loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Tanesco kufumuliwa

Akizungumza hivi karibuni katika semina ya wiki moja ya viongozi wa Kamati ya Majadiliano ya Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma za Ushauri (TUICO), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisema pia vitengo muhimu vitatu vitatenganishwa.

“Mfumo wa Tanesco uliopo kwa sasa, umechangia uendeshaji wake kutokidhi mahitaji na matarajio ya Watanzania kwenye sekta ndogo ya umeme. “Serikali imeona iandae mkakati na mwelekeo wa kurekebisha sekta ndogo ya umeme, ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa Shirika la Tanesco,” alisema Maswi.

Katika mkakati huo unaohusu pia kupunguza bei ya umeme, Serikali inakusudia kuongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma hiyo kwa sasa ya asilimia 36 hadi kufikia 75 kufikia mwaka 2025, huku idadi ya waliounganishiwa umeme ikiongezeka kutoka asilimia 24 za sasa hadi kufikia asilimia 50.

Vitengo

Kuanzia Julai 2014 hadi Juni 2015, Maswi alisema muundo wa Tanesco utaendelea kubakia kama ulivyo sasa. Aliweka bayana kuwa kuanzia Julai 2015 hadi Juni 2018, Idara ya Uzalishaji Umeme itatenganishwa kutoka Idara ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme na maboresho hayo yanatakiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.

Kati ya Julai 2018 na Juni 2021, Maswi alisema Idara ya Usambazaji Umeme itatenganishwa na Idara ya Usafirishaji wa Umeme na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2021.

Kampuni

Kuhusu kampuni hizo, Maswi alisema sehemu hiyo ya maboresho itachukua muda mrefu kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2025, ambapo ofisi za Kanda za Tanesco, zitabadilishwa na kuwa kampuni zinazojitegemea za usambazaji umeme kulingana na mahitaji ya soko la umeme kwa wakati huo.

Kwa sasa Tanesco ina kanda tano, ambazo ni Kanda ya Nyanda za Juu-Kusini Magharibi, Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha, Kanda ya Kati, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani na Kanda ya Ziwa.

Tayari mkakati huo umeshapitiwa na Serikali June mwaka huu na umekubaliwa kutekelezwa kwa miaka hiyo 11, kuanzia June mwaka huu hadi mwaka 2025.

Usalama wa ajira

Maswi aliwatoa hofu watumishi kwa kusema ajira na maslahi yao yatalindwa wakati wa utekelezaji wa mkakati wa maboresho hayo.

Alisema, katika kutekeleza mpango huo, kutakuwa na mpango maalumu wa kuendeleza rasilimali watu ndani ya Tanesco, kwa kuwa matarajio ni pamoja na kuongezeka kwa kazi zitakazotokana na mgawanyiko mkubwa wa majukumu.

“Katika mpango huu, wafanyakazi mnahakikishiwa usalama wa ajira na stahiki za mikataba yenu. Tanesco bora itajengwa na waliopo ndani kwa kukubali mabadiliko ya kujijenga upya,” alisema Maswi.

Kiini cha mabadiliko

Maswi alisema mfumo wa sasa unaosimamia sekta ya umeme, una changamoto nyingi zinazojumuisha kuwepo kwa ufinyu wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Changamoto nyingine aliyoitaja, ni muundo mdogo wa sekta hiyo ambao haukidhi soko la umeme sambamba na uwezo mdogo wa uzalishaji wa umeme.

Pia alisema sekta hiyo bado ina tatizo la ushiriki mdogo wa sekta binafsi katika uwekezaji na uchakavu wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, unaosababisha upotevu wa umeme.

Tatizo lingine linalokabili sekta hiyo kwa mujibu wa Maswi, ni uhujumu katika miundombinu na utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kuwekeza.

Malengo

Lengo kubwa la kuboresha muundo wa Tanesco, Maswi alisema ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika, wenye ubora na kwa bei nafuu, ikiwa ni pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja.

Malengo mengine ni pamoja na kuimarisha ufanisi, utawala bora na utendaji katika utoaji wa huduma, kuvutia wawekezaji binafsi kwenye sekta hiyo na kuhakikisha upatikanaji wa umeme unakuwa wenye ubora na uhakika.

Katika hayo, alisema Serikali imedhamiria kuongeza uwekezaji kutoka sekta binafsi na umma, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kujenga uchumi wa Taifa, kupunguza upotevu wa umeme katika miundombinu iliyopo na kuanzisha soko huru la nishati ya umeme lenye ushindani.

Wafanyakazi

Baada ya kufafanua namna shirika hilo litakavyofumuliwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano wa TUICO – Tawi la Tanesco, Abdul Mkama, aliiomba Serikali kuhakikisha bei ya umeme inakuwa rafiki kwa Mtanzania wa pato la chini.

Alisema endapo bei ya umeme itaendelea kuwa ya juu, mkakati huo wa kurekebisha sekta ndogo ya umeme nchini, hautakuwa na faida kwani licha ya umeme kuwa wa kutosha, bado wananchi hawataweza kunufaika na mageuzi hayo.

Kupungua kwa bei hiyo ya umeme kunatarajiwa kuanza kuonekana baada ya kubadilisha mitambo ya ufuaji wa umeme, kutoka kutumia mafuta mazito na dizeli, kwenda kutumia gesi asilia.

Inatarajiwa baada ya kuanza kutumika kwa gesi mwakani katika mitambo ya kufua umeme, Tanesco inunue umeme kutoka kampuni za ufuaji umeme kwa dola za Marekani senti zisizozidi 8, na kufanya nishati hiyo bei yake kushuka kwa mwananchi mmoja mmoja.

Kwa sasa kwa mujibu wa takwimu za Tanesco, wateja wa majumbani, uniti moja ya umeme inauzwa kwa dola za Marekani senti 19, kwa wateja wa biashara senti 13 na viwanda vya kati na vikubwa senti 10 huku umeme wa taa za barabarani ukiwa senti 19.

Tanesco inauza umeme wake kwa bei hiyo, kwa kuwa imekuwa ikilazimika kununua umeme unaofuliwa kwa dizeli na mafuta mazito kutoka kwa wafanyabiashara kwa kati ya senti za Marekani 33 na 50.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi