loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Taifa Stars sikio la kufa

Ikihitaji ushindi dhidi ya Msumbiji (Black Mambas), Tanzania ‘Taifa Stars’ ilijikuta ikifungwa mabao 2-1 kwenye mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto mjijni Maputo.

Katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stars ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na hivyo kuhitaji ushindi jana, lakini ikafungwa na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-3.

Kwa kushindwa huko, Stars imekosa nafasi ya kuingia katika hatua ya mwisho ya mchujo ambayo ni makundi na ingekuwa katika Kundi F lenye timu za Zambia, Cape Verde na Niger, kupata timu za kufuzu kwa fainali za mwakani zilizopangwa kufanyika Januari nchini Morocco.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Maputo, Stars ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 kufikia dakika 15 kabla ya pambano kumalizika, kabla ya Mbwana Samata kufunga bao la kusawazisha, ambalo halikudumu dakika nyingi, kwani Msumbiji waliongeza bao jingine na kufifisha matumaini ya Stars.

Akizungumza juzi kabla ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Stars, Mart Nooij, alisema anakiamini kikosi chake na kwamba kitapigana kuhakikisha kinapata ushindi.

“Nakiamini kikosi changu kitacheza vizuri zaidi kuliko kilivyofanya Dar es Salaam kwa vile hakitakuwa katika shinikizo la mashabiki ambalo mara nyingi hufanya wachezaji wasijiamini,” alisema Mholanzi huyo ambaye aliwahi kuwa kocha wa Msumbiji.

Kocha Nooij alifanya mabadiliko mawili katika kikosi kilichoanza Dar es Salaam kwa kuwaweka benchi winga Mrisho Ngassa na beki Oscar Joshua na kuanza na Saidi Moradi na Mcha Khamis ambaye aliingia katika mechi ya kwanza badala ya Ngassa na kufunga mabao yote mawili.

Mholanzi huyo alianza na Deogratias Munishi, Moradi, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Thomas Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Samata na Mcha.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilifanya maandalizi yake mkoani Mbeya na kisha kwenda nchini Afrika Kusini kwa siku mbili kabla ya kutua Maputo, Ijumaa jioni. Stars ilifika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya mabao 2-2 Harare.

Tanzania imefuzu Afcon mara moja tu mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria, wakati Msumbiji imecheza fainali nne za michuano hiyo katika miaka ya 1986, 1996, 1998 na 2010, zote wakitolewa hatua ya makundi kama Taifa Stars.

Katika mechi nyingine juzi, Malawi, Rwanda na Botswana zilifuzu kwa hatua hiyo ya makundi baada ya kushinda mechi zao dhidi ya Benin, Congo na Guinea Bissau.

Malawi ikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Benin katika mechi ya kwanza, ilisawazisha bao hilo nyumbani kwake na kwenda sare ya bao 1-1 na hivyo kupigiana penalti na The Flames inayofundishwa na Young Chimodzi ilishinda kwa penalti 4-3 huku nyota wa Benin, Stephane Sessegnon wa Sunderland akikosa.

Malawi itakuwa Kundi B pamoja na Mali, Ethiopia na Algeria. Kwa upande wao, Rwanda ‘Amavubi’ ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Congo Brazzaville ilipata ushindi wa mabao 2-0 mjini Kigali yaliyofungwa na Michel Ndahinduka na Meddy Kagere, kabla ya kushinda kwa penalti 4-3.

Itakuwa Kundi A pamoja na Nigeria, Afrika Kusini na Sudan. Botswana ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya sare ya bao 1-1 mjini Conakry huku ikijivunia ushindi wake wa mabao 2-0 Gaborone.

Imeingia katika Kundi G pamoja na Misri, Tunisia na Senegal. Sierra Leone imesonga mbele baada ya Shelisheli kuikatalia kuingia kwao kwa kuhofia maambukizi ya ebola na sasa itaingia Kundi D pamoja na Cameroon, Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Uganda ilikuwa ugenini kucheza na Mauritania ikijivunia ushindi wa mabao 2-0.

KLABU ya Simba  imetambulisha  mashindano mapya ya Super  Cup, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi