loader
Dstv Habarileo  Mobile
Sumbawanga watumia BRN kusambaza maji vijijini

Sumbawanga watumia BRN kusambaza maji vijijini

Utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa kuwashirikisha kikamilifu walengwa wa huduma za maji wakiwemo wanufaika wenyewe wa maji katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kubuni, kupanga, kujenga, kuendesha na kufanya matengenezo ya miradi ya maji na pia kuchangia gharama za utoaji wa huduma hiyo.

Pamoja na jitihada za Serikali za kuendeleza za maji kuanzia miaka ya 1970, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama siyo ya kuridhisha. Lengo la Sera ya Maji Kitaifa likiwa kuwapatia wananchi wote maji safi na salama katika umbali usiozidi meta 400.

Kitakwimu, utekelezaji wa lengo hilo kwa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga unaonesha kuwa ni wananchi wanaokadiriwa kufikia asilimia 49.8 ya wakazi wake ndio wanaofaidika na huduma ya maji safi na salama inayotokana na maji ya bomba, visima virefu, mito pamoja na chemchemi zilizopo.

Ili kukabiliana na tatizo la upatikaji wa maji safi na salama kutoweza kuifikia idadi kubwa ya wakazi katika Halmashauri hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Maji imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (MMS) maarufu kama BRN.

Kasi ya mpango huo endelevu wa Matokeo Makubwa Sasa imeanza kuonekana katika vijiji vilivyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambapo kukamilika kwa miradi hiyo ya maji kutawanusuru wakazi wa maeneo hayo ambao mara kwa mara wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa ya milipuko, ikiwemo ya kuharisha na kipindupindu kutokana na kunywa maji machafu kutokana na kukabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa majisafi na salama.

Kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 3.3 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika miradi ya maji na Programu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RWSSP) ifikapo 2015; kukamilika kwa miradi hiyo miwili ambapo wakazi wapatao 131,103 watanufaika.

Akifafanua, Kaimu Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Habib Salum Bushiri anasema wanufaika wa mradi endelevu wa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni wakazi wapatao 44,778 wanaoishi katika vijiji vya Kinambo, Solola na Mafinga katika Bonde la Ziwa Rukwa.

Kwa upande wa programu ya RWSSP wanufaika ni idadi ya wakazi wapatao 86,325 katika vijiji vya Nankanga, Kyamatundu, Ikozi, Mpui na mji mdogo wa Laela.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Adam Abeid Missana alifanya ziara ya kikazi ya siku moja kwa kutembelea mradi wa maji unaotekelezwa chini ya mpango wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika kijiji cha Mfinga kilichopo katika Kata ya Mfinga akiongozana na wataalamu ili kukagua miradi ya maji.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bushiri, ukarabati wa miundo ya maji ya mradi huo unaotekelezwa katika kijiji cha Mfinga chini ya mpango wa MMS, ulianza Machi 20 mwaka huu ambapo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 45.

Shughuli zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa tangi la maji lenye uwezo wa kuhifadhi meta za ujazo 100 wa maji kwa wakati mmoja uchimbaji wa mtaro wa kusambazia maji wenye urefu wa mbali wa kilomita 7.5 na ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji kijijini hapo.

Ziara hiyo iliambatana na kutembelea na kukagua chanzo cha maji, ujenzi wa mtaro wa maji wenye urefu wa kilomita 7.5 na tangi la maji lenye uwezo wa kuhifadhi meta 100 za ujazo wa maji kwa wakati mmoja pia vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa katika taasisi mbalimbali zikiwemo shule mbili, zahanati, majengo ya ibada na maeneo ya makazi ya wananchi.

Mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya maji unaotekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umebuniwa na wakazi wenyewe wa kijiji hicho cha Mfinga ili waweze kuondokana na kadhia ya uhaba mkubwa wa maji safi na salama.

Ukosefu wa maji unawalazimu wakazi wa kijiji hicho cha Mfinga kutembea mwendo mrefu kutafuta maji kadhia ambayo pia imesababisha baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na akina mama kutumia muda mwingi katika foleni ya maji na wanaporejea nyumbani wanakuta waume zao wamekasirika.

“Tatizo la maji linasababisha tupoteze muda wetu mwingi na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, jambo ambalo linasababisha mifarakano kwa wanandoa na baadhi yao wameachana,” anasema Mwanahamisi Jumanne.

Mwanahamisi anasema maji wanayopata baada ya kutembea umbali mrefu hayana ubora wowote kwa sababu yanapatikana kwenye vijito ambayo vinatumiwa na wanyama kama punda na ng’ombe.

“Pia sisi tunaoga na kufulia humo humo kisha tunayachota kwa matumizi ya nyumbani ikiwemo kupikia na kunywa,“ anasema Mwanahamisi.

Diwani wa Kata ya Mfinga, Juma Hamis, anasema mradi wa maji ambao unatekelezwa katika kata yake chini mpango wa Matokeo Makubwa Sasa utakapokamilika utasaidia kuharakisha maendeleo kwa kuwa magonjwa yatapungua na wananchi hasa wanawake na watoto watatumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo badala ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kutupatia mradi huu wa maji katika mpango wa MMS ambapo ukikamilika basi kero yote ya maji inayotukabili itakuwa imepata ufumbuzi wa kudumu, isitoshe utatunusuru na milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa ya kipindupindu na kuharisha,“ anasema Hamis.

Anaongeza kuwa sasa Kata hiyo iko katika mikakati ya kuunda kamati ya watumiaji wa maji ambayo itasimamia usafi wa maji pia kiwango cha asilimia ya uchotaji maji na kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu wa maji na ukarabati na ulinzi wa miundo mbinu hiyo ya maji.

Anafafanua kuwa kila ndoo moja ya maji itatozwa kiasi cha Sh 100- fedha ambazo zitakusanywa na kuingizwa katika Mfuko wa Maji wa kata ambazo zitasaidia kukarabati miundombinu ya maji pindi ikiharibika.

Pia ameomba mradi huo wa maji uweze kufika hadi kijiji cha jirani cha Kasekala kilichopo katika kata hiyo kikiwa na wakazi chenye wakati 2,400 ambao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Missana anaeleza kuwa changamoto kubwa ni kiwango kikubwa cha uharibufu wa mazingira kinachofanywa katika vyanzo vya maji ikiwemo ukataji miti na shughuli zingine za kibinadamu ikiwemo kulima na kuchungia wanyama katika vyanzo hivyo .

“Lazima wanufaika watambue kuwa mradi huu ni mali yao na jukumu la kuikarabati na kuitunza ni wajibu wao na wala si jukumu tena la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Manassa anaeleza.

Amewataka wananchi Kata ya Mfinga zianzishe Jumuiya za Watumiaji Maji ambazo pamoja na majukumu mengine ni kusimamia usalama wa miundo mbinu ya maji hususani mabomba ya kusambazia maji ambayo yameshatandazwa lakini yameaanza kuibiwa.

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Sumbawanga

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi