loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sukari ni 'tumbaku mpya' kiafya

Katika utafiti wao, wataalamu wa afya wamegundua kwamba hata maziwa ya mtindi yaliyoondolewa mafuta huweza kuwa na vijiko vidogo vitano vya sukari huku baadhi ya rojo za nyanya za kwenye chupa zikiwa na vijiko hadi vinne vya sukari.

"Kwa sasa sukari ni tumbaku mpya kiafya," anasema Simon Capewell, Profesa wa Mambo ya Tiba na Matumizi ya Vyakula Mwilini katika Chuo Kikuu cha Liverpool. Profesa huyo anasema:

"Kila mahala duniani kote vinywaji baridi ama vyakula vinatengenezwa kwa kunogeshwa na sukari nyingi kwa ajili ya walaji; wazazi na watoto, ambao hawajui kama wanakula 'sumu'.

Viwanda vinajali faida tu, lakini suala la afya havina habari," anasema Profesa huyo. Anasema unene ambao unasababishwa zaidi na kula vyakula vyenye sukari nyingi pamoja na mafuta ni tatizo la kila mahala duniani siku hizi ikiwa ni pamoja na nchi zinazoendelea. Uchunguzi unaonesha kwamba unene na kisukari, huigharimu Uingereza zaidi ya paundi bilioni 5 kwa mwaka.

"Kama hatua hazitachukuliwa gharama za kutibu magonjwa yatokanayo na unene na kisukari zitafika paundi bilioni 50 ifikapo mwaka 2050," ripoti moja ya wasomi nchini Uingereza inaonesha.

Profesa Capewell ambaye ni mmoja wa wanaharakati wa masuala ya afya anayepiga kampeni kubwa dhidi ya matumizi ya vyakula vya sukari ameshauri viwanda kufanya mbadiliko ya hiari kwa kupunguza viwango vya sukari katika bidhaa zao hata kabla sheria kali hazijatungwa kudhibiti hali hiyo.

Utafiti unaonesha kwamba raia wa kawaida wa Uingereza kwa siku, kuanzia chai, vitafunwa na vinywaji hadi anapolala huwa ametumia wastani wa vijiko vidogo 12 vya sukari kwa siku na wengine hutumia hadi vijiko 46.

Kiwango cha juu kabisa cha sukari ambacho kimependekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni vijiko vya chai vitano vya sukari kwa siku, ingawa wanasayansi wengi wanaona kwamba bado ni vingi wakitaka kiwango cha juu kabisa kiwe nusu yake.

WHO kwa muda mrefu ilishasema kuwa kuna ushahidi mkubwa kwamba vinywaji vingi ambavyo ni vitamu kutokana na sukari ama vyakula vilivyoongezwa sukari ni chanzo kikubwa cha unene na kisukari, sambamba na magonjwa mengine ya moyo.

Utafiti uliofanywa karibuni na wanaharakati wanaopinga matumizi makubwa ya sukari umeonesha kwamba vyakula vingi vya kwenye makopo na chupa vina sukari nyingi ambayo haina faida mwilini zaidi ya hasara.

Pamoja na kuchukiwa na kampuni ya soda kwa kuwataka wananchi kuachana kabisa na bidhaa hizo kama ikiwezekana, Action of Sugar wanasema viwanda vinavyozalisha chakula na kuongeza sukari vilazimishwe kama havitaki, kuipunguza kwa asilimia kati ya 20 na 30 katika kipindi cha miaka mitano.

Kundi hilo linaamini hatua hiyo ikichukuliwa na viwanda, itasaidia kupunguza unene na magonjwa yatokanayo na unene. Graham MacGregor, Profesa katika Chuo cha Afya cha Wolfson jijini London, Uingereza, na ambaye pia ni Mwenyekiti wa Action on Sugar anasema:

"Tuna dhima ya kupambana na tatizo la unene na si Uingereza pekee bali duniani kote.

"Pa kuanzia ni kuweka mpango na mkakati wa kuhakikisha viwanda vinavyotengeneza chakula vinapunguza sukari katika bidhaa zao na hii pia itasaidia watu kupunguza tabia ya kupenda kula ama kunywa vitu vyenye sukari nyingi. Kupenda sukari nyingi ni tabia tu ambayo mtu anaweza kuiacha akiamua," anasema. Anaongeza: "Mpango huu lazima baadaye uchukuliwe na serikali yetu na zingine duniani, hususan idara za afya katika kuhakikisha kiwango cha sukari kwenye vyakula na vinywaji kinapunguzwa."

Dk Aseem, Mkurugenzi wa Kundi la Action on Sugar, anasema: "Watu wanapaswa kujua kwamba chakula kilichoongezwa sukari hakijaongezwa kirutubisho muhimu cha mwili kwa hiyo waanze kujenga tabia ya kutopenda sukari nyingi." Dk Aseem anazidi kusema:

"Mbali na sukari nyingi kuwa sababu kubwa ya unene, kuna ushahidi mwingi unaoonesha kwamba kuongeza sukari kwenye chakula kunaongeza pia uwezekano wa mtumiaji kupata aina ya pili ya ugonjwa wa kisukari ama kupata ugonjwa wa ini kujaa mafuta na hata matatizo kwenye uyeyushaji wa chakula kwa ajili ya kutengeneza nguvu mwilini.

"Ni wakati mwafaka sasa wa kuwalinda watoto wetu dhidi ya tatizo hili kubwa la kiafya kwa sasa na hivyo, wazalishaji wote wa chakula wanatakiwa haraka kupunguza kiwango cha sukari wanachoongeza kwenye vyakula na hususan kwenye vyakula vya watoto. Wanapaswa pia kuacha kuwalenga watoto katika matangazo ya bidhaa zao zenye sukari nyingi," anasema.

Lakini baadhi ya kampuni zinazozalisha vyakula nchini Uingereza zinadai kwamba wataalamu hao wanazungumza zaidi maneno kuliko ushahidi wa kisayansi.

Wanadai kwamba chapisho moja la WHO halikuonesha uhusiano wa moja kwa moja wa ugonjwa wa kisukari na unene na kwamba mara nyingi unene unatokana na maumbile kama si mtu kupenda kula na si kwa sababu ya matumizi ya sukari.

Wenye viwanda pia wanajificha nyuma ya jarida la watafiti fulani waliokuja na maelezo kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonesha kuwa kisukari kinatokana na matumizi ya sukari. Barbara Gallani wa Chama Wazalishahi wa Vyakula na Vinywaji anasema haamini kama sukari ni sababu ya unene.

Hata hivyo, Profesa Shrinath Reddy, Mhadhiri wa Magonjwa ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Harvard na mjumbe wa jopo la wataalamu wa WHO anasema kwamba, hoja za wenye viwanda vya chakula ni za kupuuzwa kwa sababu wanatafuta pa kutokea ili waendeleze biashara zao hata kama wanawalisha watu 'sumu'.

Anasema ushahidi uliopo kuhusu uhusiano wa matumizi ya sukari na unene ama kisukari si wa kupapasa ama kufikirika.

Imetafsiriwa kutoka gazeti la Daily Mail la Uingereza na Hamisi Kibari.

Tafsiri hii si rasmi.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi