa wachimbaji wadogo, Ngonyani alisema, ndani ya miaka miwili ijayo, shirika hilo litanunua mitambo miwili ya uchimbaji wa kisasa ambayo wataitumia na kwa kuanzia, gharama za ulipiaji mitambo hiyo, shirika litaitoza Serikali.

Alisema baada ya muda, wachimbaji hao watazoeshwa na kueleweshwa umuhimu wa kuchangia gharama na kisha baadaye watatozwa gharama hizo baada ya wao kuanza kufaidika na uchimbaji wa kisasa.

“Tunataka wachimbaji wadogo wa madini nchini wanufaike na wao wawe sehemu ya uwekezaji kwenye rasilimali zao, kama ambavyo hao wawekezaji wa nje wanavyowekeza, na sasa Watanzania nao watawekeza, kwani hao wametoa fedha zao mfukoni za mtaji? Si benki zimewakopesha na sisi watu wetu watakopeshwa na benki, ila lazima tuwawezeshe,” alisema Ngonyani.

Alisema lengo la Stamico kwa wachimbaji wadogo ni kuhakikisha wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba kisasa ili pia watoa mitaji ambao ni benki, wawe na uhakika wa fedha zao kurejeshwa. Kwa mujibu wa mtendaji huyo, ikibidi, shirika hilo litawawekea dhamana wachimbaji wadogo wawezeshwe kibenki.

Alisema hilo litawezekana baada ya mkakati wao wa kuanzisha na kuboresha taarifa za wachimbaji wadogo zikiainisha mahali walipo, aina ya madini wanayochimba na mahitaji yao.

Mkakati mwingine ni kubaini vyanzo vya migogoro kwenye maeneo ya wachimbaji na kutafuta suluhu ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Mgodi wa Biharamulo Katika hatua nyingine, Ngonyani alizungumzia mradi wa uchimbaji madini kwenye mgodi wa dhahabu wa Tulawaka ambao hivi sasa umenunuliwa na shirika hilo na kuitwa Biharamulo unaosimamiwa na kampuni ya Stami Gold.

Alisema mgodi huo utaanza kazi rasmi Agosti 8, mwaka huu na kwamba baada ya miaka miwili na nusu, watapata faida ya Sh bilioni saba.

Awali mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Barrick Gold na mwishoni mwa mwaka jana, Stamico ikaununua kwa dola milioni tano.

Kuuzwa kwa mgodi huo kutoka Barrick kwenda Stamico, kunatajwa kulitokana na mwekezaji huyo wa awali kuona gharama za uendeshaji ni kubwa hivyo akaamua kuacha uwekezaji.

Kwa upande wake, Meneja Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagweleka alisema hivi sasa miradi mitano iko kwenye ubia na shirika hilo kwa ajili ya uwekezaji. Miradi hiyo ni pamoja na mgodi wa dhahabu wa Itetemia ambao Stamico imeingia ubia na Kampuni ya Madini ya Tancan Ltd. Mradi mwingine ni wa Buckreef ambao ni wa dhahabu ulioko Geita.

Pia Stamico imeingia ubia na Kampuni tanzu ya Tanzam 2000, ambapo Stamico wana hisa asilimia 45 na 55 iko kwa kampuni hiyo na kwamba wanategemea uzajishaji utaanza Novemba mwaka huu.

Vile vile upo mradi wa Kiwira unaozalisha makaa ya mawe kwa ajili ya kufua umeme utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Meneja Fedha na Utawala wa Stamico, Peter Gembe, hivi sasa mradi huo ni wa ubia na Kampuni ya JV Partnership. Lengo ni kufua megawati 200 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye Gridi ya Taifa.

“Tunapanua mgodi chini ya ardhi, awali mgodi ulikuwa unazalisha tani 150,000 za makaa ya mawe ila sasa tunataka zifike tani 300,000, pia tutajenga mitambo mipya ili iwe na uwezo wa kuzalisha hizo megawati 200 badala ya zile sita za awali,” alisema Gembe.

Stamico ni Shirika la Umma lililoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa na kuzalisha nafasi za ajira kwa Watanzania.

SHIRIKA la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi