loader
Dstv Habarileo  Mobile
Swahili Fashion inavyozidi kufungua njia

Swahili Fashion inavyozidi kufungua njia

Katika onesho hilo lililowashirikisha wabunifu ndani na nje ya nchi kulikuwa pia na utoaji wa tuzo mbalimbali za washindi wa vipengele vilivyokuwa vikiwaniwa. Kwa mwaka huu onesho la Swahili Fashion linaonekana kuwa na mvuto zaidi hasa ikilinganishwa kuwa kulikuwa na wabunifu kutoka nchi nyingi ambao nao walionesha kazi nzuri.

Wabunifu kutoka Zambia, Kenya, Uganda, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Ghana, Jamhuri ya Czech na nyingine. Akizungumzia onesho hilo kwa mwaka huu Mwandaaji Mustapha Hassanali anasema kuwa kwa mwaka huu wabunifu wengi wameonesha kazi zao mpya tayari kwa mwaka ujao.

Anasema kuwa wabunifu wameonesha uwezo katika kubuni ambapo kila kazi iliyooneshwa inaweza kuwa na manufaa pia kwa watanzania. Alisema kuwa wabunifu wa nje takribani 15 wameonesha mavazi yao katika onesho hilo. “Najua kwa sasa Swahili Fashion imewagusa watu wengi sana kwa kuwa ni onesho kubwa katika Afrika Mashariki na Kati na hivyo linazidi kukua na kuwapata wabunifu wengi kutoka sehemu mbalimbali,” anasema Mustapha.

Anasema kuwa onesho la Swahili Fashion limewatambulisha wabunifu wa Kitanzania mbalimbali katika ulimwengu wa masuala ya mitindo duniani. “Hili ni moja ya mashindano yanayokubalika hapa nchini na hata nje ya nchi kutokana na umakini wake wa uandaaji lakini pamoja ni kutokana ukubwa wake,” anasema Mustapha.

Anaongeza kuwa Swahili Fashion inatakiwa kutumiwa vema na wadau wote wa masuala ya Mitindo nchini katika kujitangaza ndani na nje ya nchi. Anasema kuwa inatakiwa kwa sasa wabunifu wa kitanzania kuhakikisha kuwa wanatumia onesho hilo sio tu kutangaza biashara zao lakini pia kuhakikisha kuwa wanaongeza hamasa kwa watanzania ya kuvaa mavazi yaliyobuniwa hapa nchini.

Kwa upande wake Mbunifu Bora wa mwaka 2013, Evelyn Rugemalila anasema kuwa kupitia onesho la Swahili Fashion watanzania wanapata nafasi ya kuwajua zaidi wabunifu wao. Anasema kuwa hili likifanikiwa inabakia kuwa kazi kwa wabunifu wa hapa nyumbani wenyewe kutumia fursa zilizopo katika tasnia hiyo.

Anasema kuwa kwa sasa Watanzania wamehamasika kuvaa mavazi yaliyobuniwa na wabunifu wa hapa nyumbani ambapo wanashonesha magauni kutoka kwa wabunifu hao wa ndani. Anaongeza kuwa kwa upande wake akiwa kama mbunifu bora wa mwaka huu amefikia hatua hiyo kutokana na kazi zake alizowabunia watu ambao ni Watanzania wanaopenda na kuthamini kazi za wabunifu wa hapa nyumbani.

“Kupitia maonesho kama haya ya Swahili Fashion na mengineo ni wakati wa wabunifu kujuana na kufanya kazi kwa pamoja lakini pia ni fursa ya kuwapata wateja wetu,” anasema Evelyn. Kwa upande wake mbunifu mwingine ambae anamiliki lebo ya Zaidi Afrika, Zamda George ambae amekuwa akijihusisha na tasnia ya ubunifu kwa takribani miaka mitano anasema kuwa Swahili Fashion ni jukwaa la kujikuza kibiashara zaidi.

Anasema, kwa sasa wadau wengi wanatengeneza nguo zao kwa wabunifu wa ndani hasa magauni ya harusi. Anaongeza kuwa kwa kupitia onesho la Swahili Fashion alijitangaza zaidi na kuimarisha biashara zake na kwa sasa anashona gauni moja la harusi kwa Sh 800,000 huku nguo ya kawaida ya kima cha chini ni Sh 50,000.

“Kwa kawaida natumia wiki mbili kukamilisha gauni la harusi na ambalo linakuwa imara na lenye mvuto na kwa sasa ubunifu wa mavazi hapa nchini ni biashara ambayo nadhani inatakiwa kutazamwa kwa jicho la pili kwa kuwa inaweza kuwa na faida sio tu kwetu lakini hata kwa nchi pia,”anasema Zamda.

Katika onesho la mwaka huu pia kulikuwa na utoaji wa tuzo kwa washindi wa vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na masuala ya mavazi. Tasnia ya uanamitindo ikiwa ni tasnia ambayo ipo karibu zaidi na ubunifu wa mavazi nayo pia kulikuwa na shindano la kutafuta wanamitindo bora wa kike na kiume.

Kwa upande wa kipengele cha Mwanamitindo bora wa kiume, nafasi ilichukuliwa na Lota Mollel huku wa kike ikichukuliwa na Winfrida Ngonyani. Akizungumza na gazeti hili, Winfrida ambae aliwahi kuwa Miss Universe mwaka jana anasema kuwa kwake kupitia Swahili Fashion anajiongezea fursa mbalimbali za kipato.

“Mimi ninaona kuwa Swahili Fashion imenifungulia njia kwa kiasi fulani kwa kuwa ninapata fedha mbili tatu kama mwanamitindo lakini pia nimejiongezea wigo wa kufanya kazi mbalimbali na watu tofautitofauti,”anasema Winfrida. Moja kati ya vipengele 18 vilivyoshindaniwa katika tuzo hizo ni pamoja na Mbunifu Bora Chipukizi ambapo mwanadada kutoka Kenya Bhoke Samuel alishinda.

Katika kipengele cha mbunifu chipukizi kama hicho pia kiliwahi kushindaniwa miaka ya nyuma na wabunifu walioshinda wengi wao wameendelea kufanya vema zaidi hadi mwaka huu. Mfano mzuri ni Grace Kijo ambae aliwahi kushiriki mwaka 2009 kama mbunifu chipukizi lakini kwa mwaka huu 2013 ameingia pia kama mbunifu mkubwa na kuonesha nguo nzuri.

Anasema kuwa kwa mwaka anabuni zaidi nguo za kike na kuongeza kuwa anajipanga kuhakikisha kuwa anatumia jukwaa la Swahili Fashion kufika mbali zaidi katika tasnia ya ubunifu.

“Kwa kuwa kwa sasa nikijilinganisha na miaka ya nyuma naona kuwa nimepiga hatua na ndio maana mwaka huu hata ukiangalia na miaka iliyopita kwa mwaka huu kazi yangu inaonekana kuwa imeimarika zaidi,” anasema Grace. Katika onesho la Swahili Fashion la mwaka huu wabunifu wengi walionekana kuendelea kukipa kitenge nafasi zaidi kwa kukitumia katika kunakshi kazi zao za sanaa.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi