loader
Dstv Habarileo  Mobile
Taaluma ya mipango, usimamizi kete muhimu kwa maendeleo

Taaluma ya mipango, usimamizi kete muhimu kwa maendeleo

George Hawasii ni Mkurugenzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Kanda ya Ziwa anasema katika mahafali ya pili ya chuo hicho kuwa Serikali ina nia ya dhati katika kukuza na kuendeleza taaluma ya mipango na usimamizi wa maendeleo kwa wananchi.

Anasema Serikali inafanya hivyo ili utekelezaji wa mipango ya maendeleo ifanyike kwa umakini na ufanisi mkubwa na hatimaye kufanikisha Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa. Katika kuyafikia Matokeo Makubwa Sasa, Mkuu wa Chuo hicho, Constantine Lifuliro anasema kumekuwepo na kasi ya ongezeko la uhitaji wa wadau wa maendeleo katika kutumia huduma zitolewazo na kituo hicho cha Kanda ya Ziwa.

Chuo kipo kwenye mchakato wa kujenga majengo yake ya kudumu baada ya kupata eneo lenye ukubwa wa ekari 19 katika maeneo ya Kiseke Manispaa ya Ilemela, jijini Mwanza. Hivi sasa chuo hicho hasa katika kituo cha Kanda ya Ziwa kipo katika majengo ya kukodi ya Kanisa la AICT Bwiru.

Uongozi wa Chuo umeonesha jitihada za kuongeza ukubwa wa eneo ili liweze kuwa na nafasi ya kutosha kuwahudumia wananchi wa Kanda ya Ziwa ambapo katika mahafali ya kwanza tulielezwa kuwepo kwa hekta 7.3 katika eneo hilo hilo la Kiseke Tayari uongozi wa Chuo umekamilisha ununuzi wa kiwanja hicho na kinatarajia kuanza kujenga majengo ya kudumu yatakayogharimu kiasi cha Sh bilioni 53 hadi kukamilika kwake kwa kuandika andiko la mradi.

Ujenzi wa chuo kituo hicho ambacho makao makuu yake yapo Dodoma utakuwa wa awamu mbili kwa miaka mitatu mitatu, awamu ya kwanza itagharimu kiasi cha Sh bilioni 30 itahusisha ujenzi wa jengo la taaluma, mabweni mawili ya wanafunzi, zahanati, kantini na miundombinu ya barabarani ili kufanya kituo kiweze kufikika kwa urahisi.

Lifuliro anasema awamu ya pili itagharimu kiasi cha Sh bilioni 23 itahusisha ujenzi wa ukumbi wa shughuli mbalimbali, mabweni mawili ya wanafunzi, jengo la utawala, maktaba, nyumba nne za wafanyakazi pamoja na ujenzi wa mandhari ya chuo.

Tayari andiko la mradi limewasilishwa Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa ajili ya kutafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Kituo cha Mwanza kilizinduliwa Desemba 14, 2012 na kwamba kilianzishwa ili kuweza kusogeza huduma kwa wadau wa mipango ya maendeleo hasa watumishi wa Serikali katika ngazi za zote zikiwemo za wilaya, kata, vijiji na wadau wa maendeleo.

Kituo hicho kilianza mwaka 2010 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya chuo kama yalivyoainishwa na sheria ili kukidhi matakwa ya wadau wa maendeleo katika kanda hii “Ni wazi kuwa uhitaji wa wadau kwa taaluma inayotolewa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijiji- Kituo cha Mwanza unazidi kuongezeka kila mwaka kwani kilipoanza kilidahili wanafunzi 323 katika programu ya Stashahada katika mipango ya Maendeleo vijijini katika mwaka wa masomo 2011/12,” alisema.

Katika mwaka wa masomo 2012/13 jumla ya wanafunzi 674 walidahiliwa kati yao 422 walikuwa wa programu ya astashahada katika mipango ya maendeleo vijijini na 252 walikuwa wa programu ya Stashahada katika mipango ya maendeleo.

Katika mwaka wa masomo 2013/14 idadi ya wanafunzi waliodahiliwa wanafika 1,055 wakiwemo wanwake 510 sawa na asilimia 48.3 na wanaume 545 sawa na asilimia 51.7, waliodahiliwa mwaka huu ni mara tatu ya wanafunzi waliodahiliwa wakati chuo kilipoanzishwa.

Sambamba na utoaji mafunzo ya muda mrefu pia kituo kimekuwa kikiendesha mafunzo ya muda mfupi ambayo yameongeza ujuzi, ufahamu na mtazamo kwa washiriki hususan Maofisa watendaji wa Serikali, viongozi wa vikundi vya kijamii na viongozi wa asasi zisizo za kiserikali.

Ernest Masanja ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Machinga (SHIUMA), ni miongoni mwa wadau walioshiriki mafunzo ya muda mfupi anasema kwao wao kama machinga wa jijini Mwanza wamesoma kozi fupi ya kutatua migogoro baina yao na Serikali.

Anasema machinga wamekuwa wakijiendesha wenyewe kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji, na Polisi na kwamba katika kozi hiyo wamefundishwa namna ya kubuni miradi mbalimbali, kuendesha shughuli zao na suala zima la hisa.

Dk Primus Nkwera ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi, anamwakilisha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kwenye mahafali ya Pili ya Chuo hicho kituo cha Mwanza anasema Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya kituo. Pia itakiwezesha kituo kupata vitendea kazi na rasilimali watu inayohitajika ili shughuli zinazofanywa na kituo ziwe endelevu.

“Ninatambua ukweli kuwa matokeo mazuri ya wahitimu yanatokana na mambo mengi ikiwa ni pamoja na mazingira rafiki ya kusomea hivyo Serikali itashirikiana bega kwa bega katika kuhakikisha kituo kinafikia malengo yake,” anasema Nkwera. “Nia ya Serikali ni kuona chuo kinafanikisha mambo yote kama yaliyokusudiwa kulingana na malengo ya kuanzishwa kwa kituo cha Kanda ya Ziwa kwani maendeleo halisi ni yale yanayolenga vijijini ambako kuna asilimia kubwa ya umma wa Watanzania,” anasema.

Kituo cha mafunzo cha Kanda ya Ziwa kinaendelea kukua na kuimarika kwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kufanya utafiti na kutoa ushauri elekezi kwa wadau mbalimbali hapa nchini. “Jitihada hizi zinaendeleza jukumu la msingi la chuo kufikisha utaalam wa mipango ya maendeleo vijijini kwa kutoa wataalamu mahiri wa ngazi mbalimbali wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya kiushindani katika dunia ya utandawazi,” anasema.

Kuanzishwa kwa Kituo cha Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini-Kanda ya Ziwa ni hatua kubwa ya kimaendeleo ya chuo inayolenga kupanua taaluma ya mipango na usimamizi wa maendeleo kwa wadau wengi zaidi. Taifa lipo kwenye kutekeleza hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa umakini ili kupata Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta za umma na binafsi.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Grace Chilongola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi