loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Taasisi ya Clinton yakabidhiwa shamba la mbegu

Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 1,058 liko katika Kijiji cha Isuka Lukani, wilayani Kilolo, mkoani Iringa likizalisha mbegu za mahindi, maharage, soya, alizeti na ngano.

Katika makabidhiano hayo Serikali iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi na CDI iliwakilishwa na Mtendaji Mkuu wake, Walker Morris.

“Nimeruka kutoka New York Marekani hadi Kilolo Iringa ili nishiriki tukio hili muhimu; tukio hili linafanyika baada ya kiongozi wetu mkuu wa taasisi hii Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton na mwanawe Chelsea Clinton Agosti mwaka jana kushuhudia mkataba wa makubaliano,” alisema.

Alisema dhima yao katika makubaliano hayo ni kuona wakulima wanaongeza tija katika shughuli zao za kilimo.

“Tunataka kuona wakulima wanazalisha zaidi, wanapata masoko yenye bei nzuri na wanafurahia kilimo kwa kupata faida zaidi,” alisema.

Awali mwakilishi wa taasisi hiyo nchini, Michael Fredericksen alisema wanataka kufanya shamba hilo kuwa kituo kikuu cha uzalishaji kitakachotoa mafunzo ya matumizi ya mbegu bora kwa wakulima.

Fredericksen alisema teknolojia ya kisasa yakiwemo matumizi ya zana bora za kilimo na ujenzi wa maabara ya upimaji wa udongo vitawekezwa katika shamba hilo.

“Uzalishaji rasmi wa mbegu tunatarajia kuanza msimu ujao wa kilimo,” alisema na kuhakikisha kwamba kila ekari moja ya mahindi wanataka wazalishe gunia 40 hadi 45.

Akizungumzia madhumuni ya ubia, Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Zambi alisema “ni uzalishaji wa mbegu bora zitakazomuondoa mkulima kwenye kilimo cha mazoea cha matumizi ya mbegu za kienyeji kila mwaka.”

Alisema matumizi ya mbegu za kienyeji yameendelea kupunguza tija katika kilimo na akawataka Watanzania kutumia fursa ya ubia huo kubadili mfumo wao wa uzalishaji.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu Nchini (ASA), Dk Firmin Mizambwa alisema katika hafla hiyo kwamba ni asilimia 15 hadi 20 ya wakulima wote nchini wanaotumia mbegu bora. Alisema ubia huo unatarajiwa kuharakisha mapinduzi ya ukuaji wa sekta ya kilimo ambacho ni tegemeo kwa wananchi walio wengi.

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi