loader
Dstv Habarileo  Mobile
TAMASHA LA MICHEZO KARATU: Waandaaji waumiza vichwa kuliboresha

TAMASHA LA MICHEZO KARATU: Waandaaji waumiza vichwa kuliboresha

Taasisi ya Filbert Bayi Foundation (FBF) ndio inayoandaa tamasha hilo la kila mwaka, ambalo limekuwa likidhaminiwa na Olympic Solidarity, lengo likiwa ni kuibua na kuviendeleza vipaji vya wanariadha chipukizi wa mji huo wa Karatu.

Bayi alianzisha tamasha hilo ili kusaka vipaji vya chipukizi ambao baadaye watarithi mikoba yake iliyomfanya kuvunja rekodi ya dunia mwaka 1974 ya mbio za mita 1,500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Christchurch, New Zealand.

Kwanini Karatu?:

Bayi ni mzaliwa wa eneo hilo la Karatu ambalo ni moja ya wilaya za Mkoa wa Arusha na sehemu ambayo amekulia na pia ndiko alikoanzia kukimbia. Mkoa wa Arusha hasa ukanda wa Karatu ndiko kwenye vijana wengi wenye vipaji vya mchezo wa riadha, hivyo Bayi aliona ni mahali muafaka kuanzisha tamasha hilo ili kuwasaka akina Bayi wapya.

Ni miaka 40 sasa tangu Bayi avunje rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 ambayo miaka mitano baadaye rekodi hiyo ilivunjwa na Muingereza Sebastian Coe, ambaye hakudumu sana na rekodi hiyo. Lakini kwa upande wa Michezo ya Jumuiya ya Madola, Bayi bado ndiye anayeshikilia rekodi hiyo aliyoiweka miaka 40 iliyopita wakati tukielekea katika Michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Scotland mwaka huu.

Michezo Mingine:

Awali, tamasha hilo lilikuwa likishirikisha mchezo wa riadha tu, lakini miaka ilivyozidi kwenda waandaaji waliamua kuongeza michezo mingine ili kuibua vipaji vya wachezaji wa michezo mingine. Michezo kama mbio za baiskeli, mpira wa wavu, soka, pamoja na ngoma na kwaya viliongezwa na kuongeza msisimko katika tamasha hilo la kila mwaka.

Pamoja na kuongezwa kwa michezo hiyo, lakini mchezo wa riadha wa kilometa 10 kwa wanaume, kilometa tano kwa wanawake na 2.5 kwa watoto kulizidi kuufanya mchezo huo kuwa maarufu zaidi katika tamasha hilo. Kwa upande wa washiriki mchezo wa riadha kuanzia ule wa wanaume, wanawake na watoto yote ilisheheni washiriki kibao na kuufanya mchezo huo kupendwa zaidi katika tamasha hilo.

Tamasha la Mwaka Huu:

Mbali na mbio za kawaida za kilometa 10, tano na zile za watoto za kilometa 2.5, ambazo mwaka huu kwa mara ya kwanza ziliwatenganisha watoto wa shule za msingi na sekondari, pia kulikuwa na mchezo wa soka, mpira wa wavu, baiskeli, ngoma na kwaya.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa FBF, Bayi washiriki wa tamasha hilo wamekuwa wakipungua mwaka hadi mwaka, kitu ambacho hata yeye hajui kwa nini na kinamsikitisha sana.

Bayi aliwachongea viongozi wa michezo wa Karatu kwa Mkuu wao wa Wilaya Daud Mtibenda, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa tamasha hilo, ambalo pia lilihudhuriwa na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Ghullam Rashid na wajumbe wa kamati hiyo Seleman Jabir pamoja na Suleiman Ame.

Michezo kama ya soka na wavu imekuwa ikichezwa kuanzia vitongojini ili kuwasaka wakali watakaoshindana katika fainali na kumpata bingwa wa mchezo huo. Washindi hupata zawadi za fedha taslimu au vifaa vya michezo kama mipira, nyavu, jezi na filimbi ili kuzisaidia timu zao ambazo nyingi huwa na tatizo la upungufu wa vifaa vya michezo.

Kwa upande wa mchezo wa mbio za baiskeli, mwaka huu ilikuwa tofauti kwani washiriki wengi walikuwa wakitumia baiskeli za kisasa tofauti na huko nyuma ambako wengi wakitumia baiskeli za kawaida.

Mkuu wa Wilaya:

Mkuu huyo wa Wilaya wakati akijibu risala ya Bayi kuhusu uchache wa washiriki kila miaka inavyozidi kwenda, aliwataka vijana kujitokeza zaidi katika michezo na kuwaamuru wale wote waliovamia viwanja vya michezo kuvirejesha haraka.

Alisema kuwa agizo lake la awali la kuwataka waliochukua viwanja vya michezo kuvirejesha, halikuwahi kutekelezwa hivyo aliwataka maofisa utamaduni kufuatilia suala hilo haraka na kumpelekea taarifa. Amri hiyo ya Mkuu wa Wilaya ilipokewa kwa furaha wananchi wa Karatu waliojitokeza kwa wingi kushuhudia ufungaji huo wa tamasha ambao ulifana sana.

Washindi wa Tamasha:

Kwa upande wa baiskeli, Tom holden, Deni Julius na Paulo Didas wote wa Arusha walishika nafasi tatu za kwanza kwa kutumia muda wa saa 1:46:24:47, 1:47:27:03 na 1:47:41:43. Katika mbio za kilometa 10 wanaume, Wilbert Peter wa Chuo cha Polisi Moshi (CCP) alitamba Catherine Range wa Magereza Arusha aliibuka mshindi katika mbio za kilometa tano kwa upande wa wanawake.

Kwa upande wa mbio za kilometa 10 kwa wanaume, Peter aliibuka wa kwanza kwa kutumia dakika 30:58.34 huku John Leonard alishika nafasi ya pili kwa kutumia dakika 31:17.82 na joseph Teophil wa Guwang alimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 31:23.95.

Kwa upande wa akinadada waliotimua mbio kwa umbali wa kilometa tano, Range alimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 17:30.81, wakati mwanariadha wa kimataifa Mary Naali alijikuta akimaliza wa pili licha ya kuongoza mbio hizo kwa muda mrefu alipotumia dakika 17:31.07 na Angelina Tsere aliibuka watatu kwa kutumia dakika 17:57.78.

Katika mbio za kilometa 2.5 kwa upande wa wanafunzi wa shule za msingi kwa wasichana, Elizaberth Renald (13) aliibuka mshindi kwa kutumia dakika 09:36.04, huku Jasmin Hamad (13) alishika nafasi ya pili kwa kutumia dakika 09:56.68 na Neema Faraji alikuwa watatu kwa kutumia dakika 09:59.03.

Kwa upande wa wavulana katika mbio hizo, Baraka Sebastian (14) alimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 08:27.82 wakati James Francis aliibuka wa pili kwa kutumia dakika 08:27.67 na Jacob Elisante alishika nafasi ya tatu kwa dakika 09:00.09. Mwaka huu waandaaji wa tamasha hilo waliongeza zawadi za washindi na kuwafanya walioibuka na ushindi kwenda majumbani kwao wakiwa na vitita vya pesa.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi